< Mwanzo 3 >

1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”
Sasa nyoka alikuwa mwerevu kuliko myama mwingine yeyote wa kondeni ambaye Yahwe Mungu alikuwa amemuumba. Akamwambia mwanamke, “Je ni kweli Mungu amesema, 'Msile matunda kutoka kwenye mti wowote bustanini'?”
2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini,
Mwanamke akamwambia nyoka, “Twaweza kula tunda kutoka kwenye miti ya bustani,
3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’”
lakini kuhusu tunda la mti ambao uko katikati ya bustani, Mungu alisema, 'msile, wala msiuguse, vinginevyo mtakufa.'”
4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa.
Nyoka akamwambia mwanamke, “hakika hamtakufa.
5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
Kwasababu Mungu anajua kwamba siku mkila macho yenu yatafumbuliwa, na mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
6 Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala.
Na mwanamke alipoona kuwa mti ni mzuri kwa chakula, na kuwa unapendeza macho, na kwamba mti ulitamanika kwa kumfanya mtu awe mwerevu, alichukua sehemu ya tunda na akala. Na sehemu yake pia akampatia mumewe aliyekuwa naye, naye akala.
7 Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika.
Macho ya wote wawili yalifumbuliwa, na wakajua kuwa wako uchi. Wakashona majani ya miti pamoja na wakatengeneza vya kujifunika wao wenyewe.
8 Ndipo yule mwanaume na mkewe, waliposikia sauti ya Bwana Mungu alipokuwa akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka mbele za Bwana Mungu katikati ya miti ya bustani.
Wakasikia sauti ya Yahwe Mungu akitembea bustanini majira ya kupoa kwa jua, kwa hiyo mwanaume na mke wake wakajificha wao wenyewe kwenye miti ya bustani kuepuka uwepo wa Yahwe Mungu.
9 Lakini Bwana Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?”
Yahwe Mungu akamuita mwanaume na kumwambia, “uko wapi?”
10 Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.”
Mwanaume akasema, “nilikusikia bustanini, na nkaogopa, kwa sababu nilikuwa uchi. kwa hiyo nikajificha.”
11 Mungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?”
Mungu akasema, “Ni nani alikwambia kuwa ulikuwa uchi? Je umekula kutoka mti ambao nilikuagiza usile matunda yake?”
12 Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.”
Mwanaume akasema, “Mwanamke uliyenipa kuwa na mimi, alinipatia tunda kutoka kwenye mti, na nikala.”
13 Ndipo Bwana Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
Yahwe Mungu akamwambia mwanamke, “Nini hiki ulichofanya?” mwanamke akasema, “nyoka alinidanganya, na nikala.”
14 Hivyo Bwana Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili, “Umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa na wa porini! Utatambaa kwa tumbo lako na kula mavumbi siku zote za maisha yako.
Yahwe Mungu akamwambia nyoka, “kwa sababu umefanya jambo hili, umelaaniwa wewe mwenyewe miongoni mwa wanyama wote wa kufugwa na wanyama wote wa mwituni. Itakuwa kwa tumbo lako utakwenda, na mavumbi utakula kwa siku zote za maisha yako.
15 Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na wake, yeye atakuponda kichwa, nawe utamuuma kisigino.”
Nitaweka uadui kati yako na mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake. Atakujeruhi kichwa chako na utamjeruhi kisigino chake.”
16 Kwa mwanamke akasema, “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto. Tamaa yako itakuwa kwa mumeo naye atakutawala.”
Kwa mwanamke akasema, nitaongeza uchungu wakati wa kuzaa watoto; itakuwa katika maumivu utazaa watoto. Tamaa yako itakua kwa mume wako, lakini atakutawala.”
17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’ “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako, kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo siku zote za maisha yako.
Kwa Adam akasema, “kwa sababu umesikiliza sauti ya mke wako, na umekula kutoka katika mti, ambao nilikuagiza, nikisema, “usile matunda yake', ardhi imelaaniwa kwa sababu yako; kupitia kazi yenye maumivu utakula matunda ya ardhi kwa siku zote za maisha yako.
18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako, nawe utakula mimea ya shambani.
Ardhi itazaa miiba na mbigili kwa ajili yako, na utakula mimea ya shambani.
19 Kwa jasho la uso wako utakula chakula chako hadi utakaporudi ardhini, kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo, kwa kuwa wewe u mavumbi na mavumbini wewe utarudi.”
Kwa jasho la uso wako utakula mkate, mpaka utakapo irudia ardhi, ambayo kwayo ulitwaliwa. kwa kuwa wewe ni mavumbi na kwenye mavumbi utarudi.”
20 Adamu akamwita mkewe Eva, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.
Mwanaume akaita mke wake jina Hawa kwa sababu alikuwa mama wa wote wenye uhai.
21 Bwana Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.
Yahwe Mungu akatengeneza mavazi ya ngozi kwa ajili ya Adam na mke wake na akawavalisha.
22 Kisha Bwana Mungu akasema, “Sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kunyoosha mkono wake na kuchuma pia kutoka mti wa uzima akala, naye akaishi milele.”
Yahwe Mungu akasema, “sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, ajuaye mema na mabaya. Kwa hiyo sasa hataruhusiwa kugusa kwa mkono wake, na kuchukua tunda la mti wa uzima, na kula akaishi tena milele.”
23 Hivyo Bwana Mungu akamfukuzia mbali kutoka Bustani ya Edeni, akalime ardhi ambamo alitolewa.
Kwa hiyo Yahwe Mungu akamuondoa kutoka kwenye bustani ya Edeni, kwenda kulima ardhi ambayo kwahiyo alikuwa ametwaliwa.
24 Baada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki ya Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika huku na huko kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima.
Kwa hiyo Mungu akamfukuza mtu huyu nje ya bustani, na akaweka kerubi mashariki mwa bustani ya Edeni, na upanga wa moto ulio geuka geuka kila upande, ili kulinda njia ya kwenda kwenye mti wa uzima.

< Mwanzo 3 >