< Mwanzo 30 >

1 Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”
Raheli alipoona kwamba hamzalii Yakobo watoto, Raheli akamwonea wivu dada yake. Akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, sivyo nitakufa.”
2 Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?”
Hasira ya Yakobo ikawaka juu ya Raheli. Akasema, “Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia usipate watoto?
3 Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mtumishi wangu wa kike. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto na kwa kupitia yeye mimi pia niweze kuwa na uzao.”
Akasema, “Tazama, kuna mjakazi wangu Bilha. Lala naye, hivyo aweze kuzaa watoto magotini pangu, nami nitapata watoto kwake.
4 Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili,
Hivyo akampa Bilha mjakazi kama mke wake, na Yakobo akalala naye.
5 Bilha akapata mimba, naye akamzalia Yakobo mwana.
Bilha akashika mimba na kumzalia Yakobo mwana.
6 Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu, amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita Dani.
Kisha Raheli akasema, “Mungu ameamua kwa faida yangu. Ameyasikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita jina lake Dani
7 Bilha mtumishi wa kike wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili.
Bilha, mjakazi wa Raheli, akashika mimba tena na kumzalia Yakobo mwana wa pili.
8 Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na ndugu yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita Naftali.
Raheli akasema, “Kwa mashindano yenye nguvu nimeshindana na dada yangu na kushinda.” Akamwita jina lake Naftali.
9 Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mtumishi wake wa kike Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake.
Lea alipoona kwamba ameacha kuzaa, akamchukua Zilpa, mjakazi wake, na kumpa Yakobo kama mke wake.
10 Mtumishi wa Lea yaani Zilpa, akamzalia Yakobo mwana.
Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana.
11 Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita Gadi.
Lea akasema, “Hii ni bahati njema!” Hivyo akamwita jina lake Gadi.
12 Mtumishi wa kike wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili.
Kisha Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili.
13 Ndipo Lea aliposema, “Jinsi gani nilivyo na furaha! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita Asheri.
Lea akasema, “Nina furaha! Kwa maana mabinti wataniita furaha.” Hivyo akamwita jina lake Asheri.
14 Wakati wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akakuta tunguja, ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
Siku za mavuno ya ngano Rubeni akaenda shambani na kuona tunguja. Akazileta kwa mama yake. Kisha Raheli akamwambia Lea, “Nipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
15 Lakini Lea akamwambia, “Haikukutosha kumtwaa mume wangu? Je, utachukua na tunguja za mwanangu pia?” Raheli akasema, “Vema sana! Yakobo atakutana nawe kimwili leo usiku, kwa malipo ya tunguja za mwanao.”
Lea akamwambia, “Je ni jambo dogo kwako, kumchukua mme wangu? Je na sasa unataka kuchukua tunguja za mwanangu pia? Raheli akasema, “Kisha atalala nawe leo usiku, kwa kubadilishana na tunguja za mwanao.
16 Kwa hiyo Yakobo alipokuja kutoka shambani jioni ile, Lea akaenda kumlaki, akamwambia, “Lazima ukutane nami kimwili. Nimekukodisha kwa tunguja za mwanangu.” Kwa hiyo akakutana naye kimwili usiku ule.
Jioni Yakobo akaja kutoka uwandani. Lea akaenda kumlaki na kusema, “Leo usiku utalala nami, kwani nimekuajiri kwa tunguja za mwanangu.” Hivyo Yakobo akalala na Lea usiku huo.
17 Mungu akamsikiliza Lea, naye akapata mimba akamzalia Yakobo mwana wa tano.
Mungu akamsikia Lea, na akashika mimba na kumzalia Yakobo mwana wa tano.
18 Ndipo Lea akasema, “Mungu amenizawadia kwa kumpa mume wangu mtumishi wangu wa kike.” Kwa hiyo akamwita Isakari.
Lea akasema, “Mungu amenipa ujira wangu, kwa sababu nilimpa mme wangu mjakazi wangu.” Akamwita jina lake Isakari.
19 Lea akapata mimba tena akamzalia Yakobo mwana wa sita.
Lea akashika mimba tena na kuzaa mwana wa tano kwa Yakobo.
20 Ndipo Lea aliposema, “Mungu amenizawadia kwa zawadi ya thamani sana. Wakati huu mume wangu ataniheshimu kwa sababu nimemzalia wana sita.” Kwa hiyo akamwita Zabuloni.
Lea akasema, “Mungu amenipa zawadi njema. Sasa mme wangu ataniheshimu, kwa sababu nimemzalia wana sita.” Akamwita jina lake Zabuloni.
21 Baadaye akamzaa mtoto wa kike akamwita Dina.
Baadaye akazaa binti na kumwita jina lake Dina.
22 Ndipo Mungu akamkumbuka Raheli, akasikia maombi yake na akafungua tumbo lake.
Mungu akamkumbuka Raheli na kumsikiliza. Akampa kushika mimba.
23 Akapata mimba na akamzaa mwana na kusema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”
Akashika mimba na kuzaa mwana. Akasema, “Mungu ameiondoa aibu yangu.”
24 Akamwita Yosefu na kusema, “Bwana na anipe mwana mwingine.”
Akamwita jina lake Yusufu, akisema, Yahwe ameniongeza mwana mwingine.”
25 Baada ya Raheli kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani, “Nipe ruhusa nirudi katika nchi yangu.
Baada ya Raheli kumzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, “Niache niande, ili kwamba niende nyumbani kwetu na katika nchi yangu.
26 Nipe wake zangu na watoto, ambao nimetumika kuwapata, nami niende zangu. Unajua ni kazi kiasi gani ambayo nimekufanyia.”
Nipe wake zangu na watoto wangu niliokutumikia kwa ajili yao, na uniache niondoke, kwani unafahamu nilivyokutumikia.
27 Lakini Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, tafadhali ukae. Nimegundua kwa njia ya uaguzi kwamba Bwana amenibariki kwa sababu yako.”
Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, subiri, kwa sababu nimejifunza kwa kutumia uaguzi kwamba Yahwe amenibariki kwa ajili yako.”
28 Akaongeza kumwambia, “Taja ujira wako nami nitakulipa.”
Kisha akasema, “Taja ujira wako, nami nitalipa.”
29 Yakobo akamwambia, “Unajua jinsi ambavyo nimekutumikia na jinsi ambavyo wanyama wako walivyolishwa vizuri chini ya uangalizi wangu.
Yakobo akamwambia, “Unajua nilivyokutumikia, na jinsi ambavyo mifugo wako wamekuwa nami.
30 Kidogo ulichokuwa nacho kabla sijaja kimeongezeka sana, naye Bwana amekubariki popote nilipokuwa. Lakini sasa, ni lini nitashughulikia mambo ya nyumba yangu mwenyewe?”
Kwani walikuwa wachache kabla sijaja, na wameongezeka kwa wingi. Popote nilipokutumikia Mungu amekubariki. Je ni lini mimi nitaandaa kwa ajili ya nyumba yangu pia?”
31 Labani akamuuliza, “Nikupe nini?” Yakobo akamjibu, “Usinipe chochote lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako.
Hivyo Labani akasema, “Je nikulipe nini? Yakobo akasema, 'Usinipe chochote. Ikiwa utafanya jambo hili kwa ajili yangu, nitawalisha tena kondoo wako na kuwatunza.
32 Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabakabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabakabaka. Hawa watakuwa ujira wangu.
Niache nipite kati ya kundi lako lote leo, kwa kuondoa kila kondoo mwenye milia na mabaka, na kila kondoo mweusi kati yao, na kati ya wenye mabaka na milia katika mbuzi. Hawa watakuwa ujira wangu.
33 Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi yeyote wangu ambaye hana mabakabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.”
Uadilifu wangu utashuhudia kwa ajili yangu hapo baadaye, utakapokuja kuangalia ujira wangu. Kila ambaye hana milia na hana madoa miongoni mwa mbuzi, na mweusi kati ya kondoo, ikiwa wataonekana kwangu, watahesabiwa kuwa wameibwa.”
34 Labani akasema, “Ninakubali na iwe kama ulivyosema.”
Labani akasema, “Nakubali. Na iwe kama yalivyo maneno yako.”
35 Siku ile ile Yakobo akawaondoa beberu wote waliokuwa na mistari au madoadoa na mbuzi wake wote waliokuwa na mistari au madoadoa (wote waliokuwa na alama nyeupe juu yao) na wana-kondoo weusi wote, akawaweka chini ya uangalizi wa wanawe.
Siku hiyo Labani akaondoa mabeberu yaliyokuwa na milia na madoa, na majike ya mbuzi yaliyokuwa na milia na madoa, kila aliyekuwa mweupe, na weusi wote katika mbuzi, akawakabidhi katika mikono ya wanaye.
36 Kisha Labani akamwacha Yakobo kwa mwendo wa safari ya siku tatu kati yake na Yakobo, wakati Yakobo akiendelea kuchunga lile kundi la Labani lililobaki.
Pia Labani akaweka safari ya siku tatu kati yake na Yakobo. Hivyo Yakobo akabaki kuchunga wale kondoo wa Labani waliosalia.
37 Hata hivyo, Yakobo, akachukua fito mbichi zilizokatwa wakati huo huo za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo.
Yakobo akachukua matawi mabichi yaliyokatwa ya mipopla, mlozi na mwaramoni mbichi akatoa maganda ili michilizi myeupe ionekane, na akaifanya sehemu nyeupe ya ndani ya mti iliyokuwa ndani ya fito ionekane.
38 Kisha akaweka fito alizozibambua kwenye mabirika yote ya kunyweshea mifugo, ili ziwe mbele ya makundi walipokuja kunywa maji. Wanyama walipokuja kunywa maji, hali wakiwa wanahitaji mbegu,
Kisha akaziweka fito alizokuwa amezibambua mbele ya makundi ya kondoo, mbele ya mabirika yakunyweshea walipokuja kunywa maji. Wakashika mimba walipokuja kunywa maji.
39 wakapandwa hizo fito zikiwa mbele yao. Wanyama waliopata mimba mbele ya hizo fito walizaa wanyama wenye mistari, madoadoa na mabakabaka.
Wanyama wakapandana mbele ya fito; nao wakazaa watoto wenye milia, mabaka na wenye madoa.
40 Yakobo akawatenga wadogo wa kundi peke yao, lakini akazielekeza nyuso za hao waliobaki kwenye wale wenye mistari na weusi waliokuwa mali ya Labani. Hivyo akatenga makundi yake mwenyewe, na wala hakuwachanganya na wanyama wa Labani.
Yakobo akawatenga hawa wanakondoo, lakini akawafanya waliosalia kuelekea wanyama wenye milia na kondoo weusi wote katika kundi la Labani. Kisha akayatenga makundi yake mwenyewe pekee na hakuwaweka pamoja na wale wa Labani.
41 Kila mara wanyama wenye nguvu walipohitaji mbegu, Yakobo aliweka zile fito kwenye mabirika mbele ya hao wanyama, ili wapandwe karibu na hizo fito,
Pindi kondoo wenye nguvu katika kundi walipopandana, Yakobo alilaza fito katika mabirika ya maji mbele ya macho ya kundi, ili kwamba washike mimba kati ya fito.
42 lakini ikiwa wanyama walikuwa wadhaifu hakuziweka hizo fito. Hivyo wanyama wadhaifu wakawa wa Labani, na wanyama wenye nguvu wakawa wa Yakobo.
Lakini wakati waliodhaifu walipokuja, hakuweka fito mbele yao. Hivyo wanyama dhaifu wakawa wa Labani, na wenye nguvu wakawa wa Yakobo.
43 Kwa njia hii Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, watumishi wa kike na wa kiume na ngamia na punda.
Mtu huyo akastawi sana. Akawa na kundi kubwa la kondoo, wajakazi na wajoli, ngamia na punda.

< Mwanzo 30 >