< Mwanzo 47 >
1 Yosefu akaenda na kumwambia Farao, “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka nchi ya Kanaani wakiwa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na kila kitu walicho nacho, nao sasa wapo huko Gosheni.”
2 Akachagua ndugu zake watano na kuwaonyesha kwa Farao.
3 Farao akawauliza hao ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?” Wakamjibu, “Watumishi wako ni wachunga mifugo, kama vile baba zetu walivyokuwa.”
4 Pia wakamwambia Farao, “Tumekuja kukaa huku kwa muda mfupi, kwa sababu njaa ni kali huko Kanaani, na mifugo ya watumishi wako haina malisho. Kwa hiyo sasa, tafadhali uruhusu watumishi wako wakae huko Gosheni.”
5 Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako,
6 nayo nchi ya Misri ipo mbele yako, uwakalishe baba yako na ndugu zako katika sehemu iliyo bora kupita zote katika nchi. Na waishi Gosheni. Kama unamfahamu yeyote miongoni mwao mwenye uwezo maalum, waweke wawe wasimamizi wa mifugo yangu.”
7 Ndipo Yosefu akamleta Yakobo baba yake na kumtambulisha mbele ya Farao. Baada ya Yakobo kumbariki Farao,
8 Farao akamuuliza, “Je una umri gani?”
9 Naye Yakobo akamwambia Farao, “Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni miaka 130. Miaka yangu imekuwa michache na ya taabu, wala haikufikia miaka ya kusafiri ya baba zangu.”
10 Kisha Yakobo akambariki Farao, naye akaondoka mbele ya uso wake.
11 Ndipo Yosefu akawakalisha baba yake na ndugu zake katika nchi ya Misri na kuwapa milki katika sehemu bora sana ya nchi, wilaya ya Ramesesi, kama Farao alivyoelekeza.
12 Pia Yosefu akampa baba yake, na ndugu zake na wote wa nyumbani mwa baba yake vyakula, kwa kulingana na hesabu ya watoto wao.
13 Hata hivyo, hapakuwepo chakula katika sehemu yote kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana; Misri na Kanaani zote zikaharibiwa kwa sababu ya njaa.
14 Yosefu akakusanya fedha zote zilizopatikana kutoka mauzo ya nafaka huko Misri na Kanaani, akazileta kwenye jumba la kifalme la Farao.
15 Fedha za watu wa Misri na Kanaani zilipokwisha, Wamisri wote wakamjia Yosefu na kumwambia, “Tupatie chakula. Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Fedha zetu zimekwisha.”
16 Yosefu akawaambia, “Basi leteni mifugo yenu, nitawauzia chakula kwa kubadilisha na mifugo yenu, kwa kuwa fedha zenu zimekwisha.”
17 Kwa hiyo wakaleta mifugo yao kwa Yosefu, naye akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi zao, kondoo na mbuzi zao, ngʼombe na punda zao. Katika mwaka huo wote Yosefu akawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote.
18 Mwaka ule ulipokwisha, wakamjia mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatuwezi kuficha ukweli mbele za bwana wetu kwamba, kwa kuwa fedha zetu zimekwisha na wanyama wetu ni mali yako, sasa hakuna chochote kilichosalia kwa ajili ya bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu.
19 Kwa nini tuangamie mbele ya macho yako, sisi pamoja na nchi yetu? Utununue sisi pamoja na ardhi yetu ili kubadilishana kwa chakula. Nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe sisi mbegu ili tuweze kuishi wala tusife, nchi yetu isije ikawa ukiwa.”
20 Kwa hiyo Yosefu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Wamisri, mmoja baada ya mwingine, waliuza mashamba yao, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana kwao. Nchi ikawa mali ya Farao,
21 naye Yosefu akawafanya watu watumike kama watumwa, kuanzia upande mmoja wa Misri hadi upande mwingine.
22 Hata hivyo, hakununua nchi ya makuhani, kwa sababu walikuwa wanapata mgawo wao wa kawaida kutoka kwa Farao, nao walikuwa na chakula cha kuwatosha kutokana na mgawo waliopewa na Farao. Hii ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao.
23 Yosefu akawaambia watu, “Kwa vile nimewanunua ninyi pamoja na nchi yenu leo kuwa mali ya Farao, hapa kuna mbegu kwa ajili yenu ili mweze kuziotesha.
24 Lakini wakati mazao yatakapokuwa tayari, mpeni Farao sehemu ya tano. Sehemu hizo nne zitakazobaki mtaziweka kama mbegu kwa ajili ya mashamba na kwa ajili ya chakula chenu wenyewe na cha watu wa nyumbani mwenu na watoto wenu.”
25 Wakamwambia, “Umeokoa maisha yetu. Basi na tupate kibali mbele ya macho ya bwana wetu; tutakuwa watumwa wa Farao.”
26 Basi Yosefu akaiweka iwe sheria kuhusu nchi ya Misri, ambayo inatumika mpaka leo, kwamba, sehemu ya tano ya mazao ni mali ya Farao. Ni nchi ya makuhani tu ambayo haikuwa ya Farao.
27 Basi Waisraeli wakaishi Misri katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali huko wakastawi na kuongezeka kwa wingi sana.
28 Yakobo akaishi Misri miaka kumi na saba, nayo miaka ya maisha yake ilikuwa 147.
29 Wakati ulipokaribia wa Israeli kufa, akamwita mwanawe Yosefu na kumwambia, “Kama nimepata kibali machoni pake, weka mkono wako chini ya paja langu na uniahidi kuwa utanifanyia fadhili na uaminifu. Usinizike Misri,
30 lakini nitakapopumzika na baba zangu, unichukue kutoka Misri, ukanizike walipozikwa.” Yosefu akamwambia, “Nitafanya kama unavyosema.”
31 Akamwambia, “Niapie.” Ndipo Yosefu akamwapia, naye Israeli akaabudu, akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.