< Mwanzo 44 >

1 Kisha Yosefu akampa yule msimamizi wa nyumbani mwake maagizo haya: “Jaza magunia ya watu hawa kiasi cha chakula ambacho wanaweza kuchukua, na uweke fedha ya kila mtu kwenye mdomo wa gunia lake.
Yusufu akamwamru msimamizi wa nyumba yake, akisema, “Jaza magunia ya watu hawa kwa chakula, kiasi wawezacho kubeba, na uweke pesa ya kila mtu katika mdomo wa gunia lake.
2 Kisha weka kikombe changu kile cha fedha kwenye mdomo wa gunia la yule mdogo wa wote pamoja na fedha zake ambazo angenunulia nafaka yake.” Naye akafanya kama Yosefu alivyosema.
Uweke kikombe changu, cha fedha, katika mdomo wa gunia la mdogo, na pesa yake ya chakula pia.” Msimamizi akafanya kama Yusufu alivyosema.
3 Kulipopambazuka, hao watu wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda zao.
Kukapambazuka asubuhi, na wale watu wakaruhusiwa kuondoka, wao na punda zao.
4 Kabla hawajafika mbali kutoka mjini, Yosefu akamwambia mtumishi wake, “Wafuatilie wale watu mara moja, utakapowakuta, waambie, ‘Kwa nini mmelipiza wema kwa ubaya?
Walipokuwa wametoka mjini lakini hawajafika mbali, Yusufu akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Inuka, uwafuatie wale watu, na utakapowapata, wambie, 'Kwa nini mmelipa uovu badala ya mema?
5 Je, kikombe hiki sicho anachonywea bwana wangu na pia hukitumia kwa kutabiri mambo yajayo? Hili ni jambo ovu mlilolitenda.’”
Je hiki siyo kikombe ambacho bwana wangu hukinywea, na kikombe akitumiacho kwa uaguzi? Mmefanya vibaya, kwa jambo hili mlilolifanya.”
6 Alipowafikia, akarudia maneno haya kwao.
Msimamizi wa nyumba akawapata na kuwambia maneno haya.
7 Lakini wakamwambia mtumishi, “Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Liwe mbali na watumishi wako wasije wakafanya jambo kama hilo!
Wakasema, “Kwa nini bwana wetu anasema maneno kama haya? Na iwe mbali na watumishi wako kwamba wanaweza kufanya jambo hili.
8 Hata hivyo tulikurudishia zile fedha kutoka nchi ya Kanaani ambazo tulizikuta kwenye midomo ya magunia yetu. Hivyo kwa nini tuibe fedha au dhahabu kutoka nyumbani kwa bwana wako?
Tazama, pesa tulizozikuta katika midomo ya magunia yetu, tulizileta kwako kutoka katika nchi ya Kanaani. Ni kwa jinsi gani basi tunaweza kuiba katika nyumba ya bwana wako fedha au dhahabu?
9 Ikiwa yeyote miongoni mwa watumishi wako atapatikana nacho, auawe, na sisi wengine tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”
Yeyote kitakayeonekana kwake miongoni mwa watumishi wako, atakufa, nasi sote tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”
10 Akajibu, “Vema sana; na iwe kama msemavyo. Yeyote atakayekutwa nacho atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine mtakuwa hamna lawama.”
Msimamizi akasema, “Basi na iwe kwa kadili ya maneno yenu. Yeye ambaye kikombe kitaonekana kwake atakuwa mtumwa wangu, nanyi wengine mtakuwa bila hatia.”
11 Kila mmoja wao akafanya haraka kushusha gunia lake chini na kulifungua.
Kisha kila mtu akaharakisha na kulishusha gunia lake chini. na kila mtu akalifungua gunia lake.
12 Ndipo msimamizi akaendelea kutafuta, akianzia kwa mkubwa wa wote na akaishia kwa mdogo wa wote. Basi kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini.
Msimamizi akatafuta. akaanza na mkubwa wa wote na kumaliza kwa mdogo wa wote, na kikombe kikaonekana katika gunia la Benjamini.
13 Kwa jambo hili, wakararua nguo zao. Ndipo wote wakapakiza mizigo yao juu ya punda zao na kurudi mjini.
Wakararua mavazi yao. Kila mtu akapakia juu ya punda wake nao wakarudi mjini.
14 Yosefu alikuwa bado yuko nyumbani mwake wakati Yuda na kaka zake walipoingia, wote wakajitupa chini mbele yake.
Yuda na ndugu zake wakaja katika nyumba ya Yusufu. Bado alikuwepo pale, nao wakainama mbele zake hata chini.
15 Yosefu akawaambia, “Ni jambo gani hili mlilolifanya? Hamjui kuwa mtu kama mimi anaweza kufahamu mambo kwa njia ya kutabiri?”
Yusufu akawambia, “Je ni nini hili mlilolifanya? Je hamjui kwamba mtu kama mimi anafanya uaguzi.
16 Yuda akajibu, “Tutaweza kusema nini kwa bwana wangu? Tutaweza kuzungumza nini? Tutawezaje kuthibitisha kwamba hatuna hatia? Mungu amefunua hatia ya watumishi wako. Sasa sisi tu watumwa wa bwana wangu, sisi wenyewe pamoja na yule aliyepatikana na kikombe.”
Yuda akasema, “Je tunaweza kumwambia nini bwana wangu? Tuseme nini? au ni jinsi gani twaweza kujithibitisha wenyewe? Mungu ameona uovu wa watumishi wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, wote sisi na yule ambaye kikombe kimeonekana mkononi mwake.”
17 Lakini Yosefu alisema, “Liwe mbali nami kufanya jambo kama hili! Mtu yule tu aliyekutwa na kikombe ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Ninyi wengine, rudini kwa baba yenu kwa amani.”
Yusufu akasema, “Na iwe mbali nami kwamba naweza kufanya hivyo. Mtu ambaye kikombe kimeonekana mkononi mwake, huyu ndiye atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine, nendeni kwa amani kwa baba yenu.”
18 Ndipo Yuda akamwendea na kumwambia: “Tafadhali bwana wangu, mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa bwana wangu. Usimkasirikie mtumishi wako, ingawa wewe ni sawa na Farao mwenyewe.
Ndipo Yuda alipomkaribia na kusema, “Bwana wangu, tafadhari mwache mtumishi wako aseme neno katika masikio ya bwana wangu, na usiziache hasira zako kuwaka dhidi ya mtumishi wako, kwani wewe ni kama Farao.
19 Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, ‘Mnaye baba au ndugu?’
Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, kusema, Je mnaye baba au ndugu?'
20 Nasi tukakujibu, ‘Tunaye baba yetu ambaye ni mzee; pia yupo mwanawe mdogo aliyezaliwa katika uzee wake. Ndugu yake amekufa, na huyu mdogo ndiye mwana pekee kwa mama yake aliyebaki, naye baba yake anampenda.’
Nasi tukamwambia bwana wangu, 'Tunaye baba, ni mzee, na mwana wa uzee wake, ni mdogo. Na ndugu yake alishakufa, na yeye peke yake ndiye amebaki kwa mama yake, na baba yake anampenda.'
21 “Ndipo ulipowaambia watumishi wako, ‘Mleteni kwangu ili niweze kumwona kwa macho yangu mwenyewe.’
Nawe ukawambia matumishi wako, 'Mleteni ili nimwone.'
22 Nasi tukamwambia bwana wangu, ‘Kijana hawezi kumwacha baba yake; akimwacha, baba yake atakufa.’
Nasi tukamwambia bwana wangu, 'Kijana hawezi kumwacha babaye. Kwani akimwacha babaye baba yake angekufa.'
23 Lakini ukawaambia watumishi wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’
Na ukawambia watumishi wako, 'Mdogo wenu asipokuja pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.'
24 Tuliporudi nyumbani kwa mtumwa wako baba yangu, tulimwambia lile bwana wangu alilokuwa amesema.
Na ikawa tulipokwenda kwa mtumishi wako baba yangu, tulimwambia maneno ya bwana wangu.
25 “Ndipo baba yetu aliposema, ‘Rudini Misri mkanunue chakula kingine.’
Na baba yetu akasema, Nendeni tena, mkatununulie chakula.'
26 Lakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka Misri mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi ndipo tutakapokwenda. Hatutaweza kuuona uso wa yule mtu mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi.’
Nasi tukasema, “Hatuwezi kushuka. Ikiwa mdogo wetu atakuwa nasi, ndipo tutakaposhuka, kwani hatuwezi kuuona uso wa mtu yule mdogo wetu asipokuwa pamoja nasi.'
27 “Mtumwa wako baba yangu alituambia, ‘Mnajua mke wangu alinizalia wana wawili.
Mtumishi wako baba yetu akatwambia, 'Mnajua kwamba mke wangu alinizalia wana wawili.
28 Mmojawapo alipotea, nami nikasema, “Hakika ameraruliwa vipande vipande.” Nami sijamwona tangu wakati huo.
Na mmoja akatoka kwangu nami nikasema, “Bila shaka ameraruliwa vipande, na tangu hapo sijamwona.”
29 Ikiwa mtaniondolea huyu tena na akapatwa na madhara, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini nikiwa mwenye huzuni.’ (Sheol h7585)
Nanyi mkimchukua huyu naye kutoka kwangu mabaya yanaweza kumpata, mtashusha mvi zangu kwa kaburini kwa huzuni. (Sheol h7585)
30 “Hivyo sasa, kama kijana hatakuwa pamoja nasi nitakaporudi kwa mtumishi wako baba yangu, na kama baba yangu, ambaye maisha yake yamefungamanishwa na uhai wa kijana huyu,
Kwa hiyo, basi, nitapokuja kwa mtumishi wako baba yangu, na kijana hayupo nasi, kwa kuwa uhai wake umefungamanishwa katika uhai wa kijana,
31 akiona kijana hayupo nasi, atakufa. Watumishi wako watashusha kichwa chenye mvi cha baba yetu kaburini kwa huzuni. (Sheol h7585)
itakuwa, atakapoona kwamba kijana hayupo nasi atakufa. Na watumishi wako watazishusha mvi za mtumishi wako baba yetu kaburini kwa masikitiko. (Sheol h7585)
32 Mtumwa wako alimhakikishia baba yangu usalama wa kijana. Nikamwambia, ‘Kama sikumrudisha kwako nitakuwa mwenye lawama mbele yako, baba yangu, maisha yangu yote!’
Kwani mtumishi wako alikuwa mdhamini wa kijana kwa baba yangu na alisema, 'Ikiwa sitamleta kwako, ndipo nitakapokuwa mwenye hatia kwa baba yangu daima.”
33 “Sasa basi, tafadhali mruhusu mtumishi abaki hapa kama mtumwa wa bwana wangu badala ya kijana, naye kijana umruhusu arudi na ndugu zake.
Kwa hiyo sasa, tafadhari mwache mtumishi wake akae kama mtumwa kwa bwana wangu badala ya kijana, na umwache kijana aende na ndugu zake.
34 Ninawezaje kurudi kwa baba yangu kama kijana hatakuwa pamoja nami? La hasha! Usiniache nikaone huzuni ile itakayompata baba yangu.”
Kwa maana nitakwenda jinsi gani kwa baba yangu ikiwa kijana hayupo nami? Ninaogopa kuona mabaya yatakayompata baba yangu.”

< Mwanzo 44 >