< Mwanzo 8 >
1 Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa naye ndani ya safina, akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakaondoka.
Mungu akamtazama Nuhu, wanyama wote wa mwitu, na wanyama wote wa kufugwa ambao walikuwa pamoja naye kwenye safina. Mungu akafanya upepo uvume juu ya nchi, na maji yakaanza kuzama chini.
2 Zile chemchemi zilizo chini sana ya ardhi pamoja na malango ya mafuriko ya mbinguni yakawa yamefungwa nayo mvua ikawa imekoma kunyesha kutoka angani.
Chemichemi za vilindi pamoja na madirisha ya mbingu vikafungwa, na mvua ikakoma kunyesha.
3 Maji yakaendelea kupungua taratibu katika nchi. Kunako mwisho wa siku ya 150, maji yalikuwa yamepungua,
Maji ya gharika yakaanza kuzama kidogo kidogo katika nchi. na mwisho wa siku miamoja na hamsini maji yakawa yamezama chini.
4 katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati.
safina ikatulia katika mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, juu ya milima ya Ararati.
5 Maji yakaendelea kupungua hadi mwezi wa kumi, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana.
Maji yakaendelea kuzama chini hadi mwezi wa kumi. Siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana.
6 Baada ya siku arobaini Noa akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina
Ikatokea kwamba baada ya siku arobaini Nuhu alifungua dirisha la safina ambayo aliitengeneza.
7 na akamtoa kunguru, akawa akiruka kwenda na kurudi mpaka maji yalipokwisha kukauka juu ya nchi.
Akatuma kunguru na akaruka hadi maji yalipo kauka katika nchi.
8 Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya uso wa ardhi.
Kisha akatuma njiwa kuona kama maji yamezama chini kutoka kwenye uso wa nchi,
9 Lakini hua hakupata mahali pa kutua kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Noa ndani ya safina. Noa akanyoosha mkono akamchukua yule hua akamrudisha ndani ya safina.
lakini njiwa hakuona sehemu ya kutua unyayo wake, na akarudi kwake ndani ya safina, kwa kuwa maji yalikuwa bado yamefunika nchi yote. Akanyoosha mkono wake, akamchukua na kumuweka ndani ya safina pamoja naye.
10 Noa akangojea siku saba zaidi kisha akamtoa tena hua kutoka safina.
Akasubiri siku saba zingine akatuma tena njiwa kutoka kwenye safina.
11 Wakati hua aliporejea kwa Noa jioni, alikuwa amechukua katika mdomo wake jani bichi la mzeituni, lililochumwa wakati ule ule! Ndipo Noa akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya uso wa dunia.
Njiwa akarudi kwake jioni. Tazama! katika mdomo wake kulikuwa na jani bichi la mzeituni lililochumwa. Kwa hiyo Nuhu akatambua kuwa maji yamekwisha zama chini ya nchi.
12 Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Noa.
Akasubiri siku saba zingine na akamtuma njiwa tena. Njiwa hakurudi kwake tena.
13 Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ya mwaka 601, wa kuishi kwake Noa, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Noa akafungua mlango wa safina akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka.
Ikawa kwamba katika mwaka wa mia sita na moja, katika mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikuwa yamekauka katika nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, akatazama nje, na akaona kwamba, Tazama, uso wa nchi ulikuwa umekauka.
14 Katika siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili dunia ilikuwa imekauka kabisa.
Katika mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa imekauka.
15 Ndipo Mungu akamwambia Noa,
Mungu akamwambia Nuhu,
16 “Toka ndani ya safina, wewe na mkeo na wanao na wake zao.
“Toka nje ya safina, wewe, mke wako, wanao wa kiume, na wake wa wanao pamoja nawe.
17 Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe: Ndege, wanyama na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”
Wachukuwe utoke nje pamoja nao kila kiumbe hai chenye mwili ambacho kiko nawe - ndege, wanyama wa kufugwa, na kila kitambaacho ambacho hutambaa juu ya nchi - ili kwamba viweze kukua na kuwa na idadi kubwa zaidi ya viumbe hai katika nchi yote, kwa kuzaliana na kuongezeka juu ya nchi.”
18 Kwa hiyo Noa akatoka nje pamoja na mkewe, wanawe na wake zao.
Kwa hiyo Nuhu akatoka nje pamoja na watoto wake wa kiume, mke wake, na wake wa wa wanawe pamoja naye.
19 Wanyama wote na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi na ndege wote, kila kitu kiendacho juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina, kila aina ya kiumbe, kimoja baada ya kingine.
Kila kiumbe hai, kila kitambaacho, na kila ndege, na kila kiendacho juu ya nchi, kwa kabila zao, wakaiacha safina.
20 Kisha Noa akamjengea Bwana madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.
Nuhu akajenga madhabahu kwa Yahwe. Akachukua baadhi ya wanyama walio safi na baadhi ya ndege walio safi, na kutoa sadaka ya kuteketezwa juu ya madhabahu.
21 Bwana akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.
Yahwe akanusa harufu nzuri ya kuridhisha na akasema moyoni mwake, “Sita laani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, ingawa nia za mioyo yao ni mbaya tokea utoto. Wala sita haribu kilakitu chenye uhai, kama nilivyo fanya.
22 “Kwa muda dunia idumupo, wakati wa kupanda na wa kuvuna, wakati wa baridi na wa joto, wakati wa kiangazi na wa masika, usiku na mchana kamwe havitakoma.”
Wakati nchi isaliapo, majira ya kupanda mbegu na mavuno, baridi na joto, kiangazi na majira ya baridi, mchana na usiku havitakoma.”