< Isaya 31 >
1 Ole wao wale washukao Misri kwa ajili ya msaada, wale wategemeao farasi, wanaoweka tumaini katika wingi wa magari yao ya vita, na katika nguvu nyingi za wapanda farasi, lakini hawamwangalii yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, wala hawatafuti msaada kwa Bwana.
2 Hata hivyo yeye pia ana hekima na anaweza kuleta maafa, wala hayatangui maneno yake. Yeye atainuka dhidi ya nyumba ya mwovu, dhidi ya wale ambao huwasaidia watenda mabaya.
3 Lakini Wamisri ni wanadamu, wala si Mungu, farasi wao ni nyama, wala si roho. Wakati Bwana atakaponyoosha Mkono wake, yeye anayesaidia atajikwaa, naye anayesaidiwa ataanguka, wote wawili wataangamia pamoja.
4 Hili ndilo Bwana analoniambia: “Kama vile simba angurumavyo, simba mkubwa juu ya mawindo yake: hata ingawa kundi lote la wachunga mifugo huitwa pamoja dhidi yake, hatiwi hofu na kelele zao wala kusumbuliwa na ghasia zao; ndivyo Bwana Mwenye Nguvu Zote atakavyoshuka kufanya vita juu ya Mlima Sayuni na juu ya vilele vyake.
5 Kama ndege warukao, Bwana Mwenye Nguvu Zote ataukinga Yerusalemu; ataukinga na kuuokoa, atapita juu yake na kuufanya salama.”
6 Mrudieni yeye ambaye nyumba ya Israeli imemwasi sana.
7 Kwa kuwa katika siku ile kila mmoja wenu atazikataa sanamu za fedha na za dhahabu zilizotengenezwa kwa mikono yenu yenye dhambi.
8 “Ashuru itaanguka kwa upanga ambao si wa mwanadamu; upanga usio wa kibinadamu utawaangamiza. Watakimbia mbele ya upanga na vijana wao wa kiume watafanyizwa kazi kwa lazima.
9 Ngome zao zitaanguka kwa sababu ya hofu; kwa kuona bendera ya vita, majemadari wao watashikwa na hofu ya ghafula,” asema Bwana, ambaye moto wake uko Sayuni, nayo tanuru yake iko Yerusalemu.