< Mwanzo 37 >

1 Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.
Yakobo akaishi katika nchi aliyokaa babaye, katika nchi ya Kanaani.
2 Zifuatazo ni habari za Yakobo. Yosefu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake wa mama wengine, yaani wana wa Bilha na wana wa Zilpa wake za baba yake, naye akawa akimletea baba yake taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.
Haya ndiyo matukio yaliyomhusu Yakobo. Yusufu, aliyekuwa kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akilichunga kundi pamoja na ndugu zake. Alikuwa pamoja na wana wa Bilha na pamoja na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akaleta taarifa yao mbaya kwa baba yao.
3 Basi, Israeli akampenda Yosefu kuliko yeyote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana.
Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote kwa sababu alikuwa mwana wa uzee wake. Akamshonea vazi zuri.
4 Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yosefu kuliko yeyote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.
Ndugu zake wakaona kwamba baba yao alimpenda sana kuliko ndugu zake wote. Wakamchukia na hawakuongea naye vema.
5 Yosefu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi.
Yusufu akaota ndoto, na akawambia ndugu zake. Wakamchukia zaidi.
6 Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota:
Aliwambia, “Tafadhari sikilizeni ndoto hii niliyoiota.
7 Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafula mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ikiuzunguka na kuuinamia.”
Tazama, tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani na tazama, mganda wangu ukainuka na kusimama wima, na tazama, miganda yenu ikasogea na kuuinamia mganda wangu”
8 Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakaongeza kumchukia zaidi kwa sababu ya ndoto yake pamoja na yale aliyowaambia.
Ndugu zake wakamwambia, “Je ni kweli utatutawala? Je utatutawala juu yetu? Hata wakamchukia zaidi kwa ajili ya ndoto zake na maneno yake.
9 Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”
Akaota ndoto nyingine na kuwasimulia ndugu zake. Alisema, “Tazama, nimeota ndoto nyingine: Jua na mwezi na nyota kumi na moja ziliniinamia.”
10 Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako na mimi na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe hadi nchi?”
Akamwambia baba yake vile vile alivyowambia ndugu zake, na baba yake akamkemea. Akamwambia, Je umeota ndoto ya namna gani hii? Je mama yako na mimi na ndugu zako kweli tutakuja kukuinamia mpaka chini?”
11 Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.
Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliwema jambo hilo moyoni.
12 Basi, ndugu zake walikuwa wamekwenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu,
Ndugu zake wakaenda kulichunga kundi la baba yao huko Shekemu.
13 naye Israeli akamwambia Yosefu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.” Yosefu akajibu, “Vema sana, niko tayari.”
Israeli akamwambia Yusufu, 'Je ndugu zako hawalichungi kundi huko Shekemu? Njoo, nami nitakutuma kwao.” Yusufu akamwambia, “nipo tayari.”
14 Kwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama mambo yote ni salama kwa ndugu zako na makundi, kisha uniletee habari.” Ndipo akamtuma Yosefu kutoka Bonde la Hebroni. Yosefu alipofika Shekemu,
Akamwambia, “Basi nenda, uwaone ndugu zako na kundi wanaendeleaje, na uniletee neno.” Hivyo Yakobo akamtuma kutoka katika bonde la Hebroni, na Yusufu akaenda Shekemu.
15 mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani na akamuuliza, “Unatafuta nini?”
Mtu mmoja akamwona Yusufu. Tazama, Yusufu alikuwa akizunguka kondeni. Yule mtu akamwuliza, “Unatafuta nini?”
16 Akajibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?”
Yusufu akamwambia, “Nawatafuta ndugu zangu. Tafadhari, niambie, wananalichunga wapi kundi.”
17 Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nilisikia wakisema, ‘Twende Dothani.’” Kwa hiyo Yosefu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani.
Yule mtu akasema, “Waliondoka mahali hapa, kwa maana niliwasikia wakisema, 'Haya twende Dothani.” Yusufu akawafuata ndugu zake na kuwaona huko Dothani.
18 Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga shauri baya la kumuua.
Wakamwona kutokea mbali, na kabla hajawakaribia, wakapanga njama ya kumwua.
19 Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja!
Ndugu zake wakaambiana wao kwa wao, “Tazama, mwotaji anakaribia.
20 Njooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”
Njoni sasa, na tumwue na kumtupa katika mojawapo ya mashimo haya. Nasi tutasema, 'Mnyama mkali amemrarua.' Nasi tutaona ndoto zake zitakuwaje.”
21 Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao akasema, “Tusiutoe uhai wake.
Rubeni alilisikia hilo na kumwokoa kutoka katika mikono yao. Alisema, “Tusiuondoe uhai wake.”
22 Tusimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani kwa baba yake.
Rubeni aliwambia, “Msimwage damu. Mtupeni katika shimo hili lililopo nyikani, lakini msiweke mikono yenu juu yake” - ili kwamba aweze kumwokoa katika mikono yao na kumrudisha kwa baba yake.
23 Kwa hiyo Yosefu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililorembwa vizuri alilokuwa amevaa.
Ikawa Yusufu alipowafikia ndugu zake, walimvua vazi lake zuri.
24 Kisha wakamchukua wakamtupa katika shimo. Wakati huo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji ndani yake.
Wakamchukua na kumtupa shimoni. Shimo lilikuwa tupu bila maji.
25 Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.
Wakakaa chini kula mkate. Walipoinua macho yao na kuangalia, na, tazama, msafara wa Waishmaeli ulikuwa ukija kutoka Gileadi, pamoja na ngamia wao waliochukua viungo, malhamu na manemane. Walikuwa wakisafiri kuvichukua kuelekea Misri.
26 Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini ikiwa tutamuua ndugu yetu na kuificha damu yake?
Yuda akawambia ndugu zake, “Ni faida gani kama tutamwua ndugu yetu na kufunika damu yake?
27 Njooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, nyama yetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.
Haya, na tumwuze kwa Waishmaeli na wala tusiweke mikono yetu juu yake. Kwani yeye ni ndugu yetu, nyama yetu.” Ndugu zake wakamsikiliza.
28 Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yosefu kutoka kwenye lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri.
Wafanyabiashara wa Kimidiani wakapita. Ndugu zake wakamwinua na kumtoa Yusufu shimoni. Wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande ishirini vya fedha. Waishmaeli wakamchukua Yusufu mpaka Misri.
29 Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yosefu hayupo, alirarua nguo zake.
Rubeni akarudi kwenye shimo, na, tazama, Yusufu hakuwemo shimoni. Akararua mavazi yake.
30 Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”
Akarudi kwa ndugu zake na kusema, “Kijana yuko wapi? Na mimi, je niende wapi?”
31 Kisha wakalichukua lile joho la Yosefu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu.
Wakachinja mbuzi na kisha wakalichukua vazi la Yusufu na kulichovya katika damu.
32 Wakalichukua lile joho lililorembwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”
Kisha wakalipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeiona hii. Tafadhari angalia kwamba ni vazi la mwanao au hapana.”
33 Baba yao akalitambua akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yosefu ameraruliwa vipande vipande.”
“Yakobo akaitambua na kusema, “Ni nguo ya mwanangu. Mnyama wa mwitu amemrarua. Bila shaka Yusufu ameraruliwa katika vipande.
34 Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa nguo ya gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi.
Yakobo akararua mavazi yake na kuvaa mavazi ya magunia katika viuno vyake. Akaomboleza kwa ajili ya mwanawe siku nyingi.
35 Wanawe wote na binti zake wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu mpaka nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia. (Sheol h7585)
Wanawe na binti zake wote wakainuka na kumfariji, lakini alikataa kufarijiwa. Akasema, “Hakika nitashuka kuzimu nikimwombolezea mwanangu.” Babaye akamlilia. (Sheol h7585)
36 Wakati ule ule, Wamidiani wakamuuza Yosefu huko Misri kwa Potifa, mmojawapo wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa ulinzi.
Wamidiani wakamwuza huko Misri kwa Potifa, afisa wa Farao, kepteni wa walinzi.

< Mwanzo 37 >