< Mwanzo 42 >

1 Wakati Yakobo alipofahamu kuwa kuna nafaka huko Misri, akawaambia wanawe, “Mbona mnakaa tu hapa mnatazamana?”
Basi Yakobo akafahamu kwamba kuna nafaka huko Misri. Akawambia wanawe, “Kwa nini mnatazamana?
2 Akaendelea kuwaambia, “Nimesikia kuwa huko Misri kuna nafaka. Telemkeni huko mkanunue chakula kwa ajili yetu, ili tuweze kuishi wala tusife.”
Akasema, “Tazama, nimesikia kwamba kuna nafaka huko Misri. Shukeni huko mkatununulie chakula ili tuishi wala tusife.”
3 Ndipo wale ndugu kumi wa Yosefu, wakateremka huko Misri kununua nafaka.
Ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri kununua chakula.
4 Lakini Yakobo hakumtuma Benyamini, ndugu yake Yosefu, pamoja na wengine, kwa sababu aliogopa asije akapatwa na madhara.
Lakini Benjamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumtuma na ndugu zake, kwani alihofu kwamba madhara yaweza kumpata.
5 Hivyo wana wa Israeli walikuwa miongoni mwa wale waliokwenda Misri kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa katika nchi ya Kanaani pia.
Wana wa Israeli wakaja kununua miongoni mwao waliokuja, kwani njaa ilikuwapo katika nchi ya Kanaani.
6 Wakati huo Yosefu alikuwa mtawala wa nchi ya Misri, naye alikuwa ndiye aliwauzia watu wote nafaka. Kwa hiyo wakati ndugu zake Yosefu walipofika, wakamsujudia hadi nyuso zao zikagusa ardhi.
Basi Yusufu alikuwa mtawala juu ya nchi. Ndiye aliyekuwa akiwauzia watu wote wa nchi. Ndugu zake Yusufu wakaja na kumwinamia na nyuso zao hata chini.
7 Mara Yosefu alipowaona ndugu zake, akawatambua, lakini akajifanya mgeni na kuzungumza nao kwa ukali, akiwauliza, “Ninyi mnatoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka katika nchi ya Kanaani kuja kununua chakula.”
Yusufu akawaona ndugu zake na kuwatambua, lakini alijibadili kwao na kuongea nao kwa ukali. Akawambia, “Mmetoka wapi?” Wakasema, “Kutoka nchi ya Kanaani ili kununua chakula.”
8 Ingawa Yosefu aliwatambua ndugu zake, wao hawakumtambua.
Yusufu akawatambua ndugu zake, lakini wao hawakumtambua.
9 Ndipo Yosefu alipokumbuka ndoto zake kuwahusu wao, akawaambia, “Ninyi ni wapelelezi! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”
Yusufu akazikumbuka ndoto aliyoziota kuhusu wao. Akawambia, “Ninyi ni wapelelezi. Mmekuja kuona sehemu za nchi zisizolindwa.”
10 Wakamjibu, “Sivyo bwana wangu. Watumishi wako wamekuja kununua chakula.
Wakamwambia, “Hapana, bwana wangu. Watumishi wako wamekuja kununua chakula.
11 Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.”
Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Ni watu wa kweli. Watumishi wako siyo wapelelezi.”
12 Akawaambia, “La hasha! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”
Akawambia, “Hapana, mmekuja kuangalia sehemu za nchi zisizolindwa.”
13 Lakini wakamjibu, “Watumishi wako walikuwa kumi na wawili, wana wa mtu mmoja ambaye anaishi katika nchi ya Kanaani. Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu na mwingine alikufa.”
Wakasema, “Sisi watumishi wako tupo ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja katika nchi ya Kanaani. Tazama, mdogo yupo na baba yetu, na mwingine hayupo hai tena.”
14 Yosefu akawaambia, “Ni sawa kabisa kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi!
Yusufu akawambia, “Ndivyo nilivyowambia; ninyi ni wapelelezi.
15 Na hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa mpaka ndugu yenu mdogo aje hapa.
Mtajaribiwa kwa njia hii. Kama aishivyo Farao, hamtaondoka hapa, mdogo wenu asipokuja hapa.
16 Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu, wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!”
Mtumeni mmoja wenu amlete mdogo wenu. Mtabaki gerezani, hata maneno yenu yatakapothibitishwa, kwamba kuna ukweli ndani yenu.”
17 Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu.
Akawaweka kifungoni kwa siku tatu.
18 Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu:
Katika siku ya tatu Yusufu akaongea nao, “Fanyeni hivi nanyi mtaishi, kwani ninamcha Mungu.
19 Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa.
Kama ninyi ni watu wa kweli, mmoja wenu atazuiliwa hapa gerezani, lakini ninyi nendeni, chukueni nafaka kwa ajili ya nyumba zenu.
20 Lakini ni lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo.
Mleteni mdogo wenu kwangu ili kwamba maneno yenu yathibitishwe nanyi hamtakufa.” Wakafanya hivyo.
21 Wakaambiana wao kwa wao, “Hakika tunaadhibiwa kwa sababu ya ndugu yetu. Tuliona jinsi alivyohuzunika alipokuwa anatusihi kuponya maisha yake, lakini hatukumsikiliza, hiyo ndiyo sababu dhiki hii imetupata.”
Wakasemezana wao kwa wao, “Kwa kweli tuna hatia juu ya ndugu yetu kwani tuliona tabu ya nafsi yake alipotusihi nasi hatukusikia. Kwa hiyo taabu hii imeturudia.”
22 Reubeni akawajibu, “Sikuwaambieni msitende dhambi dhidi ya kijana? Lakini hamkunisikiliza! Sasa ni lazima tuadhibiwe kwa ajili ya damu yake.”
Rubeni akawajibu, “Je sikuwambia, 'Msitende dhambi juu ya kijana,' lakini hamkusikia? Basi, tazama, damu yake inatakiwa juu yetu.”
23 Hawakujua kuwa Yosefu angewaelewa, kwa sababu alitumia mkalimani.
Lakini hawakuja kwamba Yusufu anawaelewa, kwani kulikuwa na mkalimani kati yao.
24 Yosefu akajitenga nao akaanza kulia, kisha akawarudia na kuzungumza nao tena. Akataka Simeoni akamatwe na kufungwa mbele yao.
Akatoka kwao na kulia. Akarudi kwao na kuongea nao. Akamchukua Simoni miongoni mwao na kumfunga mbele ya macho yao.
25 Yosefu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe mahitaji ya njiani. Baada ya kufanyiwa hayo yote,
Kisha Yusufu akaagiza watumishi kujaza mifuko yao kwa nafaka, na kurudisha pesa ya kila mmoja katika gunia lake, nakuwapa mahitaji kwa safari. Wakatendewa hivyo.
26 wakapakiza nafaka juu ya punda zao, wakaondoka.
Hawa ndugu wakapandisha chakula chao juu ya punda zao na kuondoka pale.
27 Walipofika mahali pa kulala huko njiani mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake, akakuta fedha yake kwenye mdomo wa gunia lake.
Mmoja wao alipofungua gunia lake ili kumlisha punda wao katika sehemu waliyokuwa, akaona pesa yake. Tazama, ilikuwa mdomoni mwa gunia lake.
28 Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.” Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”
Akawambia ndugu zake, “Pesa yangu imerudishwa. Tazama, imo katika gunia langu.”Mioyo yao ikazimia na wakageukiana kila mmoja huku wakitetemeka. Wakasema, “Ni nini hiki alichotutendea Mungu?”
29 Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema,
Wakaenda kwa Yakobo, baba yao katika nchi ya Kanaani na kumwambia yote yaliyowapata.
30 “Huyo mtu ambaye ndiye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi.
Wakasema, “Yule mtu, bwana wa nchi, aliongea nasi kwa ukali na kutudhania kuwa wapelelezi katika nchi.
31 Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi.
Tukamwambia, 'Tu watu wa kweli sisi. Sisi siyo wapelelezi.
32 Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’
Tupo ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayupo hai tena, na mdogo yupo na baba yetu katika nchi ya Kanaani.”
33 “Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu pamoja nami hapa, kisha nendeni mpeleke chakula kwa ajili ya jamaa yenu inayoteseka kwa njaa.
Yule mtu, bwana wa nchi, akatwambia, 'Kwa hili nitajua kwamba ni watu wa kweli ninyi. Mwacheni mmojawapo wa ndugu zenu, chukueni chakula kwa ajili ya njaa katika nyumba zenu, na mwondoke.
34 Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu, ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’”
Mleteni mdogo wenu kwangu. Ndipo nitakapojua kwamba ninyi si wapelelezi, lakini ni watu wa kweli. Kisha nitamwachilia ndugu yenu, na mtafanya biashara katika nchi.”
35 Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka kwenye magunia yao, ndani ya gunia la kila mtu kulikuwa na mfuko wa fedha! Wakati wao na baba yao walipoona mifuko ya fedha, wakaogopa.
Ikawa walipoyafungua magunia yao, na tazama, kila mfuko wa fedha wa mmojawao ulikuwa katika gunia lake. Wakati wao na baba yao walipoona mifuko yao ya fedha, wakaogopa.
36 Yakobo baba yao akawaambia, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yosefu hayupo na Simeoni hayupo tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume nami!”
Yakobo baba yao akawambia, “Mmeniharibia watoto wao. Yusufu hayupo hai tena, Simoni ameondoka, nanyi mmpeleke Benjamini naye. Mambo haya yote ni kunyume changu.”
37 Ndipo Reubeni akamwambia baba yake, “Waweza kuwaua wanangu wote wawili, ikiwa sitamrudisha Benyamini kwako. Mkabidhi Benyamini katika uangalizi wangu, nami nitamrudisha.”
Rubeni akamwambia baba yake, kusema, “Unaweza kuwaua wanangu wawili nisipomrudisha Benjamini kwako. Mweke mikononi mwangu, nami nitamrudisha tena kwako.”
38 Lakini Yakobo akasema, “Mwanangu hatashuka huko pamoja nanyi; ndugu yake amekufa naye ndiye peke yake aliyebaki. Ikiwa atapatwa na madhara katika safari mnayoiendea, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini kwa masikitiko.” (Sheol h7585)
Yakobo akasema, “Mwanangu atashuka pamoja nanyi. Kwani ndugu yake amekufa na yeye peke yake amebaki. Ikiwa madhara yatampata katika njia mnayoiendea, ndipo mtakapozishusha mvi zangu kaburini kwa huzuni.” (Sheol h7585)

< Mwanzo 42 >