< Hagai 2 >
1 Katika siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba, neno la Bwana lilikuja kupitia nabii Hagai, kusema:
Katika Mwezi wa saba siku ya ishirini na moja ya mwezi, Neno la Bwana lilikuja kwa mkono wa Nabii Hagai, na kusema,
2 “Sema na Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, na mabaki ya watu. Uwaulize,
“Ongea na mkuu wa mkoa wa Yudah, Zerubabeli mwana wa Sheltieli, na kwa kuhani mkuu Yehozadaki; na kwa masalia ya watu. Waambie,
3 ‘Ni nani miongoni mwenu aliyebaki ambaye aliiona hii nyumba katika utukufu wake wa mwanzo? Sasa inaonekanaje kwenu? Je, haionekani kwenu kama si kitu?
Ni nani amebaki kati yenu aliuona utukufu wa nyumba ya kwanza? Na mnauonaje huu wa sasa? Je si kama si chochote machoni penu?
4 Lakini sasa uwe imara, ee Zerubabeli,’ asema Bwana. ‘Kuwa imara, ee kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Mwe imara, enyi watu wote wa nchi,’ asema Bwana, ‘na mfanye kazi. Kwa kuwa mimi nipo pamoja nanyi,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Sasa, muwe hodari, Zerubabeli' -hili ni tamko la Bwana - na uwe hodari, kuhani mkuu Joshua mwana wa Yehozadaki; muwe hodari, enyi watu wa nchi! - hili ni tamko la Bwana - na kazi, kwa kuwa ni pamoja nawe! hili ni tamko la Bwana wa majeshi.
5 ‘Hili ndilo nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri. Pia Roho wangu anadumu katikati yenu. Msiogope.’
Kutegemeana na ahadi ilioko katika agano nililofanya na ninyi mlipotoka Misri na Roho yangu ilisimama katikati yenu, msiogope'
6 “Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Baada ya muda kidogo kwa mara nyingine nitazitikisa mbingu na nchi, bahari na nchi kavu.
Kwa kuwa Bwana wa majeshi anasema hivi: 'kitambo kidogo kwa mara nyingine nitatikisa mbingu na dunia, bahari na nchi kavu!
7 Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Na nitatikisa kila taifa, na kila taifa wataleta vitu vya thamani kwangu, na kuijaza nyumba hii na utukufu!' asema Bwana wa Majeshi
8 ‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Dhahabu na fedha ni yangu' - hili ni tamko la Bwana wa majeshi.
9 ‘Utukufu wa nyumba hii ya sasa utakuwa mkubwa kuliko utukufu wa ile nyumba ya mwanzoni,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. ‘Na mahali hapa nitawapa amani,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.”
Utukufu wa nyumba hii utakuwa mkuu zaidi ya utukufu wa nyumba ya kwanza ', asema Bwana wa majeshi,' na nitawapa amani katika sehemu hii'- hili ni Tamko la Bwana wa majeshi
10 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Bwana lilikuja kwa nabii Hagai:
Katika siku ya ishirini na nne mwezi wa tisa, mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Bwana lilimjia nabii Hagaina kusema,
11 “Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Ulizeni makuhani jinsi sheria inavyosema:
“Bwana wa majeshi asema hivi: Muulize kuhani kuhusu sheria, na kusema:
12 Kama mtu akibeba nyama iliyowekwa wakfu katika pindo la vazi lake, kisha lile pindo likagusa mkate au mchuzi, divai, mafuta au chakula kingine, je, kitu hicho kitakuwa kimewekwa wakfu?’” Makuhani wakajibu, “La hasha.”
kama mtu akibeba nyama iliyotolewa kwa Bwana katika pindo la vazi lake, kama upindo utagusa mkate au mchuzi, mvinyo au mafuta, au chakula kingine, je chakula hicho kinafanyika kitakatifu?”Kuhani alijibu akasema, “hapana”
13 Kisha Hagai akasema, “Je, kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti akigusa mojawapo ya vitu hivi, kitu hicho kitakuwa kimetiwa unajisi?” Makuhani wakajibu, “Ndiyo, huwa kimenajisiwa.”
Halafu Hagai akasema.”Kama mtu mchafu najisi kwa ajili ya kumgusa maiti na kugusa vitu hivi, wote wanaweza kuwa wachafu?” Kuhani akajibu na kusema, “Ndiyo, watakuwa wachafu.”
14 Kisha Hagai akasema, “‘Basi ndivyo walivyo machoni pangu hawa watu na taifa hili,’ asema Bwana. ‘Lolote wafanyalo na chochote watoacho hapo ni najisi.
Kwa hiyo Haghai akajibu nakusema, “Ni pamoja na hawa watu na pamoja na taifa liliko mbele yangu! - haya anayasema Bwana- na pia kila kitu kimekwisha kwa mkono wake: walichotoa hakikuwa kisafi kilikuwa kichafu.
15 “‘Sasa fikirini kwa uangalifu kuanzia leo na kuendelea: tafakarini jinsi mambo yalivyokuwa kabla halijawekwa jiwe moja juu ya lingine katika Hekalu la Bwana.
Kwa hiyo, fikiri kutoka siku hii ya leo na za nyuma, kabla hata jiwe halijawekwa kwenye jiwe lingine katika hekalu la Bwana,
16 Wakati mtu alipoendea lundo la nafaka la vipimo ishirini, kulikuwa na vipimo kumi tu. Wakati mtu alipoendea pipa la mvinyo ili kuchota vipimo hamsini, kulikuwa na vipimo ishirini tu.
ilikuwaje basi? kila mtu alipokuja kwenye vipimo ishirini vya nafaka, kumbe kulikuwa na vipimo kumi tu, na aliyekuja na aliyekuja kuchota divai ya vipimo hamsini, kumbe kuliwa na vipimo ishirini tu.
17 Kazi zenu zote za mikono nilizipiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, lakini hata hivyo, hamkunigeukia mimi,’ asema Bwana.
Niliwataabisha ninyi na kazi za mikono yenu kwa doa na koga, nalikini hamkunirudia'- asema Bwana.
18 ‘Tangu leo na kuendelea, kuanzia siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, tafakarini siku ambayo msingi wa Hekalu la Bwana uliwekwa. Tafakarini:
tafakari siku hii ya leo na kuendelea, kutoka siku ya ishirini na nne katika mwezi mwezi wa tisa, toka siku ile msingi wa hekalu la Bwana kuwekwa. Tafakarini hilo!
19 Je, bado kuna mbegu iliyobakia ghalani? Mpaka sasa, hakuna mzabibu au mtini, mkomamanga wala mzeituni uliozaa tunda. “‘Kuanzia leo na kuendelea, nitawabariki.’”
Je, bado kuna mbegu katika ghala? Mzabibu, mti wa mtini, komamanga, na mti wa mzeituni havikuzaa matunda! lakini kutoka siku hii ya leo nitawabariki!”'
20 Neno la Bwana likamjia Hagai kwa mara ya pili katika siku ya ishirini na nne ya mwezi kusema:
Tena neno la Bwana likaja kwa mara ya pili kwa Haghai siku ya ishiri na nne katika mwezi kusema,
21 “Mwambie Zerubabeli mtawala wa Yuda kwamba nitazitikisa mbingu na nchi.
“Sema na mkuu wa mkoa wa Yuda, Zerubabeli umwambie, 'Nitatikisa mbingu na dunia.
22 Nitapindua viti vya enzi vya falme, na kuziharibu kabisa nguvu za falme za kigeni. Nitapindua magari ya vita pamoja na waendeshaji wake; farasi na wapanda farasi wataanguka, kila mmoja kwa upanga wa ndugu yake.
kwa hiyo nitaanhusha kiti cha falme na kuharibu nguvu ya falme za mataifa! nitaangusha magahari na wapandao; farasi na wapanda farasi wataanguka, kila mmoja kwa sababu ya upanga wa ndugu zake.
23 “‘Katika siku ile,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, ‘nitakuchukua wewe, mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli,’ asema Bwana. ‘Nitakufanya kama pete yangu ya muhuri, kwa kuwa nimekuchagua,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.”
Siku hiyo '-hivi ndivyo asema Bwana wa Majeshi- 'Nitakuchukua wewe Zerubabeli mwana wa Sheltieli, kama mtumishi wangu'- hivi ndivyo Bwana anavyosema. “Nitakutuma kama pete ya muhuri wangu, kwa sababu mimi ndiye niliyekuchagua!'- asema Bwana wa majeshi!”