< Mwanzo 43 >
1 Wakati huu njaa ilikuwa bado ni kali mno katika nchi.
Njaa ilikuwa kali katika nchi.
2 Hivyo wakati walikuwa wamemaliza kula nafaka yote waliyoileta kutoka Misri, Yakobo baba yao akawaambia, “Rudini Misri mkatununulie chakula kingine zaidi.”
Ikawa walipokuwa wametumia chakula chote walichokitoa Misri, baba yao akawambia, “Nendeni tena; mtununulie chakula.”
3 Lakini Yuda akamwambia, “Mtu yule alituonya kwa msisitizo, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje na ndugu yenu.’
Yuda akamwambia, “Yule mtu alituonya kwa ukali, 'Hamtauona uso wangu ndugu yenu asipokuwa nanyi.'
4 Kama utakubali ndugu yetu aende pamoja nasi, tutakwenda kuwanunulia chakula.
Ikiwa utamtuma ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kuwanunulia chakula.
5 Lakini ikiwa hutamruhusu aende, hatutakwenda, kwa sababu mtu yule alituambia, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje pamoja na ndugu yenu.’”
Lakini usipompeleka, hatutashuka. Kwa maana yule mtu alitwambia, 'Hamtauona uso wangu ndugu yenu asipokuwa nanyi.”
6 Israeli akauliza, “Kwa nini mkaniletea taabu hii kwa kumwambia yule mtu mlikuwa na ndugu mwingine?”
Israeli akawambia, “Kwa nini mlinitendea mimi vibaya hivyo kwa kumwambia mtu huyo kwamba mnaye ndugu mwingine?”
7 Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa undani sana habari zetu na za jamaa yetu. Alituuliza, ‘Je, baba yenu bado yungali hai? Je mnaye ndugu mwingine?’ Sisi tulimjibu maswali yake tu. Tungewezaje kujua kwamba angesema, ‘Mleteni mdogo wenu hapa’?”
Wakasema, “Yule mtu alituuliza habari zetu na familia yetu kwa kina. Akasema, 'Je baba yenu bado yuko hai? Je mnaye ndugu mwingine?'Tukamjibu kulingana na maswali haya. Tungejuaje kwamba angetwambia, 'Mleteni ndugu yenu?”
8 Ndipo Yuda akamwambia baba yake Israeli, “Mtume kijana pamoja nami, nasi tutaondoka mara, ili sisi na wewe pamoja na watoto wetu tuweze kuishi, wala tusife.
Yuda akamwambia Israeli baba yake, “Mtume kijana pamoja nami. Tutainuka na kwenda ili kwamba tuishi tusife, wote sisi, wewe, na hata watoto wetu.
9 Mimi mwenyewe nitakuhakikishia usalama wake, mimi mwenyewe nitawajibika kumrudisha. Ikiwa sitamrudisha kwako na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako maisha yangu yote.
Mimi nitakuwa mdhamini wake. Utaniwajibisha mimi. Kama nisipomleta na kumweka mbele yako, basi nibebe lawama daima.
10 Hakika, kama hatukuchelewa kuondoka, tungekuwa tumekwenda na kurudi mara mbili.”
Kwani kama tusingekawia, bila shaka hata sasa tungekuwa tumekwisha rudi mara ya pili.”
11 Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni baadhi ya mazao bora ya nchi katika mifuko yenu na mpelekeeni yule mtu kama zawadi, zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi.
Israeli baba yao akawambia, “Kama ni hivyo, basi fanyeni hivi. Chukueni baadhi ya mazao mazuri ya nchi katika mifuko yenu. Mchukulieni yule mtu zawadi: baadhi ya malhamu, asali, viungo na manemane, jozi na lozi.
12 Chukueni fedha mara mbili, kwa kuwa mtazirudisha zile fedha zilizowekwa midomoni mwa magunia yenu. Labda ziliwekwa kwa makosa.
Chukueni pesa mara mbili mikononi mwenu. Pesa iliyorudishwa katika magunia yenu, muichukue tena katika mikono yenu. Pengine walikosea.
13 Mchukueni ndugu yenu pia mrudi kwa huyo mtu mara moja.
Mchukueni ndugu yenu pia. Inukeni na mwende tena kwa mtu yule.
14 Naye Mungu Mwenyezi awajalieni rehema mbele ya huyo mtu ili apate kumwachia yule ndugu yenu na Benyamini mweze kurudi pamoja. Kwangu mimi kama nikufiwa nimefiwa.”
Mungu Mwenyezi na awape kuona rehema mbele ya huyo mtu, hivyo kwamba awafungulie ndugu yenu mwingine na Benjamini. Kama nikipotelewa na watoto, nimepotelewa.”
15 Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na walipofika wakajionyesha kwa Yosefu.
Watu wale wakachukua zawadi hii, na katika mikono yao wakachukua mara mbili ya kiasi cha pesa, pamoja na Benjamini. Wakaamka na kushuka Misri na kusimama mbele ya Yusufu.
16 Yosefu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani kwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”
Yusufu alipomwona Benjamini akiwa nao, akamwambia mtunzaji wa nyumba yake, “Walete watu hao ndani ya nyumba, chinja mnyama na umwandae, kwani watu hawa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”
17 Yule Msimamizi akafanya kama Yosefu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani kwa Yosefu.
Mtunzaji wa nyumba akafanya kama Yusufu alivyosema. Akawaleta wale watu nyumbani kwa Yusufu.
18 Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani kwa Yosefu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda zetu.”
Wale ndugu wakaogopa kwa vile walivyoletwa katika nyumba ya Yusufu. Wakasema, “Ni kwa sababu ya pesa iliyorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tulipoletwa ndani, kwamba atafute nafasi kinyume chetu. Kwamba aweze kutukamata na kutuchukua kama watumwa, na kuchukua punda wetu.” Wakamsogelea mtunzaji wa nyumba ya Yusufu,
19 Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yosefu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumbani.
nao wakaongea naye mlangoni mwa nyumba,
20 Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula.
wakisema, “Bwana wangu, tulikuja mara ya kwanza kununua chakula.
21 Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake, kwenye mdomo wa gunia lake kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha.
Ikawa, tulipofika katika eneo la kupumzikia, tukafungua magunia yetu, na, tazama, pesa ya kila mtu ilikuwa katika gunia lake, pesa yetu kwa kiasi kamili. Tumeileta katika mikono yetu.
22 Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.”
Tumekuja na pesa nyingine pia mikonon mwetu ili kununua chakula. Hatujui aliyeziweka pesa katika magunia yetu.”
23 Akawaambia, “Vema, msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni.
Mtunzaji wa nyumba akasema, “Amani iwe kwenu, msiogope. Mungu wenu na Mungu wa baba yenu ndiye aliyeweka pesa katika magunia yenu. Nilipokea pesa yenu.” Kisha mtunzaji wa nyumba akamleta Simoni kwao.
24 Msimamizi akawapeleka wale watu katika nyumba ya Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu na kuwapa punda wao majani.
Msimamizi wa nyumba akawapeleka watu hao katika nyumba ya Yusufu. Akawapa maji, nao wakaosha miguu yao. Akawalisha punda wao.
25 Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yosefu wakati atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko.
Wakaandaa zawadi kwa ajili ya Yusufu aliyekuwa akija mchana, kwani walikuwa wamesikia kwamba watakula pale.
26 Yosefu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi walizokuwa nazo, ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia hadi nchi.
Yusufu alipokuja nyumbani, wakaleta nyumbani zawadi iliyokuwa mikononi mwao, nao wakainama mbele yake hata chini.
27 Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?”
Akawauliza juu ya hali zao na kusema,”Je baba yenu hajambo, yule mzee mliyemnena? Je bado yu hai?”
28 Wakamjibu, “Mtumishi wako baba yetu bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama chini kumpa heshima.
Wakasema, “Mtumishi wako baba yetu hajambo. Na bado yu hai” Wakajinyenyekeza na kuinama chini.
29 Alipotazama na kumwona Benyamini ndugu yake, mwana wa mama yake hasa, akauliza, “Je, huyu ndiye ndugu yenu wa mwisho, ambaye mlinieleza habari zake?” Ndipo akasema, “Mungu na akufadhili, mwanangu.”
Alipoinua macho yake akamwona Benjamini ndugu yake, mwana wa mamaye, naye akasema, “Je huyu ndiye mdogo wenu mliyemsema?” Na kisha akasema, “Mungu na awe mwenye neema kwako, mwanangu.”
30 Akiwa ameguswa sana kwa kumwona ndugu yake, Yosefu akatoka nje kwa haraka na kutafuta mahali pa kulilia. Akaingia kwenye chumba chake cha pekee na kulilia humo.
Yusufu akaharakisha kutoka chumbani, kwani aliguswa sana kuhusu nduguye. Akatafuta mahali pa kulia. Akaingia chumbani mwake na kulia umo.
31 Baada ya kunawa uso wake, akatoka nje na huku akijizuia akasema, “Pakueni chakula.”
Akaosha uso wake na kutoka nje. Akajizuia mwenyewe, akasema, “karibuni chakula.”
32 Wakampakulia Yosefu peke yake, ndugu zake peke yao na Wamisri waliokula pamoja naye peke yao, kwa sababu Wamisri wasingeweza kula pamoja na Waebrania, kwa maana ilikuwa ni chukizo kwa Wamisri.
Watumishi wakamhudumia Yusufu peke yake na wale ndugu peke yao. Wamisri pale wakala pamoja naye peke yao kwa sababu Wamisri hawakuweza kula mkate na Waebrania, kwani hilo ni chukizo kwa Wamisri.
33 Watu hao walikuwa wameketi mbele yake kwa mfuatano wa umri wao, kuanzia mzaliwa wa kwanza hadi mzaliwa wa mwisho, wakatazamana wao kwa wao kwa mshangao.
Wale ndugu wakakaa mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa kulingana na haki yake ya uzaliwa, na mdogo kulingana na ujana wake. Wale watu wakashangaa wote.
34 Wakati walipelekewa sehemu ya chakula kutoka mezani mwa Yosefu, sehemu ya Benyamini ilikuwa mara tano zaidi ya sehemu ya wale wengine. Kwa hiyo wakanywa na kufurahi pamoja naye.
Yusufu akapeleka sehemu kwao kutoka katika chakula kilichokuwa mbele yake. Lakini sehemu ya Benjamini ilikuwa mara tano zaidi ya kila ndugu zake. Wakanywa na wakamfurahia.