< Yeremia 13 >

1 Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.”
Bwana aliniambia hivi, “Nenda ukape nguo ya kitani na kuiweka karibu na kiuno chako, lakini usiiweke kwenye maji kwanza.”
2 Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama Bwana alivyoniagiza, nikajivika kiunoni.
Kwa hiyo nilinunua vazi kama vile Bwana alivyoagiza, na nikafunga karibu na kiuno changu.
3 Ndipo neno la Bwana likanijia kwa mara ya pili:
Ndipo neno la Bwana likanijia mara ya pili, kusema,
4 “Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.”
“Twaa vazi lako ulilolinunua lililo karibu na kiuno chako, uinuke, ukasafiri mpaka Frati. Ukaifiche huko katika mwamba wa jabali.
5 Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama Bwana alivyoniamuru.
Basi nikaenda na kuificha katika Frati kama vile Bwana alivyoniamuru.
6 Baada ya siku nyingi Bwana akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.”
Baada ya siku nyingi, Bwana akaniambia, “Simama, urudi Frati. Ukaichukue nguo ambayo nilikuambia ufiche.”
7 Hivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa.
Kwa hiyo nikarudi Frati na kuchimba na kuchukua nguo mahali pale nilipoificha. Lakini tazama! Nguo hiyo ilikuwa imeharibika; haikuwa nzuri kabisa.
8 Ndipo neno la Bwana likanijia:
Ndipo neno la Bwana likanijia tena, kusema,
9 “Hili ndilo Bwana asemalo: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu.
“Bwana asema hivi, Nitakiangamiza kiburi cha Yuda na Yerusalemu.
10 Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mkanda huu ambao haufai kabisa!
Watu hawa waovu wanaokataa kusikia neno langu, ambao huenda katika ugumu wa mioyo yao, ambao hufuata miungu mingine ili kuabudu na kuinama-watakuwa kama hii nguo isiyofaa kwa lolote.
11 Kwa maana kama vile mkanda ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyojifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema Bwana, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’
Kwa maana kama vile vazi lililofungwa kwenye viuno vya mtu, ndivyo nimefainya nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda zimefungwa kwangu- hili ndilo tamko la Bwana-wawe watu wangu, ili kunifanya jina, sifa, na heshima. Lakini hawakunisikiliza.
12 “Waambie: ‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Kama wao wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’
Basi uwaambie neno hili, 'Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi Kila chupa itajazwa divai.' Watakuambia, 'Je, hatujui kwamba kila chupa itajazwa divai?'
13 Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: nitawajaza ulevi wote waishio katika nchi hii, pamoja na wafalme waketio juu ya kiti cha enzi cha Daudi, makuhani, manabii na wale wote waishio Yerusalemu.
Basi uwaambie,' Bwana asema hivi: Tazama, nitawajaza kila mkaaji wa nchi hii ulevi, na wafalme wanaokaa kiti cha Daudi, na makuhani, na manabii, na wenyeji wote wa Yerusalemu.
14 Nitawagonganisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema Bwana. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’”
Ndipo nitawagonganisha kila mtu na mwenzake baba na watoto wao pamoja; hili ndilo tamko la Bwana-sitawahurumia au kuwa na huruma, wala sitawarehemu kutoka kwenye uharibifu.
15 Sikieni na mzingatie, msiwe na kiburi, kwa kuwa Bwana amenena.
Sikilizeni na makini. Msiwe na kiburi, kwa kuwa Bwana amesema.
16 Mpeni utukufu Bwana Mungu wenu, kabla hajaleta giza, kabla miguu yenu haijajikwaa juu ya vilima vitakavyotiwa giza. Mlitarajia nuru, lakini ataifanya kuwa giza nene na kuibadili kuwa huzuni kubwa.
Mtukuze Bwana, Mungu wako, kabla ya hajaleta giza, na kabla ya kuifanya miguu yako kuwa na mashaka juu ya milima wakati wa jioni. Kwa maana unatarajia mwanga, lakini ataugeuza kuwa mahali pa giza, na kuwa giza nene.
17 Lakini kama hamtasikiliza, nitalia sirini kwa ajili ya kiburi chenu; macho yangu yatalia kwa uchungu, yakitiririka machozi, kwa sababu kundi la kondoo la Bwana litachukuliwa mateka.
Kwa hiyo ikiwa husikilizi, nitaomboleza peke yangu kwa sababu ya kiburi chako. Hakika macho yangu yatalia na kutoa machozi, kwa sababu kundi la Bwana limechukuliwa mateka.
18 Mwambie mfalme na mamaye, “Shukeni kutoka kwenye viti vyenu vya enzi, kwa kuwa taji zenu za utukufu zitaanguka kutoka vichwani mwenu.”
“Mwambieni mfalme na mama wa malkia, 'Jinyenyekezeni, na kukaa chini, kwa maana taji juu ya kichwa chako, kiburi chako na utukufu wako, umeanguka.'
19 Miji iliyoko Negebu itafungwa, wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua. Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni, wakichukuliwa kabisa waende mbali.
Miji ya Negebu itafungwa, bila mtu wa kufungua. Yuda watachukuliwa mateka, wote uhamishoni.
20 Inua macho yako uone wale wanaokuja kutoka kaskazini. Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa, kondoo wale uliojivunia?
Inua macho yako na angalia wale wanaokuja kutoka kaskazini. Je, ni kundi gani alilokupa, kundi ambalo lilikuwa zuri sana kwako?
21 Utasema nini Bwana atakapowaweka juu yako wale ulioungana nao kama marafiki wako maalum? Je, hutapatwa na utungu kama mwanamke aliye katika utungu wa kuzaa?
Je, unasema nini wakati Mungu anawaweka wale ambao uliwafundisha kuwa marafiki? Je, huu si mwanzo wa maumivu ya utungu ambayo yatakuchukua kama mwanamke aliye katika kuzaa?
22 Nawe kama ukijiuliza, “Kwa nini haya yamenitokea?” Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi ndipo marinda yako yameraruliwa na mwili wako umetendewa vibaya.
Kisha unaweza kusema moyoni mwako, 'Kwa nini mambo haya yanatokea kwangu?' Itakuwa kwa uovu wa maovu yako ambapo marinda yako yamefunuliwa na umeumizwa.
23 Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake au chui kubadili madoadoa yake? Vivyo hivyo nawe huwezi kufanya mema wewe uliyezoea kutenda mabaya.
Je, watu wa Kushi hubadilisha rangi yao ya ngozi, au chui hubadilisha madoa yake? Ikiwa ndivyo, basi wewe mwenyewe, ingawa unazoea uovu, utaweza kufanya mema.
24 “Nitawatawanya kama makapi yapeperushwayo na upepo wa jangwani.
Kwa hiyo nitawaangamiza kama makapi ambayo yanaangamia katika upepo wa jangwa.
25 Hii ndiyo kura yako, fungu nililokuamuria,” asema Bwana, “kwa sababu umenisahau mimi na kuamini miungu ya uongo.
Hii ndiyo niliyokupa, sehemu ambayo nimekuagiza kwako-hili ndilo tamko la Bwana - kwa sababu umenisahau na kuamini katika udanganyifu.
26 Nitayafunua marinda yako mpaka juu ya uso wako ili aibu yako ionekane:
Kwa hiyo mimi mwenyewe nitaondoa nguo zako, na sehemu zako za siri zitaonekana.
27 uzinzi wako na kulia kwako kama farasi kulikojaa tamaa, ukahaba wako usio na aibu! Nimeyaona matendo yako ya machukizo juu ya vilima na mashambani. Ole wako, ee Yerusalemu! Utaendelea kuwa najisi mpaka lini?”
Uzinzi na ubembe wako, aibu ya tabia yako ya uasherati kwenye milima na katika mashamba! Nitayafanya yaonekane, mambo haya ya machukizo! Ole wako, Yerusalemu! Hutaki kuwa safi. Je! Hili litaendelea kwa muda gani?”

< Yeremia 13 >