< Mwanzo 31 >
1 Yakobo akawasikia wana wa Labani wakisema, “Yakobo amechukua kila kitu kilichokuwa cha baba yetu naye amepata utajiri huu wote kutokana na vile vilivyokuwa mali ya baba yetu.”
Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, “Yakobo amechukuwa yote yaliyokuwa ya baba yetu, na ni kutoka katika mali ya baba yetu amepata utajiri wake.”
2 Yakobo akatambua kwamba moyo wa Labani kwake haukuwa kama ulivyokuwa mwanzo.
Yakobo akaona mwonekano katika uso wa Labani. Akaona kwamba nia yake imebadilika.
3 Ndipo Bwana akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na kwa watu wako, nami nitakuwa pamoja nawe.”
Kisha Yahwe akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na ya ndugu zako, nami nitakuwa nawe.”
4 Hivyo Yakobo akatuma ujumbe kwa Raheli na Lea waje machungani yalikokuwa makundi yake.
Yakobo akatuma kuwaita Raheli na Lea uwandani katika kundi lake la kondoo
5 Akawaambia, “Naona moyo wa baba yenu kwangu sivyo kama ulivyokuwa mwanzoni, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.
naye akawambia, “Naona nia ya baba yenu kwangu imebadilika, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa nami.
6 Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote,
Nanyi mnajua kwamba ni kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu.
7 hata hivyo baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru.
Baba yenu amenidanganya na amebadilisha ujira wangu mara kumi, lakini Mungu hakumruhusu kunidhuru.
8 Kama alisema, ‘Wenye madoadoa watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye madoadoa, kama alisema, ‘Wenye mistari watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye mistari.
Ikiwa alisema, 'Wanyama wenye mabaka watakuwa ujira wako,' ndipo kondoo wote walipozaa watoto wenye mabaka. Na aliposema, wenye milia watakuwa ujira wako,' ndipo kundi lote lilipozaa watoto wenye milia.
9 Hivyo Mungu amechukua mifugo ya baba yenu na amenipa mimi.
Kwa njia hii Mungu amemnyang'anya mifugo baba yenu na kunipa mimi.
10 “Wakati fulani majira ya kuzaliana niliota ndoto ambayo niliinua macho na kuona kwamba wale mabeberu waliokuwa wakipanda kundi walikuwa wa mistari, madoadoa na mabakabaka.
Wakati fulani wa majira ya kupandana, niliona katika ndoto mabeberu yaliyowapanda kundi. Mabeberu yalikuwa ya milia, mabaka na madoa.
11 Malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’
Malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, 'Yakobo.' Nikasema, 'Mimi hapa.'
12 Akasema, ‘Inua macho yako uone wale mabeberu wote wanaopanda kundi wana mistari, madoadoa au mabakabaka, kwa maana nimeona yale yote ambayo Labani amekuwa akikutendea.
Akasema, 'Inua macho yako uone mabeberu wanaolipanda kundi. Wana milia, madoa na na mabaka, kwani nimeona kila jambo Labani analokutendea.
13 Mimi ndiye Mungu wa Betheli, ulikomiminia ile nguzo mafuta na pale mahali uliponiwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii mara moja urudi katika nchi uliyozaliwa.’”
Mimi ni Mungu wa Betheli, mahali ulipoitia nguzo mafuta, mahali uliponitolea nadhiri. Basi sasa inuka na uondoke katika nchi hii na kurudi katika nchi uliyozaliwa.
14 Ndipo Raheli na Lea wakajibu, “Je bado tu tunalo fungu lolote katika urithi wa nyumba ya baba yetu?
Raheli na Lea wakajibu na kumwambia, “Je kuna sehemu yoyote au urithi wetu katika nyumba ya baba yetu?
15 Je, yeye hatuhesabu sisi kama wageni? Sio kwamba ametuuza tu, bali ametumia hata na vile vilivyolipwa kwa ajili yetu.
Je hatutendei kama wageni? Kwa maana ametuuza na kwa ujumla ametapanya pesa zetu.
16 Hakika utajiri wote ambao Mungu ameuchukua kutoka kwa baba yetu ni mali yetu na watoto wetu. Hivyo fanya lolote lile Mungu alilokuambia.”
Mali zote ambazo sasa Mungu amemnyang'anya baba yetu ni zetu na watoto wetu. Sasa basi, lolote Mungu alilokuambia, fanya.
17 Ndipo Yakobo akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia,
Kisha Yakobo akainuka na kuwapandisha wanawe na wakeze kwenye ngamia.
18 naye akawaswaga wanyama wote mbele yake pamoja na vitu vyote alivyokuwa amechuma huko Padan-Aramu kwenda kwa baba yake Isaki katika nchi ya Kanaani.
Akawaongoza mifugo wake wote mbele yake, pamoja na mali zake zote, wakiwemo wanyama aliowapata huko Padani Aramu. Kisha akaenda kuelekea kwa Isaka baba yake katika nchi ya Kanaani.
19 Labani alipokuwa amekwenda kukata kondoo wake manyoya, Raheli aliiba miungu ya nyumba ya baba yake.
Labani alipokuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo wake, Raheli akaiba miungu ya nyumba ya baba yake.
20 Zaidi ya hayo, Yakobo alimdanganya Labani Mwaramu kwa kutokumwambia kwamba anakimbia.
Yakobo pia akamdanganya Labani Mwarami, kwa kutomtaarifu kwamba anaondoka.
21 Hivyo akakimbia pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo na kuvuka Mto Frati akaelekea nchi ya vilima katika Gileadi.
Hivyo akaondoka na vyote alivyokuwa navyo na kwa haraka akavuka mto, na akaenda kuelekea nchi ya vilima ya Gileadi.
22 Siku ya tatu Labani akaambiwa kwamba Yakobo amekimbia.
Siku ya tatu Labani akaambiwa kwamba Yakobo amekimbia.
23 Akiwachukua jamaa zake, akamfuatia Yakobo kwa siku saba na kumkuta kwenye nchi ya vilima katika Gileadi.
Hivyo akawachukua ndugu zake pamoja naye na kumfuatia kwa safari ya siku saba. Akampata katika nchi ya vilima ya Gileadi.
24 Ndipo Mungu akamjia Labani Mwaramu katika ndoto usiku na kumwambia, “Jihadhari usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.”
Basi Mungu akaja kwa Labani Mwarami katika ndoto usiku na kumwambia, “Ujiadhari kumwambia Yakobo jambo lolote liwe jema au baya.”
25 Yakobo alikuwa amepiga hema lake katika nchi ya vilima katika Gileadi wakati Labani alipomkuta, Labani na jamaa yake wakapiga kambi huko pia.
Labani akampata Yakobo. Basi Yakobo alikuwa amepiga hema yake katika nchi ya vilima. Labani pia akapiga kambi pamoja na ndugu zake katika nchi ya kilima ya Gileadi.
26 Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Umenidanganya na umewachukua binti zangu kama mateka katika vita.
Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini, kwamba umewachukua binti zangu kama mateka wa vita?
27 Kwa nini ulikimbia kwa siri na kunidanganya? Kwa nini hukuniambia ili nikuage kwa furaha na nyimbo za matari na vinubi?
Kwa nini umekimbia kwa siri na kunihadaa kwa kutokuniambia? Ningekuruhusu uondoke kwa sherehe na kwa nyimbo, kwa matari na vinubi.
28 Hata hukuniruhusu niwabusu wajukuu zangu na kuwaaga binti zangu. Umefanya kitu cha kipumbavu.
Haukuniacha niwabusu wajukuu wangu na binti zangu kwa kuwaaga. Basi umefanya upumbavu.
29 Nina uwezo wa kukudhuru, lakini usiku uliopita Mungu wa baba yako alisema nami, akaniambia, ‘Jihadhari, usiseme neno lolote kwa Yakobo liwe zuri au baya.’
Iko katika uwezo wangu kukudhuru, lakini Mungu wa baba yako alisema nami usiku wa leo na kuniambia, 'Jiadhari usimwambie Yakobo neno la heri wala shari.'
30 Sasa umeondoka kwa sababu umetamani kurudi nyumbani kwa baba yako. Lakini kwa nini umeiba miungu yangu?”
Na sasa, umeondoka kwa sababu umeitamani sana nyumba ya baba yako. Lakini kwa nini umeiba miungu yangu?
31 Yakobo akamjibu Labani, “Niliogopa, kwa sababu nilifikiri ungeweza kuninyangʼanya binti zako kwa nguvu.
Yakobo akajibu na kumwambia Labani, “Ni kwa sababu niliogopa na kudhani kuwa ungeninyang'anya binti zako kwa nguvu ndiyo maana nikaondoka kwa siri.
32 Lakini kama ukimkuta yeyote aliye na miungu yako, hataishi. Mbele ya jamaa yetu, angalia mwenyewe uone kama kuna chochote chako hapa nilicho nacho, kama kipo, kichukue.” Basi Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiba hiyo miungu.
Yeyote aliyeiiba miungu yako hataendelea kuishi. Mbele ya ndugu zetu, onesha chochote kilichochako nilichonacho na uchukue.” Kwa maana Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameviiba.
33 Kwa hiyo Labani akaingia ndani ya hema la Yakobo na ndani ya hema la Lea na ndani ya hema la watumishi wawili wa kike, lakini hakukuta chochote. Baadaye alipotoka katika hema la Lea, akaingia hema la Raheli.
Labani akaingia katika hema ya Yakobo, katika hema ya Lea, na katika hema za wale wajakazi wawili, lakini hakuviona. Akatoka katika hema ya Lea na kuingia katika hema ya Raheli.
34 Basi Raheli ndiye alikuwa amechukua ile miungu ya nyumbani kwao na kuiweka katika matandiko ya ngamia na kukalia. Labani akatafuta kila mahali kwenye hema lakini hakupata chochote.
Basi Raheli alikuwa ameichukua miungu ya nyumbani, na kuiweka katika ngozi ya ngamia, na kukaa juu yake. Labani akatafuta katika hema yote, lakini hakuiona.
35 Raheli akamwambia baba yake, “Usikasirike, bwana wangu kwa kuwa siwezi kusimama ukiwepo, niko katika hedhi.” Labani akatafuta lakini hakuweza kuipata miungu ya nyumbani kwake.
Akamwambia baba yake, “Usikasirike, bwana wangu, kwamba siwezi kusimama mbele yako, kwani nipo katika kipindi changu.” Hivyo akatafuta lakini hakuiona miungu ya nyumbani mwake.
36 Yakobo akakasirika na kumshutumu Labani, akisema, “Uhalifu wangu ni nini?” Akamuuliza Labani, “Ni dhambi gani niliyofanya hata unaniwinda?
Yakobo akakasirika na kuojiana na Labani. Akamwambia, “Kosa langu ni nini? Dhambi yangu ni ipi, hata ukanifuatia kwa ukali?
37 Sasa kwa kuwa umepekua vitu vyangu vyote umepata nini kilicho cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya jamaa yako na yangu, nao waamue kati yetu sisi wawili.
Kwa maana umechunguza mali zangu zote. Umeona nini kati ya kitu chochote cha nyumbani mwako? Viweke hapa mbele ya ndugu zetu, ili waamue kati yetu wawili.
38 “Mpaka sasa nimekuwa pamoja nawe miaka ishirini. Kondoo wako na mbuzi wako hawajaharibu mimba, wala sijala kondoo dume kutoka makundi yako.
Kwa miaka ishirini nimekuwa nawe. Kondoo wako na mbuzi wako hawakutoa mimba, wala sikula dume lolote la kondoo katika wanyama wako.
39 Sikukuletea mfugo aliyeraruliwa na wanyama pori, nilibeba hasara mimi mwenyewe. Tena ulinidai malipo kwa chochote kilichoibwa mchana au usiku.
Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea. Badala yake, nilichukua upotevu huo, kwamba wameibwa mchana au usiku.
40 Hii ndiyo iliyokuwa hali yangu: Niliumia kwa joto la mchana na baridi usiku, pia usingizi ulinipa.
Nilikuwepo wakati wote; mchana joto lilinipata, na baridi wakati wa usiku; na sikupata usingizi.
41 Ilikuwa hivi kwa miaka ile ishirini niliyokuwa nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka ile kumi na minne kwa ajili ya binti zako wawili, miaka sita kwa ajili ya makundi yako, nawe ulibadilisha ujira wangu mara kumi.
Miaka hii ishirini nimekuwa katika nyumba yako. Nilikufanyia kazi miaka kumi na nne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita kwa ajili ya wanyama wako. Umebadili ujira wangu mara kumi.
42 Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Abrahamu na Hofu ya Isaki, hakuwa pamoja nami, hakika ungenifukuza mikono mitupu. Lakini Mungu ameona taabu yangu na kazi ngumu ya mikono yangu, naye usiku uliopita amekukemea.”
Isipokuwa Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu, yule Isaka anayemwofu, amekuwa nami, bila shaka sasa ungenipeleka mikono mitupu. Mungu ameliona teso langu na jinsi nilivyofanya kazi kwa bidii, na hivyo akakukemea usiku wa leo.
43 Labani akamjibu Yakobo, “Wanawake hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu na makundi haya ni makundi yangu. Vyote unavyoviona ni vyangu. Lakini hata hivyo ninaweza kufanya nini kuhusu hawa binti zangu, au kuhusu watoto waliowazaa?
Labani akajibu na kumwambia Yakobo, “Mabinti hawa ni mabinti zangu, wajukuu ni wajukuu wangu, na wanyama ni wanyama wangu. Yote uyaonayo ni yangu. Lakini nitafanya nini leo kwa hawa binti zangu, au kwa watoto wao waliowazaa?
44 Njoo sasa na tufanye agano, wewe na mimi, na liwe kama shahidi kati yetu.”
Hivyo sasa, na tufanye agano, wewe nami, na liwe shahidi kati yangu nawe.”
45 Hivyo Yakobo akachukua jiwe, akalisimamisha kama nguzo.
Hivyo Yakobo akachukua jiwe na kuliweka kama nguzo.
46 Akawaambia jamaa yake, “Kusanyeni mawe.” Hivyo wakachukua mawe na kuyakusanya yakawa lundo, wakala chakula hapo karibu na hilo lundo.
Yakobo akawambia ndugu zake, “Kusanyeni mawe.” Hivyo wakachukua mawe na kufanya rundo. Kisha wakala pale kati ya lile rundo.
47 Labani akaliita Yegar-Sahadutha na Yakobo akaliita Galeedi.
Labani aliliita Yega Saha Dutha, lakini Yakobo akaiita Galeedi
48 Labani akasema, “Lundo hili ni shahidi kati yako na mimi leo.” Ndiyo maana likaitwa Galeedi.
Labani akasema, “Rundo hili ni shahidi kati yangu nawe leo.” Kwa hiyo jina lake likaitwa Galedi.
49 Pia liliitwa Mispa, kwa sababu alisema, “Bwana na aweke ulinzi kati yako na mimi wakati kila mmoja akiwa mbali na mwingine.
Inaitwa pia Mispa, kwa sababu Labani alisema, “Yahwe na atuangalie mimi nawe, tunapokuwa hatuonani.
50 Kama ukiwatenda mabaya binti zangu au ukioa wake wengine zaidi ya binti zangu, hata ingawa hakuna hata mmoja aliye pamoja nasi, kumbuka kwamba Mungu ni shahidi kati yako na mimi.”
Ikiwa utawatesa binti zangu, au ikiwa utachukua wanawake wengine mbali na binti zangu, japokuwa hakuna mwingine yupo nasi, tazama, Mungu ni shahidi kati yangu nawe.”
51 Pia Labani akamwambia Yakobo, “Hili ndilo lundo, na hii ndiyo nguzo niliyoisimamisha kati yako na mimi.
Labani akamwambia Yakobo, Tazama rundo hili, na tazama nguzo, nililoliweka kati yako nami.
52 Lundo hili ni shahidi na nguzo hii ni shahidi, kwamba sitavuka lundo hili kuja upande wako kukudhuru, nawe kwamba hutavuka lundo hili na nguzo hii kuja upande wangu kunidhuru.
Rundo hili ni shahidi, na nguzo ni shahidi, kwamba sitapita rundo hili kuja kwako, na kwamba wewe hautapita rundo hili kuja kwangu, kwa madhara.
53 Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba zao, aamue kati yetu.” Hivyo Yakobo akaapa kwa jina la Hofu ya baba yake Isaki.
Mungu wa Ibrahimu, na mungu wa Nahori, miungu ya baba zao, waamue kati yetu.”Yakobo akaapa kwa Hofu ya Isaka baba yake.
54 Yakobo akatoa dhabihu juu ya kilima na akawaalika jamaa zake kula chakula. Baada ya kula, wakalala huko.
Yakobo akatoa sadaka juu ya mlima na akawaita ndugu zake kula chakula. Walikula na kukaa usiku kucha juu ya mlima.
55 Kesho yake asubuhi na mapema, Labani akawabusu wajukuu zake, binti zake na kuwabariki. Kisha akaondoka, akarudi nyumbani.
Labani akaamka asubuhi na mapema, akawabusu wajuu zake na binti zake na kuwabariki. Kisha Labani akaondoka na kurudi kwake.