< Mwanzo 30 >
1 Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”
2 Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?”
3 Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mtumishi wangu wa kike. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto na kwa kupitia yeye mimi pia niweze kuwa na uzao.”
4 Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili,
5 Bilha akapata mimba, naye akamzalia Yakobo mwana.
6 Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu, amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita Dani.
7 Bilha mtumishi wa kike wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili.
8 Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na ndugu yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita Naftali.
9 Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mtumishi wake wa kike Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake.
10 Mtumishi wa Lea yaani Zilpa, akamzalia Yakobo mwana.
11 Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita Gadi.
12 Mtumishi wa kike wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili.
13 Ndipo Lea aliposema, “Jinsi gani nilivyo na furaha! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita Asheri.
14 Wakati wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akakuta tunguja, ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
15 Lakini Lea akamwambia, “Haikukutosha kumtwaa mume wangu? Je, utachukua na tunguja za mwanangu pia?” Raheli akasema, “Vema sana! Yakobo atakutana nawe kimwili leo usiku, kwa malipo ya tunguja za mwanao.”
16 Kwa hiyo Yakobo alipokuja kutoka shambani jioni ile, Lea akaenda kumlaki, akamwambia, “Lazima ukutane nami kimwili. Nimekukodisha kwa tunguja za mwanangu.” Kwa hiyo akakutana naye kimwili usiku ule.
17 Mungu akamsikiliza Lea, naye akapata mimba akamzalia Yakobo mwana wa tano.
18 Ndipo Lea akasema, “Mungu amenizawadia kwa kumpa mume wangu mtumishi wangu wa kike.” Kwa hiyo akamwita Isakari.
19 Lea akapata mimba tena akamzalia Yakobo mwana wa sita.
20 Ndipo Lea aliposema, “Mungu amenizawadia kwa zawadi ya thamani sana. Wakati huu mume wangu ataniheshimu kwa sababu nimemzalia wana sita.” Kwa hiyo akamwita Zabuloni.
21 Baadaye akamzaa mtoto wa kike akamwita Dina.
22 Ndipo Mungu akamkumbuka Raheli, akasikia maombi yake na akafungua tumbo lake.
23 Akapata mimba na akamzaa mwana na kusema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”
24 Akamwita Yosefu na kusema, “Bwana na anipe mwana mwingine.”
25 Baada ya Raheli kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani, “Nipe ruhusa nirudi katika nchi yangu.
26 Nipe wake zangu na watoto, ambao nimetumika kuwapata, nami niende zangu. Unajua ni kazi kiasi gani ambayo nimekufanyia.”
27 Lakini Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, tafadhali ukae. Nimegundua kwa njia ya uaguzi kwamba Bwana amenibariki kwa sababu yako.”
28 Akaongeza kumwambia, “Taja ujira wako nami nitakulipa.”
29 Yakobo akamwambia, “Unajua jinsi ambavyo nimekutumikia na jinsi ambavyo wanyama wako walivyolishwa vizuri chini ya uangalizi wangu.
30 Kidogo ulichokuwa nacho kabla sijaja kimeongezeka sana, naye Bwana amekubariki popote nilipokuwa. Lakini sasa, ni lini nitashughulikia mambo ya nyumba yangu mwenyewe?”
31 Labani akamuuliza, “Nikupe nini?” Yakobo akamjibu, “Usinipe chochote lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako.
32 Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabakabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabakabaka. Hawa watakuwa ujira wangu.
33 Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi yeyote wangu ambaye hana mabakabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.”
34 Labani akasema, “Ninakubali na iwe kama ulivyosema.”
35 Siku ile ile Yakobo akawaondoa beberu wote waliokuwa na mistari au madoadoa na mbuzi wake wote waliokuwa na mistari au madoadoa (wote waliokuwa na alama nyeupe juu yao) na wana-kondoo weusi wote, akawaweka chini ya uangalizi wa wanawe.
36 Kisha Labani akamwacha Yakobo kwa mwendo wa safari ya siku tatu kati yake na Yakobo, wakati Yakobo akiendelea kuchunga lile kundi la Labani lililobaki.
37 Hata hivyo, Yakobo, akachukua fito mbichi zilizokatwa wakati huo huo za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo.
38 Kisha akaweka fito alizozibambua kwenye mabirika yote ya kunyweshea mifugo, ili ziwe mbele ya makundi walipokuja kunywa maji. Wanyama walipokuja kunywa maji, hali wakiwa wanahitaji mbegu,
39 wakapandwa hizo fito zikiwa mbele yao. Wanyama waliopata mimba mbele ya hizo fito walizaa wanyama wenye mistari, madoadoa na mabakabaka.
40 Yakobo akawatenga wadogo wa kundi peke yao, lakini akazielekeza nyuso za hao waliobaki kwenye wale wenye mistari na weusi waliokuwa mali ya Labani. Hivyo akatenga makundi yake mwenyewe, na wala hakuwachanganya na wanyama wa Labani.
41 Kila mara wanyama wenye nguvu walipohitaji mbegu, Yakobo aliweka zile fito kwenye mabirika mbele ya hao wanyama, ili wapandwe karibu na hizo fito,
42 lakini ikiwa wanyama walikuwa wadhaifu hakuziweka hizo fito. Hivyo wanyama wadhaifu wakawa wa Labani, na wanyama wenye nguvu wakawa wa Yakobo.
43 Kwa njia hii Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, watumishi wa kike na wa kiume na ngamia na punda.