< Wahebrania 8 >
1 Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu ambaye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Aliye Mkuu mbinguni,
2 yeye ahudumuye katika patakatifu, hema la kweli lililowekwa na Bwana, wala si na mwanadamu.
3 Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo, ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa.
4 Kama angekuwa duniani, hangekuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria.
5 Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Mose alionywa alipokaribia kujenga hema, akiambiwa: “Hakikisha kuwa unavitengeneza vitu vyote kwa mfano ulioonyeshwa kule mlimani.”
6 Lakini huduma aliyopewa Yesu ni bora zaidi kuliko yao, kama vile agano ambalo yeye ni mpatanishi wake lilivyo bora zaidi kuliko lile la zamani, nalo limewekwa misingi wa ahadi zilizo bora zaidi.
7 Kwa maana kama hapakuwa na kasoro katika lile agano la kwanza, pasingekuwa na haja ya kutafuta nafasi kwa ajili ya jingine.
8 Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema: “Siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.
9 Agano langu halitakuwa kama lile nililofanya na baba zao nilipowashika mkono kuwaongoza watoke nchi ya Misri, kwa sababu hawakuendelea kuwa waaminifu katika agano langu, nami nikawaacha, asema Bwana.
10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli baada ya siku zile, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu katika nia zao na kuziandika mioyoni mwao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake, wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’ kwa sababu wote watanijua mimi, tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.
12 Kwa sababu nitasamehe uovu wao, wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”
13 Kwa kuliita agano hili “jipya,” Mungu amefanya lile agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.