< Mwanzo 50 >

1 Basi Yosefu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu.
Yusufu akahuzunika sana hata akauangukia uso wa baba yake, akamlilia, na kumbusu.
2 Ndipo Yosefu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa ili asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze,
Yusufu akawaagiza watumishi wake matabibu kumtia dawa babaye. Hivyo matabibu wakampaka dawa Israeli.
3 wakatumia siku arobaini, kwa maana ndio muda uliotakiwa wa kutia dawa ili asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini.
Wakatimiza siku arobain, kwani huo ndio uliokuwa muda kamili wa kutia dawa. Wamisri wakamlilia kwa siku sabini
4 Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yosefu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni,
Siku za maombolezo zilipotimia, Yusufu akaongea na watumishi wa baraza la kifalme wa Farao kusema, “Ikiwa nimepata kibali machoni penu, tafadharini ongeeni na Farao, kusema,
5 ‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’”
'Baba yangu aliniapisha, kusema, “Tazama, ninakaribia kufa. Unizike katika kaburi nililolichimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani. Ndipo utakaponizika.” Basi sasa niruhusu niende nimzike baba yangu, na kisha nitarudi.”
6 Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.”
Farao akajibu, “Nenda na umzika baba yako, kama alivyokuwapisha.”
7 Hivyo Yosefu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake na watu mashuhuri wote wa Misri.
Yusufu akaenda kumzika baba yake. Maofisa wa Farao wote wakaenda pamoja naye - washauri wa nyumba yake, maofisa waandamizi wote wa nchi ya Misri,
8 Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani kwa Yosefu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni.
pamoja na nyumba yote ya Yusufu na ndugu zake, na nyumba yote ya baba yake. Lakini watoto wao, kondoo wao na makundi ya mbuzi wao yaliachwa katika nchi ya Gosheni.
9 Magari makubwa na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana.
Vibandawazi na wapanda farasi pia walikwenda pamoja naye. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu.
10 Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu; Yosefu akapumzika huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake.
Hata walipokuja katika sakafu ya kupuria ya Atadi upande mwingine wa Yordani, wakaomboleza kwa majonzi ya huzuni kubwa. Yusufu akafanya maombolezo ya siku saba kwa ajili ya babaye pale.
11 Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu.
Wenyeji wa nchi, Wakanaani, walipoona maombolezo katika sakafu ya Atadi, wakasema, “Hili ni tukio la kuhuzunisha sana kwa Wamisri.” Ndiyo maana eneo hilo likaitwa Abeli Mizraimu, lililoko mbele ya Yordani.
12 Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza:
Hivyo wanawe wakamfanyia Yakobo kama alivyokuwa amewaagiza.
13 Wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Abrahamu alilinunua kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia.
Wana wake wakampeleka katika nchi ya Kanaani na wakamzika katika pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre. Ibrahimi alikuwa amelinunua pango pamoja na shamba kwa ajili ya eneo la kuzikia. Alikuwa amelinunua kutoka kwa Efroni Mhiti.
14 Baada ya Yosefu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wamekwenda naye kumzika baba yake.
Baada ya kuwa amemzika babaye, Yusufu akarudi Misri, yeye, pamoja na ndugu zake, na wote waliokuwa wamemsindikiza ili kumzika babaye.
15 Ndugu zake Yosefu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yosefu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?”
Nduguze Yusufu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje ikiwa Yusufu atatukasirikia na akataka kutulipa kikamilifu kwa ajili ya uovu tuliomtenda?”
16 Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya:
Hivyo wakamwagiza Yusufu, kusema, “Baba yako alitoa maelekezo kabla hajafa, kusema,
17 ‘Hili ndilo mtakalomwambia Yosefu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yosefu akalia.
'Mwambieni hivi Yusufu, “Tafadhari samehe makosa ya ndugu zako na dhambi yao uovu waliokutenda.” Basi wasamehe watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yusufu akalia walipomwambia.
18 Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.”
Ndugu zake pia wakaenda na kuinamisha nyuso zao mbele zake. Wakasema, “Tazama, sisi ni watumishi wako.”
19 Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu?
Lakini Yusufu akawajibu, “Msiogope, Je mimi ni badala ya Mungu?
20 Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi.
Lakini kwenu, mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, kuhifadhi maisha ya watu wengi, kama mwonavyo leo.
21 Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawahakikishia na kusema nao kwa wema.
Hivyo basi msiogope. Nitawahudumia ninyi na watoto wenu wadogo.” Kwa njia hii aliwatia moyo na kuongea na mioyo yao kwa upole.
22 Yosefu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka 110,
Yusufu akakaa Misri, pamoja na familia ya baba yake. Akaishi miaka mia moja na kumi.
23 naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yosefu walipozaliwa.
Yusufu akawaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu. Pia aliwaona wana wa Makiri mwana wa Manase, waliowekwa katika magoti ya Yusufu.
24 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Abrahamu, Isaki na Yakobo.”
Yusufu akawambia ndugu zake, “Ninakaribia kufa; lakini kwa hakika Mungu atawajilia na kuwaongoza kutoka katika nchi hii na kuwapeleka katika nch aliyoapa kumpa Ibrahimu, kwa Isaka na kwa Yakobo.”
25 Naye Yosefu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.”
Kisha Yusufu akawaapisha watu wa Israeli kwa kiapo. Akasema, “Bila shaka Mungu atawajilia. Wakati huo mtachukuwa mifupa yangu kutoka hapa.”
26 Kwa hiyo Yosefu akafa akiwa na umri wa miaka 110. Baada ya kumtia dawa ili asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.
Hivyo Yusufu akafa, mwenye miaka 110. Wakampaka dawa na akawekwa katika jeneza huko Misri.

< Mwanzo 50 >