< Wahebrania 1 >

1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali,
Nyakati zilizopita Mungu alizungumza na mababu zetu kupitia manabii mara nyingi na kwa njia nyingi.
2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu. (aiōn g165)
Lakini katika siku hizi tulizonazo, Mungu ameongea nasi kupitia Mwana, ambaye alimweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia yeye pia aliumba ulimwengu. (aiōn g165)
3 Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni.
Mwanawe ni nuru ya utukufu wake, tabia pekee ya asili yake, na anayeendeleza vitu vyote kwa neno la nguvu zake. Baada ya kukamilisha utakaso wa dhambi, aliketi chini mkono wa kulia wa enzi huko juu.
4 Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.
Amekuwa bora kuliko malaika, kama vile jina alilolirithi lilivyo bora zaidi kuliko jina lao.
5 Kwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wowote Mungu alipata kumwambia, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuzaa?” Au tena, “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu?”
Kwa maana ni kwa malaika gani aliwahi kusema, “Wewe ni mwanangu, leo nimekuwa baba yako?” Na tena, “Nitakuwa baba kwake, naye atakuwa mwana kwangu?”
6 Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema, “Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.”
Tena, wakati Mungu alipomleta mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, husema, “Malaika wote wa Mungu lazima wamwabudu.”
7 Anenapo kuhusu malaika asema, “Huwafanya malaika wake kuwa pepo, watumishi wake kuwa miali ya moto.”
Kuhusu malaika asema, “Yeye ambaye hufanya malaika zake kuwa roho, na watumishi wake kuwa ndimi za moto.”
8 Lakini kwa habari za Mwana asema, “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, kitadumu milele na milele, nayo haki itakuwa fimbo ya utawala ya ufalme wako. (aiōn g165)
Lakini kuhusu Mwana husema, “Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele. Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya haki. (aiōn g165)
9 Umependa haki na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuweka juu ya wenzako kwa kukupaka mafuta ya furaha.”
Umependa haki na kuchukia uvunjaji wa sheria, kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekupaka mafuta ya furaha kuliko wenzako.”
10 Pia asema, “Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.
Hapo mwanzo, Bwana, uliweka msingi wa dunia. Mbingu ni kazi za mikono yako.
11 Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu; zote zitachakaa kama vazi.
Zitatoweka, lakini wewe utaendelea. Zote zitachakaa kama vazi.
12 Utazikungʼutakungʼuta kama joho, nazo zitachakaa kama vazi. Lakini wewe hubadiliki, nayo miaka yako haikomi kamwe.”
Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilika kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule, na miaka yako haitakoma.”
13 Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wowote, “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako”?
Lakini ni kwa malaika yupi Mungu alisema wakati wowote, “Keti mkono wangu wa kulia mpaka nitakapowafanya adui zako kuwa kiti cha miguu yako”?
14 Je, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?
Je, malaika wote siyo roho zilizotumwa kuwahudumia na kuwatunza wale watakaourithi wokovu?

< Wahebrania 1 >