< Wahebrania 10 >

1 Sheria ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kwa njia ya dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu.
Sheria ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje, basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu?
2 Kama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi.
Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma.
3 Lakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka,
Lakini dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao.
4 kwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.
Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi.
5 Kwa hiyo, Kristo alipokuja duniani, alisema: “Dhabihu na sadaka hukuzitaka, bali mwili uliniandalia;
Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: “Hukutaka dhabihu wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili.
6 sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukupendezwa nazo.
Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi.
7 Ndipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja, imeandikwa kunihusu katika kitabu: Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’”
Hapo nikasema: Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha Sheria.”
8 Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe).
Kwanza alisema: “Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi.” Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na Sheria.
9 Kisha akasema “Mimi hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile Agano la kwanza ili kuimarisha la pili.
Kisha akasema: “Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako.” Hivyo Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine moja.
10 Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu.
Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.
11 Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi.
Kila kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi, dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi.
12 Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu.
Lakini Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha akaketi upande wa kulia wa Mungu.
13 Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake,
Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake.
14 kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.
Basi, kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.
15 Pia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema:
Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema:
16 “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao baada ya siku hizo, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika katika nia zao.”
“Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao.”
17 Kisha aongeza kusema: “Dhambi zao na kutokutii kwao sitakumbuka tena.”
Kisha akaongeza kusema: “Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu.”
18 Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.
Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa dhambi.
19 Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu,
Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu.
20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani, mwili wake,
Yeye ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake mwenyewe.
21 basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu,
Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu.
22 sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi.
Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.
Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema.
Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.
25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.
Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia.
26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi.
Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi.
27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu.
Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga.
28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu.
Mtu yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu.
29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema?
Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani?
30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.”
Maana tunamfahamu yule aliyesema, “Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza,” na ambaye alisema pia, “Bwana atawahukumu watu wake.”
31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.
Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno!
32 Kumbukeni siku zile za kwanza, ambazo mkiisha kutiwa nuru mlistahimili mashindano makali ya maumivu.
Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili.
33 Wakati mwingine mlitukanwa na kuteswa hadharani; wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale waliofanyiwa hivyo.
Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo.
34 Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyangʼanywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.
Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang'anywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele.
35 Kwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno.
Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa.
36 Inawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi.
Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi.
37 Kwa kuwa bado kitambo kidogo tu, “Yeye ajaye atakuja wala hatakawia.
Maana kama yasemavyo Maandiko: “Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia.
38 Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani. Naye kama akisitasita, sina furaha naye.”
Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye.”
39 Lakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaositasita na kuangamia, bali tuko miongoni mwa hao wenye imani na hivyo tunaokolewa.
Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na tunaokolewa.

< Wahebrania 10 >