< Yeremia 18 >

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana:
Neno la Bwana lilimjia Yeremia, kusema,
2 “Shuka uende mpaka nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu.”
“Simama, uende kwa nyumba ya mfinyanzi; kwa maana nitakusikilizisha neno langu huko.
3 Kwa hiyo nikashuka mpaka kwenye nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake.
Basi, nikaenda nyumbani kwa mfinyanzi, na tazama! Mfinyanzi alikuwa akifanya kazi kwenye gurudumu la mfinyanzi.
4 Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake, hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kama vile ilivyoonekana vyema kwake yeye.
Lakini chombo cha udongo ambacho alikuwa akikifinyanga kiliharibika mkononi mwake, kwa hiyo alibadili mawazo yake na akafanya kitu kingine ambacho kilionekana kuwa kizuri machoni pake.
5 Kisha neno la Bwana likanijia kusema:
Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,
6 “Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?” asema Bwana. “Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ee nyumba ya Israeli.
“Je, siwezi kuwa kama huyu mfinyanzi kwenu, nyumba ya Israeli? Angalia! Kama udongo katika mkono wa mfinyanzi-ndivyo ulivyo mkononi mwangu, nyumba ya Israeli.
7 Ikiwa wakati wowote nikitangaza kuwa taifa au ufalme utangʼolewa, utaangushwa na kuangamizwa,
Kwa wakati mmoja, ninaweza kutangaza jambo fulani juu ya taifa au ufalme, kwamba nitaufukuza, kuuvunja, au kuuharibu.
8 ikiwa lile taifa nililolionya litatubia uovu wake, ndipo nitakapokuwa na huruma, wala sitawapiga kwa maafa niliyokuwa nimewakusudia.
Lakini kama taifa ambalo nimefanya tamko hilo linageuka na kuacha maovu yake, basi nitaghairi nisitende maafa niliyokuwa nimepanga.
9 Ikiwa wakati mwingine nitatangaza kuwa taifa ama utawala ujengwe na kuwekwa wakfu,
Wakati mwingine, ninaweza kutangaza jambo fulani kuhusu taifa au ufalme, kwamba nitaujenga au kuupanda.
10 ikiwa utafanya maovu mbele zangu na hukunitii, ndipo nitakapoghairi makusudio yangu mema niliyokuwa nimeyakusudia.
Lakini ikiwa watafanya mabaya machoni pangu kwa kutosikiliza sauti yangu, basi nitaghairi mema ambayo nilikuwa nimewaambia nitawafanyia.
11 “Basi kwa hiyo waambie watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Tazama! Ninaandaa maafa kwa ajili yenu, nami ninabuni mabaya dhidi yenu. Kwa hiyo geukeni kutoka njia zenu mbaya, kila mmoja wenu, tengenezeni njia zenu na matendo yenu.’
Basi sasa, waambie watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, 'Bwana asema hivi: Tazameni, nitawaangamiza. Mimi ni karibu kufinyanga mabaya dhidi yenu. Tubuni, kila mtu kutoka njia yake mbaya, hivyo njia zako na matendo yako yatakuletea mema.'
12 Lakini wao watajibu, ‘Hakuna faida. Tutaendelea na mipango yetu wenyewe, kila mmoja wetu atafuata ukaidi wa moyo wake mbaya.’”
Lakini watasema, 'Hili halina maana. Tutafanya kulingana na mipango yetu wenyewe. Kila mmoja wetu atafanya mabaya kwa kuufuata uchupavu wa moyo wake.'
13 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana: “Ulizia miongoni mwa mataifa: Ni nani alishasikia jambo kama hili? Jambo la kutisha sana limefanywa na Bikira Israeli.
Kwa hiyo Bwana asema hivi, 'Uliza watu wa mataifa, ambao wamewahi kusikia habari kama hii? Bikira wa Israeli amefanya kitendo cha kutisha.
14 Je, barafu ya Lebanoni iliwahi kutoweka kwenye miteremko yake ya mawe wakati wowote? Je, maji yake baridi yatokayo katika vyanzo vilivyo mbali yaliwahi kukoma kutiririka wakati wowote?
Je, theluji ya Lebanoni imetoka milima yenye miamba juu ya pande zake? Je, mito ya mlima inayotoka mbali iliharibiwa, mito hiyo ya baridi?
15 Lakini watu wangu wamenisahau mimi, wanafukizia uvumba sanamu zisizofaa kitu, zilizowafanya wajikwae katika njia zao na katika mapito ya zamani. Zimewafanya wapite kwenye vichochoro na kwenye barabara ambazo hazikujengwa.
Hata hivyo watu wangu wamesahau. Wamefanya sadaka kwa sanamu zisizo na maana na wamefanya mashaka katika njia zao; wameacha njia za kale za kutembea katika njia ndogo.
16 Nchi yao itaharibiwa, itakuwa kitu cha kudharauliwa daima; wote wapitao karibu nayo watashangaa na kutikisa vichwa vyao.
Nchi yao itakuwa ya hofu, kitu cha kuzomewa milele. Kila mtu atakayepita karibu naye atashuhudia na kutingisha kichwa chake.
17 Kama upepo utokao mashariki, nitawatawanya mbele ya adui zao; nitawapa kisogo wala sio uso, katika siku ya maafa yao.”
Nitawaangamiza mbele ya adui zao kama upepo wa mashariki. Nitawageuzia kisogo, wala sio uso wangu, siku ya msiba wao.'”
18 Wakasema, “Njooni, tutunge hila dhidi ya Yeremia; kwa kuwa kufundisha sheria kwa kuhani hakutapotea, wala shauri litokalo kwa mwenye hekima, wala neno la manabii. Hivyo njooni, tumshambulie kwa ndimi zetu na tusijali chochote asemacho.”
Basi watu wakasema, “Njoni, tufanye njama dhidi ya Yeremia, maana sheria haitapotea kabisa kwa makuhani, wala ushauri kutoka kwa wenye hekima, au maneno ya manabii. Njoo, mshambulie kwa maneno yetu na tusisikilize tena chochote anachosema.”
19 Nisikilize, Ee Bwana, sikia wanayosema washtaki wangu!
Sikiliza, Ee Bwana! Na kusikiliza sauti ya adui yangu.
20 Je, mema yalipwe kwa mabaya? Lakini wao wamenichimbia shimo. Kumbuka kwamba nilisimama mbele yako na kunena mema kwa ajili yao, ili wewe ugeuze hasira yako kali mbali nao.
Je, maafa kutoka kwao itakuwa malipo yangu kwa kuwa mema kwao? Kwa maana wamenichimbia shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele yako ili niseme mema kwa ajili yao na kugeuza ghadhabu yako isiwapate.
21 Kwa hiyo uwaache watoto wao waone njaa; uwaache wauawe kwa makali ya upanga. Wake zao wasiwe na watoto, na wawe wajane; waume wao wauawe, nao vijana wao waume wachinjwe kwa upanga vitani.
Basi uwape watoto wao njaa, na uwatie mikononi mwa wale wanaotumia upanga. Basi, waache wanawake wao wafiwe na kuwa wajane, na watu wao watauawa, na vijana wao wauawe kwa upanga wa vita.
22 Kilio na kisikike kutoka kwenye nyumba zao ghafula uwaletapo adui dhidi yao, kwa kuwa wamechimba shimo ili kunikamata na wameitegea miguu yangu mitego.
Kelele ya kusikitisha isikiwe kutoka katika nyumba zao, kama utakapoleta washambuliaji ghafla juu yao. Kwa kuwa wamechimba shimo kunikamata na wameficha mitego katika miguu yangu.
23 Lakini unajua, Ee Bwana, hila zao zote za kuniua. Usiyasamehe makosa yao wala usifute dhambi zao mbele za macho yako. Wao na waangamizwe mbele zako; uwashughulikie wakati wa hasira yako.
Lakini wewe, Bwana, unajua mipango yao yote dhidi yangu ya kuniua. Usisamehe uovu na dhambi zao. Usiondoe dhambi zao mbali nawe. Badala yake, waache waangamizwe mbele yako. Tenda juu yao wakati wa ghadhabu yako.

< Yeremia 18 >