< Wahebrania 4 >

1 Kwa hiyo, kwa kuwa bado ahadi ya kuingia rahani iko wazi, tujihadhari ili hata mmoja wenu asije akaikosa.
Mungu alituahidia kwamba tutaweza kupata pumziko hilo alilosema. Basi, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo.
2 Kwa maana sisi pia tumesikia Injili iliyohubiriwa kwetu, kama nao walivyosikia; lakini ujumbe ule waliousikia haukuwa na maana kwao, kwa sababu wale waliousikia hawakuuchanganya na imani.
Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani.
3 Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha, kama vile Mungu alivyosema, “Kwa hiyo nikaapa katika hasira yangu, ‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’” Lakini kazi yake ilikamilika tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema: “Nilikasirika, nikaapa: Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko.” Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu.
4 Kwa maana mahali fulani amezungumza kuhusu siku ya saba, akisema: “Katika siku ya saba Mungu alipumzika kutoka kazi zake zote.”
Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: “Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote.”
5 Tena hapo juu asema, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”
Tena jambo hili lasemwa pia: “Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko.”
6 Kwa hiyo inabaki kuwa wazi kwa wengine kuingia, nao wale wa kwanza waliopokea Injili walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii.
Wale waliotangulia kuhubiriwa Habari Njema hawakupata pumziko hilo kwa sababu hawakuamini. Wapo, basi, wengine ambao wangejaliwa kulipata.
7 Kwa hiyo Mungu ameweka siku nyingine, akaiita Leo, akisema kwa kinywa cha Daudi baadaye sana, kwa maneno yaliyotangulia kunenwa: “Leo, kama mkiisikia sauti yake, msiifanye mioyo yenu migumu.”
Jambo hili ni wazi, kwani Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa “Leo”. Miaka mingi baadaye Mungu alisema juu ya hiyo siku kwa maneno ya Daudi katika Maandiko yaliyokwisha tajwa: “Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu.”
8 Kwa maana kama Yoshua alikuwa amewapa raha, Mungu hangesema tena baadaye kuhusu siku nyingine.
Kama Yoshua angaliwapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine.
9 Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu;
Kwa hiyo, basi, bado lipo pumziko kwa watu wa Mungu kama kule kupumzika kwake Mungu siku ya saba.
10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyopumzika kutoka kazi zake.
Maana, kila anayepata pumziko aliloahidi Mungu atapumzika baada ya kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika baada ya yake.
11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.
Basi, tujitahidi kupata pumziko hilo, ili asiwepo yeyote miongoni mwenu atakayeshindwa, kama walivyofanya wao kwa sababu ya ukosefu wao wa imani.
12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na mafuta. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya watu.
13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.
Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake. Kwake, sisi sote tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu.
14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu.
Basi, tunapaswa kuzingatia kwa uthabiti imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka kwa Mungu mwenyewe—Yesu, Mwana wa Mungu.
15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi.
Huyu Kuhani Mkuu wetu si mmoja ambaye hawezi kutuunga mkono katika unyonge wetu, ila ni Kuhani Mkuu ambaye alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi.
16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu, palipo na neema, ili tukajipatie huruma na neema ya kutusaidia wakati wa lazima.

< Wahebrania 4 >