< Isaya 14 >
1 Bwana atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, na kuwakalisha katika nchi yao wenyewe. Wageni wataungana nao na kujiunga na nyumba ya Yakobo.
2 Mataifa watawachukua na kuwaleta mahali pao wenyewe. Nayo nyumba ya Israeli itamiliki mataifa kama watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana. Watawafanya watekaji wao kuwa mateka, na kutawala juu ya wale waliowaonea.
3 Katika siku Bwana atakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili,
4 utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli: Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho! Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma!
5 Bwana amevunja fimbo ya mwovu, fimbo ya utawala ya watawala,
6 ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa kwa mapigo yasiyo na kikomo, nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa kwa jeuri pasipo huruma.
7 Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani, wanabubujika kwa kuimba.
8 Hata misunobari na mierezi ya Lebanoni inashangilia mbele yako na kusema, “Basi kwa sababu umeangushwa chini, hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.”
9 Kuzimu kote kumetaharuki kukulaki unapokuja, kunaamsha roho za waliokufa ili kukupokea, wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu, kunawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme: wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa. (Sheol )
10 Wote wataitikia, watakuambia, “Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo; wewe umekuwa kama sisi.”
11 Majivuno yako yote yameshushwa mpaka kuzimu, pamoja na kelele ya vinubi vyako, mafunza yametanda chini yako, na minyoo imekufunika. (Sheol )
12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko! Umetupwa chini duniani, wewe uliyepata kuangusha mataifa!
13 Ulisema moyoni mwako, “Nitapanda juu hadi mbinguni, nitakiinua kiti changu cha enzi juu ya nyota za Mungu, nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko, kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.
14 Nitapaa juu kupita mawingu, nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”
15 Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu, hadi kwenye vina vya shimo. (Sheol )
16 Wale wanaokuona wanakukazia macho, wanatafakari hatima yako: “Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia na kufanya falme zitetemeke,
17 yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa, aliyeipindua miji yake, na ambaye hakuwaachia mateka wake waende nyumbani?”
18 Wafalme wote wa mataifa wamelala kwa heshima kila mmoja katika kaburi lake.
19 Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako kama tawi lililokataliwa, umefunikwa na waliouawa pamoja na wale waliochomwa kwa upanga, wale washukao mpaka kwenye mawe ya shimo. Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo,
20 Hutajumuika nao kwenye mazishi, kwa kuwa umeharibu nchi yako na kuwaua watu wako. Mzao wa mwovu hatatajwa tena kamwe.
21 Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe kwa ajili ya dhambi za baba zao, wasije wakainuka ili kuirithi nchi na kuijaza dunia kwa miji yao.
22 Bwana Mwenye Nguvu Zote asema, “Nitainuka dhidi yao, nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli pamoja na watu wake walionusurika, watoto wake na wazao wake,” asema Bwana.
23 “Nitaifanya kuwa mahali pa bundi, na kuwa nchi ya matope; nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
24 Bwana Mwenye Nguvu Zote ameapa, “Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa, nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.
25 Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu, juu ya milima yangu nitawakanyagia chini. Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu, nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”
26 Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote, huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.
27 Kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amekusudia, ni nani awezaye kumzuia? Mkono wake umenyooshwa, ni nani awezaye kuurudisha?
28 Neno hili lilikuja mwaka ule Mfalme Ahazi alipofariki:
29 Msifurahi, enyi Wafilisti wote, kwamba fimbo iliyowapiga imevunjika; kutoka mzizi wa huyo nyoka atachipuka nyoka mwenye sumu kali, uzao wake utakuwa joka lirukalo, lenye sumu kali.
30 Maskini kuliko maskini wote watapata malisho, nao wahitaji watalala salama. Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa, nayo njaa itawaua walionusurika.
31 Piga yowe, ee lango! Bweka, ee mji! Yeyukeni, enyi Wafilisti wote! Wingu la moshi linakuja toka kaskazini, wala hakuna atakayechelewa katika safu zake.
32 Ni jibu gani litakalotolewa kwa wajumbe wa taifa hilo? “Bwana ameifanya imara Sayuni, nako ndani yake watu wake walioonewa watapata kimbilio.”