< Isaya 57 >
1 Mwenye haki hupotea, wala hakuna hata mmoja awazaye hilo moyoni mwake; watu wanaomcha Mungu huondolewa, wala hakuna hata mmoja anayeelewa kuwa wenye haki wameondolewa ili wasipatikane na maovu.
2 Wale waendao kwa unyofu huwa na amani; hupata pumziko walalapo mautini.
3 “Lakini ninyi: Njooni hapa, ninyi wana wa wachawi, ninyi wazao wa wazinzi na makahaba!
4 Mnamdhihaki nani? Ni nani mnayemcheka kwa dharau, na kumtolea ndimi zenu? Je, ninyi si watoto wa waasi, uzao wa waongo?
5 Mnawaka tamaa katikati ya mialoni na chini ya kila mti uliotanda matawi; mnawatoa kafara watoto wenu kwenye mabonde na chini ya majabali yenye mianya.
6 “Sanamu zilizo katikati ya mawe laini ya mabondeni ndizo fungu lenu; hizo ndizo sehemu yenu. Naam, kwa hizo mmemimina sadaka za vinywaji, na kutoa sadaka za nafaka. Katika haya yote, niendelee kuona huruma?
7 Umeweka kitanda chako juu kwenye kilima kirefu kilichoinuka, huko ulikwenda kutoa dhabihu zako.
8 Nyuma ya milango yako na miimo yako umeweka alama zako za kipagani. Kwa kuniacha mimi, ulifunua kitanda chako, umepanda juu yake na kukipanua sana; ulifanya patano na wale ambao unapenda vitanda vyao, nawe uliangalia uchi wao.
9 Ulikwenda kwa Moleki ukiwa na mafuta ya zeituni, na ukaongeza manukato yako. Ukawatuma wajumbe wako mbali sana, ukashuka kwenye kaburi lenyewe! (Sheol )
10 Ulikuwa umechoshwa na njia zako zote, lakini hukusema, ‘Hakuna tumaini.’ Ulipata uhuisho wa nguvu zako, kwa sababu hiyo hukuzimia.
11 “Ni nani uliyemhofu hivyo na kumwogopa hata ukawa mwongo kwangu, wala hukunikumbuka au kutafakari hili moyoni mwako? Si ni kwa sababu nimekuwa kimya muda mrefu hata huniogopi?
12 Nitaifunua haki yako na matendo yako, nayo hayatakufaidi.
13 Utakapolia kwa kuhitaji msaada, sanamu zako ulizojikusanyia na zikuokoe! Upepo utazipeperusha zote, pumzi peke yake itazipeperusha, Lakini mtu atakayenifanya kimbilio lake, atairithi nchi na kuumiliki mlima wangu mtakatifu.”
14 Tena itasemwa: “Jengeni, jengeni, itengenezeni njia! Ondoeni vikwazo katika njia ya watu wangu.”
15 Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu, yeye aliyeinuliwa sana, yeye aishiye milele, ambaye jina lake ni Mtakatifu: “Ninaishi mimi mahali palipoinuka na patakatifu, lakini pia pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na mwenye roho ya unyenyekevu, ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu na kuihuisha mioyo yao waliotubu.
16 Sitaendelea kulaumu milele, wala sitakasirika siku zote, kwa kuwa roho ya mwanadamu ingezimia mbele zangu: yaani pumzi ya mwanadamu niliyemuumba.
17 Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi; nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira, na bado aliendelea katika njia zake za tamaa.
18 Nimeziona njia zake, lakini nitamponya, nitamwongoza na kumrudishia upya faraja,
19 nikiumba sifa midomoni ya waombolezaji katika Israeli. Amani, amani, kwa wale walio mbali na kwa wale walio karibu,” asema Bwana. “Nami nitawaponya.”
20 Bali waovu ni kama bahari ichafukayo, ambayo haiwezi kutulia, mawimbi yake hutupa takataka na matope.
21 Mungu wangu asema, “Hakuna amani kwa waovu.”