< Yakobo 2 >

1 Ndugu zangu, kama waaminio katika imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe na upendeleo kwa watu.
Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe.
2 Kwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa,
Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu.
3 nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,”
Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: “Keti hapa mahali pazuri,” na kumwambia yule maskini: “Wewe, simama huko,” au “Keti hapa sakafuni miguuni pangu,”
4 je, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu?
je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?
5 Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao?
Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala aliowaahidia wale wanaompenda.
6 Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani?
Lakini ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na kuwapeleka mahakamani?
7 Je, si wao wanaolikufuru Jina lile lililo bora sana mliloitiwa?
Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa?
8 Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema.
Kama mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: “Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe”, mtakuwa mnafanya vema kabisa.
9 Lakini kama mnakuwa na upendeleo kwa watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa ninyi ni wakosaji.
Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia.
10 Kwa maana mtu yeyote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote.
Anayevunja amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote.
11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” alisema pia, “Usiue.” Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.
Maana yuleyule aliyesema: “Usizini,” alisema pia “Usiue”. Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria.
12 Hivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru.
Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru.
13 Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu yeyote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.
Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu.
14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa?
Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa?
15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula,
Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula.
16 mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini?
Yafaa kitu gani ninyi kuwaambia hao: “Nendeni salama mkaote moto na kushiba,” bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha?
17 Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.
Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.
18 Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.” Nionyeshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo.
Lakini mtu anaweza kusema: “Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!” Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu.
19 Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani yanaamini hivyo na kutetemeka.
Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu.
20 Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu?
Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila matendo imekufa?
21 Je, Abrahamu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaki madhabahuni?
Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu.
22 Unaona jinsi ambavyo imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda.
Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake.
23 Kwa njia hiyo yakatimizwa yale Maandiko yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu.
Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: “Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu.”
24 Mnaona ya kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.
Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake na si kwa imani peke yake.
25 Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine?
Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine.
26 Kama vile ambavyo mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.
Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.

< Yakobo 2 >