< Yeremia 19 >
1 Hili ndilo asemalo Bwana: “Nenda ukanunue gudulia la udongo kutoka kwa mfinyanzi. Wachukue baadhi ya wazee wa watu na wa makuhani
Bwana akasema hivi, “Nenda ukanunue chupa ya udongo wakati ukiwa na wazee wa watu na makuhani.
2 na mtoke mwende mpaka kwenye Bonde la Ben-Hinomu, karibu na ingilio la Lango la Vigae. Huko tangaza maneno ninayokuambia,
Kisha uende mpaka bonde la Ben Hinomu wakati wa kuingia kwenye mlango uliovunjika wa mfinyanzi, na huko utangaza maneno nitakayokuambia.
3 nawe useme, ‘Sikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda na watu wa Yerusalemu. Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Sikilizeni! Nitaleta maafa mahali hapa, ambayo yatafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yawashe.
Ukisema, 'Sikilizeni neno la Bwana, wafalme wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu! Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, “Tazameni, na nitaletea msiba juu ya mahali hapa, na masikio ya kila mtu anayesikia yatawaka.
4 Kwa kuwa wameniacha na kupafanya mahali hapa kuwa pa miungu ya kigeni. Wameiteketezea sadaka miungu ambayo wao wala baba zao wala wafalme wa Yuda kamwe hawakuijua, nao wamelijaza eneo hili kwa damu isiyo na hatia.
Nitafanya hivyo kwa sababu wameniacha na kudharau mahali hapa. Katika mahali hapa wanatoa sadaka kwa miungu mingine ambayo hawakuijua. Wao, baba zao, na wafalme wa Yuda pia wamejaza mahali damu isiyo na hatia.
5 Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia miungu pa Baali ili kuteketeza wana wao katika moto kama sadaka kwa Baali, kitu ambacho sikukiamuru wala kukitaja, wala hakikuingia akilini mwangu.
Walimjengea Baali mahali pa juu na kuwachoma watoto wao kwa moto kama sadaka za kuteketezwa kwake-kitu ambacho sijawaamuru au kutaja, wala hakuingia ndani ya akili yangu.
6 Hivyo jihadharini, siku zinakuja, asema Bwana, wakati watu hawatapaita tena mahali hapa Tofethi ama Bonde la Ben-Hinomu, bali Bonde la Machinjo.
Kwa hiyo, tazama, siku zinakuja-hili ndilo tamko la Bwana-ambapo mahali hapa hapataitwa tena Tofethi, bonde la Ben Hinomu, kwa kuwa litakuwa bonde la machinjo.
7 “‘Nitaiharibu mipango ya Yuda na Yerusalemu mahali hapa. Nitawafanya waanguke kwa upanga mbele ya adui zao, katika mikono ya wale watafutao uhai wao, nami nitaitoa mizoga yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.
Katika mahali hapa nitatamgua mipango ya Yuda na Yerusalemu. Nitawafanya wapate kuuawa kwa upanga mbele ya adui zao na kwa mkono wa wale wanaotafuta maisha yao. Ndipo nitawapa miili yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa dunia.
8 Nitauharibu mji huu na kuufanya kitu cha kudharauliwa. Wote wapitao karibu watashangaa na kuudhihaki kwa sababu ya majeraha yake yote.
Ndipo nitaifanya mji huu kuwa uharibifu na kitu cha kuzomewa, kila mtu anayepita atashangaa na kuzomea kwa sababu mateso yake yote.
9 Nitawafanya wao kula nyama ya wana wao na binti zao; kila mmoja atakula nyama ya mwenzake wakati wa dhiki ya kuzungukwa na jeshi lililowekwa juu yao na adui wanaotafuta uhai wao.’
Nitawafanya wale nyama ya wana wao na binti zao; kila mtu atakula mwili wa jirani yake katika dhiki na katika uchungu ambao umeletwa kwao na maadui zao na wale wanaotaka maisha yao.'”
10 “Kisha livunje lile gudulia wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia,
Kisha utavunja chupa ya udongo mbele ya watu ambao walikwenda pamoja nawe.
11 uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi.
Uwaambie,'Bwana wa majeshi asema hivi: nitafanya jambo hili kwa watu hawa na mji huu- hii ndiyo ahadi ya Bwana, kama vile Yeremia alivyovunja chupa ya udongo ili isiweze kutengenezwa tena. Watu watazika wafu huko Tofethi hata hapatabaki mahali pa kuzika.
12 Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale waishio ndani yake, asema Bwana. Nitaufanya mji huu kama Tofethi.
Hivyo ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na wenyeji wake nitakapofanya jiji hili kama Tofethi, hili ndio tamko la Bwana;
13 Nyumba zilizoko Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, Tofethi: yaani nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani, na kumimina dhabihu za vinywaji kwa miungu mingine.’”
kwa hiyo nyumba za Yerusalemu na wafalme wa Yuda watakuwa kama Tofethi, nyumba zote zilizo juu ya watu waovu wanaoabudu nyota zote za mbinguni na kumwaga sadaka za kinywaji kwa miungu mingine.'”
14 Kisha Yeremia akarudi kutoka Tofethi, mahali ambapo Bwana alikuwa amemtuma kutoa unabii, akasimama katika ua wa Hekalu la Bwana na kuwaambia watu wote,
Ndipo Yeremia akatoka Tofethi, ambako Bwana amemtuma ahubiri. Akasimama katika ua wa nyumba ya Bwana, akawaambia watu wote,
15 “Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya mji huu pamoja na vijiji vinavyouzunguka kila maafa niliyosema dhidi yake, kwa sababu wamekuwa na shingo ngumu, na hawakuyasikiliza maneno yangu.’”
“Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazameni, nitawaletea mji huu na miji yake yote maafa yote niliyonena dhidi yake, kwa kuwa walifanya shingo zao kuwa ngumu na kukataa kusikiliza maneno yangu.'”