< Mwanzo 34 >
1 Basi Dina, binti wa Yakobo aliyezaliwa na Lea, akatoka nje kuwatembelea wanawake wa nchi ile.
Basi Dina, Binti wa Lea aliyemzalia Yakobo, akaenda kuwaona wasichana wa nchi.
2 Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile alipomwona, akamchukua na kumnajisi.
Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mwana mfalme wa nchi, akamwona na akamkamata kwa nguvu na kulala naye.
3 Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza.
Akavutiwa na Dina, binti Yakobo. Akampenda msichana na kuongea naye kwa upole.
4 Shekemu akamwambia baba yake Hamori, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.”
Shekemu akamwambia Hamori baba yeke, kusema, “Nipe msichana huyu kuwa mke wangu.”
5 Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake, kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo mpaka waliporudi nyumbani.
Basi Yakobo akasikia kwamba alikuwa amemchafua Dina binti yake. Wanawe walikuwa pamoja na wanyama uwandani, hivyo Yakaobo akawangoja hata walipokuja.
6 Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo.
Hamori baba wa Shekemu akaenda kuongea na Yakobo.
7 Basi wana wa Yakobo walikuwa wamerudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotokea. Walikuwa wamejawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti wa Yakobo, kitu ambacho hakingepasa kufanyika.
Wana wa Yakobo waliposikia neno hili wakaja kutoka uwandani. Watu hawa walichukizwa sana. Walikasirika sana kwa sababu alikuwa amemwaibisha Israeli kwa kumlazimisha binti wa Yakobo, kwa maana jambo kama hilo halikupasa kutendeka.
8 Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake.
Hamori akaongea nao, akisema, “Shekemu mwanangu anampenda binti yenu. Tafadhari mpeni kuwa mke wake.
9 Oaneni na sisi, tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu.
Mwoane nasi, tupeni binti zenu, na mjichukulie binti zetu kwa ajili yenu wenyewe.
10 Mwaweza kuishi katikati yetu, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, fanyeni biashara humu na mjipatie mali.”
Mtaishi nasi, na nchi itakuwa wazi kwa ajili yenu kufanya biashara humo, na kupata mali.”
11 Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Na nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema.
Shekemu akamwambia baba yake na ndugu zake, “Na nione kibari machoni penu, na chochote mtakachoniambia nitatoa.
12 Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.”
Niambieni kiasi kikubwa chochote cha mahari na zawadi kama mtakavyo, nami nitatoa chochote msemacho, lakini mnipe msichana kuwa mke wangu.”
13 Kwa sababu ndugu yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na baba yake Hamori.
Wana wa Yakobo wakamjibu Shekemu na Hamori baba yake kwa hila, kwa sababu Shekemu alikuwa amemnajisi Dina dada yao.
14 Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili, hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hakutahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu.
Wakawambia, “Hatuwezi kufanya jambo hili, kumpa dada yetu mtu yeyote ambaye hajatailiwa; kwani hiyo ni aibu kwetu.
15 Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote.
Kwa sharti hili peke yake tutakubaliana nanyi: iwapo mtatailiwa kama sisi, ikiwa kila mtu mme miongoni mwenu atatailiwa.
16 Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi.
Ndipo tutakapowapa binti zetu, nasi tutachukua binti zenu kwetu sisi wenyewe, na tutaishi nanyi na kuwa wamoja.
17 Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua ndugu yetu na kuondoka.”
Lakini kama hamtusikilizi na kutailiwa, ndipo tutakapomchukua dada yetu na kuondoka.
18 Pendekezo lao likawa jema kwa Hamori na Shekemu mwanawe.
Maneno yao yakawafurahisha Hamori na Shekemu mwanaye.
19 Kijana mdogo, ambaye alikuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo.
Kijana hakukawia kufanya walichokisema, kwa maana alipendezwa na binti Yakobo, na kwa sababu alikuwa mtu aliyeheshimiwa sana katika nyumba ya babaye.
20 Kwa hiyo Hamori na Shekemu mwanawe walikwenda kwenye lango la mji kuzungumza na wenzao wa mjini.
Hamori na Shekemu mwanaye wakaenda katika lango la mji wao na kuongea na watu wa mji, kusema,
21 Wakasema, “Hawa watu ni marafiki kwetu, tuwaruhusu waishi katika nchi yetu na kufanya biashara ndani yake, nchi ina nafasi tele kwa ajili yao. Tunaweza kuoa binti zao. Nao wanaweza kuoa binti zetu.
“Watu hawa wanaamani nasi, hivyo na waishi katika nchi na kufanya biashara humo kwa maana, kweli, nchi ni kubwa ya kuwatosha. Haya na tuwachukue binti zao kuwa wake, nasi tuwape binti zetu.
22 Lakini watu hao watakuwa tayari kukubali kuishi nasi kama watu wamoja nao kwa sharti kwamba wanaume wetu watahiriwe, kama wao.
Kwa shariti hili pekee watu hawa wanakubali kuishi nasi na kuwa wamoja: ikiwa kila mwanamme miongoni mwetu atatailiwa, kama wao.
23 Je, si mifugo yao, mali zao na wanyama wao wengine wote watakuwa wetu? Basi na tuwape kibali, nao wataishi miongoni mwetu.”
Je wanyama wao na vitu vyao - wanyama wao wote kuwa wetu? Haya na tukubaliane nao, nao wataishi kati yetu.”
24 Wanaume wote waliotoka nje ya lango la mji walikubaliana na Hamori na Shekemu mwanawe na kila mwanaume katika mji ule akatahiriwa.
Watu wote wa mji wakamsikiliza Hamori na Shekemu, mwanaye. Kila mwanamme akatailiwa.
25 Baada ya siku tatu, wakati wote wakiwa wangali katika maumivu, wana wawili wa Yakobo, yaani Simeoni na Lawi, ndugu zake Dina, wakachukua panga zao na kuvamia mji ambao haukutazamia vita, wakaua kila mwanaume.
Katika siku ya tatu, walipokuwa katika maumivu bado, wawili wa wana wa Yakobo (Simoni na Lawi, kaka zake Dina), wakachukua kila mmoja upanga wake na kuushambulia mji ambao ulikuwa na uhakika wa ulinzi wake, nao wakauwa wanamme wote.
26 Wakawaua Hamori na Shekemu mwanawe kwa upanga kisha wakamchukua Dina kutoka nyumba ya Shekemu na kuondoka.
Wakamwua Hamori na Shekemu kwa makali ya upanga. Wakamchukua Dina kutoka nyumba ya Shekemu na kuondoka.
27 Wana wa Yakobo walipita juu ya maiti katika kuteka nyara mji ule ambamo dada yao alikuwa amenajisiwa.
Wale wana wengine wa Yakobo wakaja kwa maiti na kuuteka nyara mji, kwa sababu watu wale walikuwa wamemnajisi dada yao.
28 Wakachukua kondoo na mbuzi, ngʼombe, punda na kila kitu kilichokuwa chao ndani ya mji ule na mashambani.
Wakachukua makundi yao ya kondoo, mbuzi, punda, na kila kitu ndani ya mji na viunga vyake
29 Walichukua utajiri wao wote pamoja na wanawake na watoto wao, wakachukua nyara kila kitu ndani ya nyumba zao.
utajiri wote. Watoto na wake zao wote, wakawachukua. Hata wakachukua kila kitu kilichokua katika nyumba.
30 Kisha Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, “Mmeleta taabu kwangu kwa kunifanya ninuke kama uvundo kwa Wakanaani na Waperizi, watu waishio katika nchi hii. Sisi ni wachache, kama wakiunganisha nguvu zao dhidi yangu na kunishambulia, mimi na nyumba yangu tutaangamizwa.”
Yakobo akawambia Simoni na Lawi, “Mmeleta shida juu yangu, kunifanya ninuke kwa wenyeji wa nchi, Wakanaani na Waperizi. Mimi nina watu wachache. Ikiwa watajikusanya pamoja kinyume changu na kunishambulia.”
31 Lakini wakamjibu, “Je, ilikuwa vyema kumtendea dada yetu kama kahaba?”
Lakini Simoni na Lawi wakasema, “Je Shekemu alipaswa kumtendea dada yetu kama kahaba?”