< Isaya 18 >
1 Ole kwa nchi ya mvumo wa mabawa, kando ya mito ya Kushi,
2 iwapelekayo wajumbe wake kwa njia ya bahari kwa mashua za mafunjo juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi, kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito.
3 Enyi mataifa yote ya ulimwengu, ninyi mnaoishi duniani wakati bendera itakapoinuliwa milimani, mtaiona, nayo tarumbeta itakapolia, mtaisikia.
4 Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Nitatulia kimya na kutazama kutoka maskani yangu, kama joto linalometameta katika mwanga wa jua, kama wingu la umande katika joto la wakati wa mavuno.”
5 Kwa maana, kabla ya mavuno, wakati wa kuchanua ukishapita na maua yakawa zabibu zinazoiva, atayakata machipukizi kwa mundu wa kupogolea matawi, naye atakata na kuyaondoa matawi yaliyopanuka.
6 Yote yataachwa kwa ajili ya ndege wawindao wa mlimani na wanyama pori, ndege watajilisha juu yake wakati wote wa kiangazi, nao wanyama pori wakati wote wa masika.
7 Wakati huo matoleo yataletwa kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote kutoka kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kutoka kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, kutoka taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito, matoleo yataletwa katika Mlima Sayuni, mahali pa Jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote.