< Mwanzo 35 >
1 Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko na ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.”
2 Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni ile iliyoko katikati yenu, jitakaseni na mkabadilishe nguo zenu.
3 Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipokwenda.”
4 Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo, pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao. Yakobo akavizika chini ya mti wa mwaloni huko Shekemu.
5 Kisha wakaondoka, na hofu ya Mungu ikawapata miji yote iliyowazunguka. Kwa hiyo hakuna aliyewafuatia wana wa Yakobo.
6 Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani.
7 Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli, kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alipojifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake.
8 Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mti wa mwaloni ulioko chini ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi.
9 Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki.
10 Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa tena Yakobo, jina lako utakuwa Israeli.” Kwa hiyo akamwita Israeli.
11 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi, ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako.
12 Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaki nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.”
13 Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye.
14 Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake.
15 Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli.
16 Kisha wakaondoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efrathi, Raheli akaanza kusikia uchungu na alipata shida kuu.
17 Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.”
18 Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe Benoni. Lakini babaye akamwita Benyamini.
19 Kwa hiyo Raheli akafa, akazikwa kando ya njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu).
20 Juu ya kaburi lake, Yakobo akasimamisha nguzo, ambayo mpaka leo inatambulisha kaburi la Raheli.
21 Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema mbele mnara wa Ederi.
22 Wakati Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aitwaye Bilha, naye Israeli akasikia jambo hili. Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili:
23 Wana wa Lea walikuwa: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni.
24 Wana wa Raheli walikuwa: Yosefu na Benyamini.
25 Wana waliozaliwa na Bilha mtumishi wa kike wa Raheli walikuwa: Dani na Naftali.
26 Wana waliozaliwa na Zilpa mtumishi wa kike wa Lea walikuwa: Gadi na Asheri. Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu.
27 Yakobo akarudi nyumbani kwa baba yake Isaki huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Abrahamu na Isaki.
28 Isaki aliishi miaka 180.
29 Kisha Isaki akapumua pumzi yake ya mwisho akafa, akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee wa miaka mingi. Nao wanawe Esau na Yakobo wakamzika.