< Isaya 33 >
1 Ole wako wewe, ee mharabu, wewe ambaye hukuharibiwa! Ole wako, ee msaliti, wewe ambaye hukusalitiwa! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa; utakapokwisha kusaliti, utasalitiwa.
2 Ee Bwana, uturehemu, tunakutamani. Uwe nguvu yetu kila asubuhi na wokovu wetu wakati wa taabu.
3 Kwa ngurumo ya sauti yako, mataifa yanakimbia; unapoinuka, mataifa hutawanyika.
4 Mateka yenu, enyi mataifa, yamevunwa kama vile wafanyavyo madumadu, kama kundi la nzige watu huvamia juu yake.
5 Bwana ametukuka, kwa kuwa anakaa mahali palipoinuka, ataijaza Sayuni kwa haki na uadilifu.
6 Atakuwa msingi ulio imara kwa wakati wenu, ghala za wokovu tele, hekima na maarifa; kumcha Bwana ni ufunguo wa hazina hii.
7 Angalia, watu wake mashujaa wanapiga kelele kwa nguvu barabarani, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.
8 Njia kuu zimeachwa, hakuna wasafiri barabarani. Mkataba umevunjika, mashahidi wake wamedharauliwa, hakuna yeyote anayeheshimiwa.
9 Ardhi inaomboleza na kuchakaa, Lebanoni imeaibika na kunyauka, Sharoni ni kama Araba, nayo Bashani na Karmeli wanapukutisha majani yao.
10 “Sasa nitainuka,” asema Bwana. “Sasa nitatukuzwa; sasa nitainuliwa juu.
11 Mlichukua mimba ya makapi, mkazaa mabua, pumzi yenu ni moto uwateketezao.
12 Mataifa yatachomwa kama ichomwavyo chokaa, kama vichaka vya miiba vilivyokatwa ndivyo watakavyochomwa.”
13 Ninyi mlio mbali sana, sikieni lile nililofanya; ninyi mlio karibu, tambueni uweza wangu!
14 Wenye dhambi katika Sayuni wametiwa hofu, kutetemeka kumewakumba wasiomcha Mungu: “Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto ulao? Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto unaowaka milele?”
15 Yeye aendaye kwa uadilifu na kusema lililo haki, yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma na kuizuia mikono yake isipokee rushwa, yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji, na yeye afumbaye macho yake yasitazame sana uovu:
16 huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu, ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani. Atapewa mkate wake, na maji yake hayatakoma.
17 Macho yenu yatamwona mfalme katika uzuri wake na kuiona nchi inayoenea mbali.
18 Katika mawazo yenu mtaifikiria hofu iliyopita: “Yuko wapi yule afisa mkuu? Yuko wapi yule aliyechukua ushuru? Yuko wapi afisa msimamizi wa minara?”
19 Hutawaona tena wale watu wenye kiburi, wale watu wenye usemi wa mafumbo, wenye lugha ngeni, isiyoeleweka.
20 Mtazame Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yenu yatauona Yerusalemu, mahali pa amani pa kuishi, hema ambalo halitaondolewa, nguzo zake hazitangʼolewa kamwe, wala hakuna kamba yake yoyote itakayokatika.
21 Huko Bwana atakuwa Mwenye Nguvu wetu. Patakuwa kama mahali pa mito mipana na vijito. Hakuna jahazi lenye makasia litakalopita huko, wala hakuna meli yenye nguvu itakayopita huko.
22 Kwa kuwa Bwana ni mwamuzi wetu, Bwana ndiye mtoa sheria wetu, Bwana ni mfalme wetu, yeye ndiye atakayetuokoa.
23 Kamba zenu za merikebu zimelegea: Mlingoti haukusimama imara, nalo tanga halikukunjuliwa. Wingi wa mateka yatagawanywa, hata yeye aliye mlemavu atachukua nyara.
24 Hakuna yeyote aishiye Sayuni atakayesema, “Mimi ni mgonjwa”; nazo dhambi za wale waishio humo zitasamehewa.