< Hosea 1 >
1 Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na wakati wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi, mfalme wa Israeli.
Hili ni neno la Bwana lililofika kwa Hosea mwana wa Beeri siku za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na katika siku za Yeroboamu mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli.
2 Wakati Bwana alipoanza kuzungumza kupitia Hosea, Bwana alimwambia, “Nenda ukajitwalie mwanamke wa uzinzi na watoto wa uzinzi, kwa sababu nchi ina hatia ya uzinzi wa kupindukia kwa kumwacha Bwana.”
Wakati Bwana alipozungumza kwanza kupitia Hosea, akamwambia, “Nenda ukajitwalie mke ambaye ni kahaba. Atakuwa na watoto ambao ni matokeo ya ukahaba wake. Kwa maana nchi inafanya uzinzi mkubwa kwa kumwacha Bwana.”
3 Kwa hiyo alimwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba na kumzalia Hosea mwana.
Basi Hosea akaenda akamwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba, akazaa mtoti mwanamume.
4 Kisha Bwana akamwambia Hosea, “Mwite Yezreeli, kwa kuwa kitambo kidogo nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa ajili ya mauaji ya kule Yezreeli, nami nitaukomesha ufalme wa Israeli.
Bwana akamwambia Hosea, Mwite jina lake Yezreeli. Kwa maana kwa muda mfupi nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa sababu ya kumwaga damu huko Yezreeli; nami nitamaliza ufalme wa nyumba ya Israeli.
5 Katika siku ile nitavunja upinde wa Israeli katika Bonde la Yezreeli.”
Itatokea siku ile nitakapovunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli.
6 Gomeri akachukua tena mimba akamzaa binti. Kisha Bwana akamwambia Hosea, “Mwite Lo-Ruhama, kwa maana sitaonyesha tena upendo kwa nyumba ya Israeli, kwamba nisije kabisa nikawasamehe.
Gomeri akachukua mimba tena akamzaa binti. Ndipo Bwana akamwambia Hosea, “Mwite jina lake Lo Ruhama; kwa maana sitawahurumia tena nyumba ya Israeli, nisije nikawasamehe kwa njia yoyote.
7 Hata hivyo nitaonyesha upendo kwa nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa si kwa upinde, upanga au vita, wala kwa farasi na wapanda farasi, bali kwa njia ya Bwana Mungu wao.”
Hata hivyo nitawahurumia nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa mwenyewe, Bwana, Mungu wao. Sitawaokoa kwa upinde, upanga, vita, farasi, au wapanda farasi. '
8 Baada ya Gomeri kumwachisha Lo-Ruhama kunyonya, Gomeri alipata mwana mwingine.
Baada ya Gomeri kumwachisha Lo Ruhama, alipata mimba na kuzaa mtoto mwingine mwanamume.
9 Kisha Bwana akasema, “Mwite Lo-Ami kwa maana ninyi si watu wangu, nami si Mungu wenu.
Ndipo Bwana akasema, “Mwite jina la Lo Ami; kwa kuwa ninyi si watu wangu, wala mimi si Mungu wenu.”
10 “Hata hivyo Waisraeli watakuwa kama mchanga kando ya bahari, ambao hauwezi kupimika wala kuhesabiwa. Mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’
Hata hivyo idadi ya watu wa Israeli itakuwa kama mchanga wa bahari, ambayo haiwezi kupimwa au kuhesabiwa. Itakuwa pale ambapo waliambiwa, “Ninyi si watu wangu,” wataambiwa, “Ninyi ni watu wa Mungu aliye hai.”
11 Watu wa Yuda na watu wa Israeli wataunganishwa tena, nao watamchagua kiongozi mmoja nao watakwea watoke katika nchi, kwa kuwa siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.
Watu wa Yuda na watu wa Israeli watakusanyika pamoja. Wao wataweka kiongozi mmoja wao wenyewe, na watatoka kutoka nchi, kwa maana itakuwa siku ya Yezreeli kuu.