< Yakobo 3 >
1 Ndugu zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi.
Ndugu zangu, siyo wengi wenu mnapaswa kuwa walimu, mkijua kwamba tutapokea hukumu kubwa zaidi.
2 Sisi sote tunajikwaa katika mambo mengi. Ikiwa mtu yeyote hakosei kamwe katika yale anayosema, yeye ni mkamilifu, naye anaweza kuuzuia pia na mwili wake wote.
Kwa kuwa wote tunakosea katika njia nyingi. Kama yeyote huwa hajikwai katika maneno yake, huyo ni mtu mkamilifu, aweza kudhibiti mwili wake wote pia.
3 Tunapotia lijamu kwenye vinywa vya farasi ili kuwafanya watutii, tunaweza kuigeuza miili yao yote.
Sasa kama tunaweka lijamu za farasi katika vinywa vyao wanatutii, na tunaweza kuigeuza miili yao yote.
4 Au angalia pia meli, ingawa ni kubwa sana, nazo huchukuliwa na upepo mkali, lakini hugeuzwa kwa usukani mdogo sana, kokote anakotaka nahodha.
Tambua pia kwamba meli, ingawa ni kubwa na husukumwa na upepo mkali, zinaongozwa kwa usukani mdogo sana kwenda popote anakotaka nahodha.
5 Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa!
Vivyo hivyo, ulimi ni kiungo kidogo cha mwili, lakini hujisifia makuu sana. Angalia msitu mkubwa unavyoweza kuwashwa kwa cheche ndogo ya moto!
6 Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa jehanamu. (Geenna )
Ulimi pia ni moto, ni ulimwengu wa uovu, umewekwa miongoni mwa viungo vya mwili wetu, ambao hunajisi mwili wote na huiweka juu ya moto njia ya maisha, na wenyewe kuchomwa moto wa kuzimu. (Geenna )
7 Kwa maana kila aina ya wanyama, ndege, wanyama watambaao na viumbe vya baharini vinafugika na vimefugwa na binadamu,
Kila aina ya mnyama wa polini, ndege, kitambaacho na kiumbe cha baharini kinadhibitiwa na wanadamu.
8 lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.
lakini hakuna mwanadamu hata mmoja ambaye anaweza kudhibiti ulimi; ni uovu usiotulia, umejaa sumu ya kufisha.
9 Kwa ulimi tunamhimidi Bwana, yaani Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu.
Kwa ulimi twamtukuza Bwana na Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu.
10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haistahili kuwa hivyo.
Katika kinywa hichohicho husema maneno ya baraka na laana. Ndugu zangu mambo haya hayapaswi kuwa.
11 Je, chemchemi yaweza kutoa katika tundu moja maji matamu na maji ya chumvi?
Je, kisima kimoja huweza kutoa maji matamu na machungu?
12 Je, ndugu zangu, mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Wala chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.
Ndugu zangu, Je, mti wa mtini unaweza kuzaa matunda ya mzeituni, au mzabibu unazaa matunda ya mtini? Wala chemchemi ya maji chumvi haitoi maji yasio na chumvi.
13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima.
Ni nani miongoni mwenu aliye na hekima na ufahamu? Hebu mtu huyo na aoneshe maisha mema katika kazi zake kwa unyenyekevu utokanao na hekima.
14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli.
Lakini kama mnao wivu mkali na nia ya ubinafsi mioyoni mwenu, msijivune na kusema uongo mkiupinga ukweli.
15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani.
Hii siyo hekima ile ishukayo kutoka juu, lakini badala yake ni ya kidunia, si ya kiroho, na ni ya kipepo.
16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.
Kwa kuwa palipo na wivu na ubinafsi upo, kuna vurugu na kila matendo maovu
17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki.
Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, kisha kupenda amani, upole na ukarimu, yenye kujaa rehema na matunda mema, bila kupendelea watu fulani, na kweli.
18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.
Na tunda la haki hupandwa katika amani kwa wale ambao wanatenda mambo ya amani.