< Mwanzo 33 >

1 Yakobo akainua macho akamwona Esau akija na watu wake 400, kwa hiyo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli na wale watumishi wake wawili wa kike.
Yakobo akainua macho yake na, tazama, Esau alikuwa anakuja, na alikuwa na watu mia nne pamoja naye. Yakobo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli, na wale wajakazi wawili.
2 Akawaweka wale watumishi wa kike na watoto wao mbele, Lea na watoto wake wakafuata, Raheli na Yosefu wakaja nyuma.
Kisha akawaweka wajakazi na wanao mbele, wakifuatiwa na Lea na watoto wake, Raheli na Yusufu wakafuata mwisho wa wote.
3 Yeye mwenyewe akatangulia mbele na kusujudu mara saba alipomkaribia ndugu yake.
Yeye mwenyewe akatangulia mbele yao. Akasujudu mara saba kuelekea ardhi, hata alipomkaribia ndugu yake.
4 Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia.
Esau akakimbia kumlaki, akamkumbatia, akakumbatia shingo yake na kumbusu. Kisha wakalia.
5 Esau akainua macho akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa uliofuatana nao ni nani?” Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.”
Esau alipoinua macho, aliona wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa watu pamoja nawe ni kinanani?” Yakobo akasema, Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.”
6 Kisha wale watumishi wa kike na watoto wao wakakaribia na kusujudu.
Kisha wajakazi wakakaribia pamoja na watoto wao, nao wakasujudia.
7 Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yosefu na Raheli, nao pia wakasujudu.
Akafuata Lea pia na watoto wake wakaja na kusujudia. Mwisho Yusufu na Raheli wakaja na kusujudia.
8 Esau akauliza, “Una maana gani kuhusu makundi hayo yote niliyokutana nayo?” Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.”
Esau akasema, Unamaanisha nini kwa makundi haya yote niliyokutana nayo?” Yakobo akasema, “Kutafuta kibali mbele za bwana wangu.
9 Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.”
Esau akasema, “Ninayo ya kutosha, ndugu yangu. Tunza uliyonayo kwa ajili yako mwenyewe.”
10 Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako, ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa takabali kubwa.
Yakobo akasema, “Hapana, tafadhari, ikiwa nimeona kibali mbele zako, basi upokee zawadi yangu kutoka mkononi mwangu, na ni kama kuona uso wa Mungu, na umenipokea.
11 Tafadhali ukubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.
Tafadhari pokea zawadi yangu uliyoletewa, kwa sababu Mungu amenitendea kwa neema, na kwa sababu ninavyo vya kutosha.” Hivyo Yakobo akamsihi, na Esau akamkubali.
12 Ndipo Esau akasema, “Na tuendelee na safari, nitakuwa pamoja nawe.”
Kisha Esau akasema, “Haya na tuondoke. Nitakutangulia.”
13 Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu unajua kwamba watoto ni wachanga na kwamba ni lazima nitunze hawa kondoo wake na ngʼombe wanaonyonyesha. Wakipelekwa kwa haraka hata kama ni kwa siku moja tu, wanyama wote watakufa.
Yakobo akamwambia, “Bwana wangu anajua kwamba watoto ni wadogo, na kwamba kondoo na ng'ombe wananyonyesha ndama wao. Ikiwa watapelekwa kwa haraka hata siku moja, wanyama wote watakufa.
14 Hivyo bwana wangu umtangulie mtumishi wako, wakati mimi nikija polepole kwa mwendo wa makundi yaliyo mbele yangu na mwendo wa watoto, mpaka nifike kwa bwana wangu huko Seiri.”
Tafadhari bwana wangu na amtangulie mtumishi wake. Nitasafiri polopole, kwa kadili ya mifugo iliyo mbele yangu, na kadili ya watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri.”
15 Esau akamwambia, “Basi na niwaache baadhi ya watu wangu pamoja nawe.” Yakobo akauliza, “Lakini kwa nini ufanye hivyo, niache tu nipate kibali machoni pa bwana wangu.”
Esau akasema, haya nikuachie baadhi ya watu wangu waliopamoja nami.” Yakobo akasema, “Kwa nini kufanya hivyo? Bwana wangu amekuwa mkalimu kwangu kiasi cha kutosha.”
16 Hivyo siku hiyo Esau akashika njia akarudi Seiri.
Hivyo Esau akaanza kurudi Seiri.
17 Pamoja na hayo, Yakobo akaenda Sukothi, mahali alipojijengea makazi kwa ajili yake na mabanda kwa ajili ya mifugo yake. Hii ndiyo sababu sehemu ile inaitwa Sukothi.
Yakobo akasafiri kuelekea Sukothi, akajijengea nyumba, na akafanya mazizi kwa ajili ya mifugo wake. Hivyo jina la eneo linaitwa Sukothi.
18 Baada ya Yakobo kutoka Padan-Aramu, alifika salama katika mji wa Shekemu huko Kanaani na kuweka kambi yake karibu na mji.
Yakobo alipokuja kutoka Padani Aramu, akafika salama katika mji wa Shekemu, uliyo katika nchi ya Kanaani. Akapiga kambi karibu na mji.
19 Akanunua kiwanja kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa bei ya vipande mia vya fedha, ambapo alipiga hema lake.
Kisha akanunu sehemu ya ardhi alipokuwa ameweka hema yake kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa vipande mia vya fedha.
20 Pale akajenga madhabahu na kupaita El-Elohe-Israeli.
Akajenga madhabahu pale na kuiita El Elohe Israeli.

< Mwanzo 33 >