< Mwanzo 7 >
1 Ndipo Bwana akamwambia Noa, “Ingia katika safina wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki.
2 Uchukue wanyama saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, na wanyama wawili wawili wa kila aina walio najisi wa kiume na wa kike.
3 Pia uchukue ndege saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, ili kuhifadhi aina zao mbalimbali katika dunia yote.
4 Siku saba kuanzia sasa nitaleta mvua juu ya nchi kwa siku arobaini usiku na mchana, nami nitafutilia mbali kutoka uso wa nchi kila kiumbe hai nilichokiumba.”
5 Noa akafanya yote kama Bwana alivyomwamuru.
6 Noa alikuwa na miaka 600 gharika ilipokuja juu ya dunia.
7 Noa na mkewe na wanawe na wake zao wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika.
8 Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vitambaavyo,
9 wa kiume na wa kike, walikuja kwa Noa wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Noa.
10 Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia.
11 Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili mwaka wa 600 wa kuishi kwake Noa, siku hiyo ndipo chemchemi zote hata zilizo chini sana ya ardhi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa.
12 Mvua ikanyesha juu ya nchi siku arobaini usiku na mchana.
13 Siku hiyo Noa, na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao wakaingia katika ile safina.
14 Nao walikuwa pamoja na kila mnyama wa mwituni kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa.
15 Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai ndani yake vikaja kwa Noa viwili viwili, vikaingia katika safina.
16 Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Noa, ndipo Bwana akamfungia ndani.
17 Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani na maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka kwenye uso wa nchi.
18 Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji.
19 Maji yakazidi kujaa juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote.
20 Maji yakaendelea kujaa yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano.
21 Kila kiumbe hai kitambaacho juu ya nchi kikaangamia: Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama pori, viumbe vyote juu ya nchi na wanadamu wote.
22 Kila kiumbe juu ya nchi kavu chenye pumzi ya uhai kikafa.
23 Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Noa peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.
24 Maji yakaifunika dunia kwa siku 150.
The Great Flood