< Mwanzo 46 >
1 Hivyo Israeli akaondoka na vyote vilivyokuwa mali yake, naye alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaki baba yake.
Israeli akasafiri na yote aliyokuwa nayo na akaja Beersheba. Pale akatoa sadaka kwa Mungu wa Isaka baba yake.
2 Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!” Akajibu, “Mimi hapa.”
Mungu akamwambia Israeli katika ndoto usiku, akisema, “Yakobo, Yakobo.”
3 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa.
Akasema, “Mimi hapa.” Akasema, “Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako. Usiogope kushuka Misri, kwa maana nitakufanya taifa kubwa huko.
4 Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yosefu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”
Nitakwenda pamoja nawe huko Misri, Nami nitakupandisha huku tena bila shaka. Na Yusufu akayafunika macho yako kwa mikono wake.”
5 Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao aliyokuwa amempelekea kumsafirisha.
Yakobo akainuka kutoka Beersheba. Wana wa Israeli wakamsafirisha Yakobo baba yao, watoto wao, na wake wao, katika mikokotene ambayo Farao alikuwa ameipeleka kuwachukua.
6 Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri.
Wakachukua mifugo yao na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani. Wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye.
7 Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote mpaka Misri.
Akaja Misri pamoja na wanawe na wana wa wanawe, binti zake na wana wa binti zake, na uzao wake wote.
8 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), waliokwenda Misri: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.
Haya ni majina ya watoto wa Israeli waliokuja Misri, Yakobo na wanawe: Rubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo;
9 Wana wa Reubeni ni: Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi.
wana wa Rubeni Hanoki na Palu na Hezroni na Karmi;
10 Wana wa Simeoni ni: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.
wana wa Simoni, Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Zohari, na Shauli, wana wa mwanamke Mkanaani;
11 Wana wa Lawi ni: Gershoni, Kohathi na Merari.
wana wa Lawi Gershoni, Kohathi, na Merari.
12 Wana wa Yuda ni: Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani). Wana wa Peresi ni: Hesroni na Hamuli.
Wana wa Yuda: Eri, Shela, Peresi, na Zera, (Lakini Eri na Onani walikufa katika nchi ya Kanaani). Na wana wa Peresi walikuwa Hezroni na Hamuli.
13 Wana wa Isakari ni: Tola, Puva, Yashubu na Shimroni.
Wana wa Isakari walikuwa Tola, Puva, Lobu, na Shimroni;
14 Wana wa Zabuloni ni: Seredi, Eloni na Yaleeli.
Wana wa Zabuloni walikuwa Seredi, Eloni, na Yahleeli
15 Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu pamoja na binti yake Dina. Jumla ya wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.
Hawa walikuwa wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padani Aramu, pamoja na na Dina binti yake. Wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.
16 Wana wa Gadi ni: Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.
Wana wa Gadi walikuwa Zifioni, Hagi, Shuni, Ezboni, Eri, Arodi, na Areli.
17 Wana wa Asheri ni: Imna, Ishva, Ishvi na Beria. Dada yao alikuwa Sera. Wana wa Beria ni: Heberi na Malkieli.
Wana wa Asheri walikuwa Imna, Ishva, Ishvi, na Beria; na Sera alikuwa dada yao. Wana wa Beria walikuwa Heberi na Malkieli.
18 Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambao Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita.
Hawa walikuwa wana wa Zilpa, ambaye Labani alikuwa amempa Lea binti yake. Wana aliomzalia Yakobo wote walikuwa kumi na sita.
19 Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni: Yosefu na Benyamini.
Wana wa Raheli mkewe Yakobo walikuwa Yusufu na Benjamini.
20 Huko Misri, Asenathi binti wa Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yosefu wana wawili, Manase na Efraimu.
Huko Misri Manase na Efraimu walizaliwa kwa Yusufu na Asenathi, binti Potifera kuhani wa Oni.
21 Wana wa Benyamini ni: Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.
Wana wa Benjamini walikuwa Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu, na Ardi.
22 Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne.
Hawa walikuwa wana wa Raheli waliozaliwa kwa Yakobo - jumla yao kumi na wanne.
23 Mwana wa Dani ni: Hushimu.
Mwana wa Dani alikuwa Hushimu.
24 Wana wa Naftali ni: Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu.
Wana wa Naftali walikuwa Yahzeeli, Guni, Yezeri, na Shilemi.
25 Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.
Hawa walikuwa wana Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alimpa Raheli binti yake - wote walikuwa saba.
26 Wote waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe zake, walikuwa watu sitini na sita.
Wate waliokwenda na Yakobo, waliokuwa uzao wake, bila kuhesabu wake wa wana wa Yakobo walikuwa sitini na sita.
27 Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yosefu huko Misri, jumla yote ya jamaa ya Yakobo, waliokwenda Misri, walikuwa sabini.
Pamoja na wana wawili wa Yusufu waliozaliwa kwake huko Misri, watu wa familia yake waliokwenda Misri walikuwa sabini jumla yao.
28 Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yosefu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni,
Yakobo akamtuma Yuda kuwatangulia mbele kwa Yusufu kuonesha njia mbele yake kwenda Gosheni, nao wakaja katika eneo la Gosheni.
29 gari kubwa zuri la Yosefu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yosefu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.
Yusufu akaandaa kibandawazi chake na akaenda kumlaki baba yake huko Gosheni. Akamwona, akaikumbatia shingo yake, na akalia shingoni mwake kwa kitambo.
30 Israeli akamwambia Yosefu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”
Israeli akamwambia Yusufu, “Basi na nife sasa, kwa kuwa nimeuona uso wako, kwamba bado uko hai.”
31 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu.
Yusufu akawambia ndungu zake na nyumba ya baba yake, “Nitakwenda na kumwambia Farao, kusema, 'Ndugu zangu na nyumba ya baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia.
32 Watu hao ni wachunga mifugo, huchunga mifugo, wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ngʼombe pamoja na kila kitu walicho nacho.’
Watu hawa ni wafugaji, kwani wamekuwa watunza wanyama. Wamekuja na makundi yao ya kondoo, na mbuzi, na vyote walivyonavyo.'
33 Farao atakapowaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’
Itakuwa, Farao atakapowaita na kuwauliza, 'Kazi yenu ni ipi?'
34 Mjibuni, ‘Watumwa wako wamekuwa wachunga mifugo tangu ujana wetu mpaka sasa, kama baba zetu walivyofanya.’ Ndipo mtakaporuhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wachunga mifugo wote ni chukizo kwa Wamisri.”
mwambieni, 'Watumishi wako wamekuwa watunza wanyama tangu ujana wetu mpaka sasa, sisi, na baba zetu.' Fanyeni hivyo ili mweze kuishi katika nchi ya Gosheni, kwani kila mfugaji ni chukizo kwa Wamisri.”