< Mwanzo 7 >

1 Ndipo Bwana akamwambia Noa, “Ingia katika safina wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki.
Yahwe akamwambia Nuhu, “Njoo, wewe na nyumba yako wote, katika safina, kwa kuwa nimeona kuwa wewe ni mwenye haki mbele yangu katika kizazi hiki.
2 Uchukue wanyama saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, na wanyama wawili wawili wa kila aina walio najisi wa kiume na wa kike.
Kwa kila mnyama aliye safi utakuja nao saba wa kiume na saba wa kike. Na kwa wanyama wasio safi, lete wawili wawili, wakiume na wakike.
3 Pia uchukue ndege saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, ili kuhifadhi aina zao mbalimbali katika dunia yote.
Pia na kwa ndege wa angani, lete saba wa kiume na saba wa kike, ili kuhifadhi kizazi chao juu ya uso wa nchi yote.
4 Siku saba kuanzia sasa nitaleta mvua juu ya nchi kwa siku arobaini usiku na mchana, nami nitafutilia mbali kutoka uso wa nchi kila kiumbe hai nilichokiumba.”
Kwa kuwa ndani ya siku saba nitasababisha mvua kunyesha juu ya nchi muda wa siku arobaini mchana na usiku. Nitaharibu kila kiumbe hai nilichokiumba juu ya uso wa ardhi.”
5 Noa akafanya yote kama Bwana alivyomwamuru.
Nuhu alifanya yote ambayo Yahwe alimuagiza.
6 Noa alikuwa na miaka 600 gharika ilipokuja juu ya dunia.
Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia sita wakati gharika ilipokuja juu ya nchi.
7 Noa na mkewe na wanawe na wake zao wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika.
Nuhu, watoto wake wa kiume, mke wake, na wake za watoto wake waliingia katika safina pamoja kwa sababu ya maji ya gharika.
8 Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vitambaavyo,
Wanyama ambao ni safi na wanyama ambao si safi, ndege, na kila kitambaacho juu ya ardhi,
9 wa kiume na wa kike, walikuja kwa Noa wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Noa.
wawili wawili mume na mke wakaja kwa Nuhu na wakaingia katika safina, kama vile Mungu alivyokuwa amemwagiza Nuhu.
10 Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia.
Ikawa kwamba baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya nchi.
11 Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili mwaka wa 600 wa kuishi kwake Noa, siku hiyo ndipo chemchemi zote hata zilizo chini sana ya ardhi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa.
Katika mwaka wa mia sita wa maisha yake Nuhu, katika mwezi wa pili, katika siku ya kumi na saba ya mwezi, katika siku iyo hiyo, chemchemi zote za vilindi vikuu zilipasuka na kufunguka, na madirisha ya mbinguni yakafunguka.
12 Mvua ikanyesha juu ya nchi siku arobaini usiku na mchana.
Mvua ikaanza kunyesha juu ya nchi kwa siku arobaini mchana na usiku.
13 Siku hiyo Noa, na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao wakaingia katika ile safina.
Katika siku iyo hiyo Nuhu pamoja na watoto wake, Shem, Ham, na Yafethi na mke wa Nuhu, na wale wake watatu wa wana wa Nuhu pamoja waliingia katika safina.
14 Nao walikuwa pamoja na kila mnyama wa mwituni kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa.
Waliingia pamoja na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho juu ya ardhi kwa jinsi yake, na kila aina ya ndege kwa jinsi yake, kila aina ya kiumbe chenye mabawa.
15 Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai ndani yake vikaja kwa Noa viwili viwili, vikaingia katika safina.
Viwili viwili katika kila chenye mwili ambacho kilikuwa na pumzi ya uhai kilikuja kwa Nuhu na kuingia katika safina.
16 Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Noa, ndipo Bwana akamfungia ndani.
Wanyama walioingia ndani walikuwa wakiume na kike katika wote wenye mwili; wakaingia kama vile Mungu alivyokuwa amemwagiza. Kisha Yahwe akawafungia mlango.
17 Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani na maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka kwenye uso wa nchi.
Kisha gharika ikaja juu ya nchi kwa siku arobaini, na maji yakaongezeka na kuinua safina juu ya nchi.
18 Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji.
Maji yakafunika kabisa nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji.
19 Maji yakazidi kujaa juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote.
Maji yakaongezeka zaidi juu ya nchi kiasi kwamba milima yote mirefu ambayo ilikuwa chini ya anga ikafunikwa.
20 Maji yakaendelea kujaa yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano.
Maji yakaongezeka dhiraa kumi na tano juu ya vilele vya milima.
21 Kila kiumbe hai kitambaacho juu ya nchi kikaangamia: Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama pori, viumbe vyote juu ya nchi na wanadamu wote.
Vitu vyote vyenye uhai ambavyo vilitembea juu ya nchi vilikufa: ndege, mifugo, wanyama wa mwituni, viumbe hai vyote kwa wingi vilivyoishi juu ya nchi, pamoja na watu.
22 Kila kiumbe juu ya nchi kavu chenye pumzi ya uhai kikafa.
Viumbe hai vyote ambavyo vilikaa juu ya ardhi, vilivyo pumua pumzi ya uhai kwa njia ya pua, vilikufa.
23 Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Noa peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.
Hivyo kila kilichokuwa hai ambacho kilikuwa juu ya uso wa mchi kilifutwa, kuanzia watu mpaka wanyama wakubwa, mpaka vitambaavyo, na mpaka ndege wa angani. Vyote viliangamizwa kutoka kwenye nchi. Nuhu tu pamoja na wale waliokuwa naye kwenye safina ndio walisalia.
24 Maji yakaifunika dunia kwa siku 150.
Maji haya kuzama chini ya nchi kwa muda wa siku miamoja na hamsini.

< Mwanzo 7 >

The Great Flood
The Great Flood