< Mwanzo 27 >
1 Isaki alipokuwa mzee na macho yake yalipokuwa yamekosa nguvu asiweze kuona tena, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.” Akajibu, “Mimi hapa.”
Isaka alipozeeka na macho yake kuwa mazito kiasi cha kutokuona, alimwita Esau, mwanawe mkubwa, na akamwambia, “Mwanangu. Yeye akasema, “Mimi hapa.”
2 Isaki akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kifo changu.
Akamwambia, “Tazama, mimi nimezeeka. Sijui siku ya kufa kwangu.
3 Sasa basi, chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukawinde nyama pori kwa ajili yangu.
Kwahiyo chukua silaha zako, podo lako na upinde wako, na uende uwandani ukaniwindie mnyama.
4 Uniandalie aina ya chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili niweze kukubariki kabla sijafa.”
Uniandalie chakula kitamu, aina ile niipendayo, uniletee ili nikile na kukubariki kabla sijafa.
5 Basi Rebeka alikuwa akisikiliza Isaki alipokuwa akizungumza na mwanawe Esau. Esau alipoondoka kwenda nyikani kuwinda nyama pori na kuleta,
Basi Rebeka akasikia Isaka alipoongea na Esau mwanawe. Esau akaenda uwandani kuwinda mawindo na kuja nayo.
6 Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau,
Rebeka akaongea na Yakobo mwanawe na kumwambia, “Tazama, nimemsikia baba yako akiongea na Esau ndugu yako. Akasema,
7 ‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili niweze kukubariki mbele za Bwana kabla sijafa.’
'Niletee mnyama na unitengenezee chakula kitamu, ili nikile na kukubariki mbele za Yahwe kabla ya kufa kwangu.'
8 Sasa, mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia:
Kwa hiyo sasa, mwanangu, usikilize sauti yangu kama ninavyokuagiza,
9 Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili niandalie chakula kitamu kwa ajili ya baba yako, kama vile anavyopenda.
Nenda kundini, na uniletee wanambuzi wawili; nami nitaandaa chakula kitamu kutokana nao kwa ajili ya baba yako, kwa namna aipendayo.
10 Kisha umpelekee baba yako ale, ili apate kukubariki kabla hajafa.”
Utakipeleka kwa baba yako, ili kwamba akile, na kukubariki kabla hajafa.”
11 Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, mimi nina ngozi nyororo.
Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Tazama, Ndugu yangu Esau ni mtu mwenye manyoya, na mimi ni mtu laini.
12 Itakuwaje kama baba yangu akinigusa? Itaonekana kwake kama niliyemfanyia ujanja na kuleta laana juu yangu badala ya baraka.”
Pengine baba yangu atanigusa, nami nitaonekana kama mdanganyifu kwake. Nami nitajiletea laana badala ya baraka.”
13 Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia, nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.”
Mama yake akamwambia, “Mwanangu, acha laana yoyote iwe juu yangu. Wewe sikiliza sauti yangu, nenda, uniletee.”
14 Kwa hiyo alikwenda akawaleta, akampa mama yake, akaandaa chakula kitamu, kama vile alivyopenda baba yake.
Hivyo Yakobo alikwenda na kuchukua wanambuzi na kuwaleta kwa mama yake, na mama yake akaandaa chakula kitamu, kama alichokipenda baba yake.
15 Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo.
Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau, mwanawe mkubwa, alizokuwa nazo nyumbani mwake, na akamvika Yakobo, mwanawe mdogo.
16 Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi.
Akamvalisha ngozi ya mwanambuzi katika mikono yake na katika sehemu laini za shingo yake.
17 Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.
Akaweka katika mikono ya Yakobo kile chakula kitamu na mkate aliokuwa ameuandaa.
18 Akamwendea baba yake akasema, “Baba yangu.” Akajibu, “Naam, mwanangu, wewe ni nani?”
Yakobo akaenda kwa baba yake na kumwambia, “Babangu.” Yeye akasema, “Mimi hapa; U nani wewe, mwanangu?”
19 Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili uweze kunibariki.”
Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza; nimefanya kama ulivyoniagiza. Basi kaa na ule sehemu ya mawindo yangu, ili unibariki.”
20 Isaki akamuuliza mwanawe. “Umepataje haraka namna hii, mwanangu?” Akajibu, “Bwana Mungu wako amenifanikisha.”
Isaka akamwambia mwanawe, “Imekuwaje umepata kwa haraka hivyo, mwanangu?” Akasema, “Ni kwa sababu Yahwe Mungu wako ameniletea.”
21 Kisha Isaki akamwambia Yakobo, “Mwanangu tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.”
Isaka akamwambia Yakobo, “Njoo karibu nami, ili nikuguse, mwanangu, ili nijue kama kweli wewe ni mwanangu Esau au hapana.”
22 Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaki, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.”
Yakobo akamkaribia Isaka baba yake; na Isaka akamgusa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mkikono ya Esau.”
23 Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki.
Isaka hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na manyoya, kama mikono ya Esau ndugu yake, hivyo Isaka akambariki.”
24 Akamuuliza, “Hivi kweli wewe ni mwanangu Esau?” Akajibu, “Mimi ndiye.”
Akasema, “Wewe kweli ni mwanangu Esau?” Naye akasema, “Ni mimi.”
25 Kisha akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nipate kukubariki.” Yakobo akamletea naye akala, akamletea na divai akanywa.
Isaka akasema, “Kilete chakula kwangu, na nile mawindo yako, ili nikubariki.” Yakobo akakileta chakula kwake. Isaka akala, na Yakobo akamletea mvinyo, akanywa.
26 Kisha Isaki baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.”
Kisha Isaka baba yake akamwambia, “Sogea karibu nami na unibusu, mwanangu.”
27 Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaki aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema, “Aha, harufu ya mwanangu ni kama harufu ya shamba ambalo Bwana amelibariki.
Yakobo akasogea na kumbusu, naye akanusa harufu ya nguo zake na kumbariki. Akasema, “Tazama, harufu ya mwanangu ni kama harufu ya shamba alilolibariki Yahwe.
28 Mungu na akupe umande kutoka mbinguni na utajiri wa duniani: wingi wa nafaka na divai mpya.
Mungu akupe sehemu ya umande wa mbinguni, sehemu ya unono wa nchi, na wingi wa nafaka na mvinyo mpya.
29 Mataifa na yakutumikie na mataifa yakusujudie. Uwe bwana juu ya ndugu zako, na wana wa mama yako wakusujudie. Walaaniwe wale wakulaanio, nao wale wakubarikio wabarikiwe.”
Watu na wakutumikie na mataifa yainame chini yako. Uwe bwana juu ya ndugu zako, na wana wa mama yako wainame chini yako. Kila anayekulaani na alaaniwe; na kila anayekubariki abarikiwe.”
30 Baada ya Isaki kumaliza kumbariki na baada tu ya Yakobo kuondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni.
Mara Isaka alipomaliza kumbariki Yakobo, na Yakobo ndo ametoka mbele ya Isaka baba yake, Esau ndugu yake akaja kutoka kuwinda.
31 Naye pia akaandaa chakula kitamu akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.”
Yeye pia akaandaa chakula kitamu na kukileta kwa baba yake. Akamwambia baba yake, “Baba, inuka na ule baadhi ya mawindo ya mwanao, ili uweze kunibariki.”
32 Isaki baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?” Akajibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.”
Isaka baba yake akamwambia, “U nani wewe? Akasema, “Mimi ni mwanao, Esau, mzaliwa wako wa kwanza.”
33 Isaki akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!”
Isaka akatetemeka sana na kusema, “Alikuwa nani aliyewinda mawindo nakuniletea? Nilikula chote kabla haujaja, nami nimembariki. Atabarikiwa, kwa kweli.”
34 Esau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki mimi, mimi pia, baba yangu!”
Esau aliposikia maneno ya baba yake, akalia kwa kilio kikubwa na cha uchungu sana, na akamwambia baba yake, “Unibariki nami, mimi pia, babangu.”
35 Lakini akasema, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu na akachukua baraka yako.”
Isaka akasema, “Ndugu yako alikuja hapa kwa hila na amechukua baraka yako.”
36 Esau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?”
Esau akasema, “Je hakuitwa Yakobo kwa haki? Kwa maana amenidanganya mara mbili hizi. Alichukua haki ya uzaliwa wangu wa kwanza, na tazama, sasa amechukua baraka yangu.” Na akasema, “Je haukuniachia baraka?
37 Isaki akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako, pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?”
Isaka akajibu na kumwambia Esau, “Tazama, nimemfanya kuwa bwana wako, na nimempa ndugu zake kuwa watumishi wake. Na nimempa nafaka na divai. Je nikufanyie nini mwanangu?
38 Esau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa.
Esau akamwambia babaye, “Je hauna hata baraka moja kwa ajili yangu, babangu? Nibariki nami, hata mimi pia, babangu.” Esau akalia kwa sauti.
39 Baba yake Isaki akamjibu, akamwambia, “Makao yako yatakuwa mbali na utajiri wa dunia, mbali na umande wa mbinguni juu.
Isaka baba yake akajibu na kumwambia, “Tazama, mahali unapoishi patakuwa mbali na utajiri wa nchi, mbali na umande juu angani.
40 Utaishi kwa upanga, nawe utamtumikia ndugu yako, lakini wakati utakapokuwa umejikomboa, utatupa nira yake kutoka shingoni mwako.”
Kwa upanga wako utaishi, nawe utamtumikia ndugu yako. lakini utakapoasi, utaiondoa nira yake shingoni mwako.”
41 Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia, ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”
Esau akamchukia Yakobo kwa sababu ya baraka ambayo baba yake alimpa. Esau akajisemea moyoni, “Siku za maombolezo kwa ajili ya baba yangu zinakaribia; baada ya hapo nitamwua Yakobo ndugu yangu.”
42 Rebeka alipokwisha kuambiwa yale aliyoyasema Esau mwanawe mkubwa, alimwita Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua.
Rebeka akaambiwa maneno ya Esau mwanawe mkubwa. Hivyo akatuma na kumwita Yakobo mwanawe mdogo na kumwambia, “Tazama, Esau ndugu yako anajifariji juu yako kwa kupanga kukuuwa.
43 Sasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani.
Kwa hiyo sasa, mwanangu, unisikie na kukimbilia kwa Labani, ndugu yangu, huko Harani.
44 Ukae naye kwa muda mpaka ghadhabu ya ndugu yako itulie.
Ukae naye kitambo, mpaka hasira ya ndugu yako itakapopungua,
45 Wakati ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze wote wawili kwa siku moja?”
hata hasira ya ndugu yako itakapokuondokea, na kusahau ulivyomtenda. Kisha nitatuma na kukurudisha kutoka pale. Kwa nini niwapoteze ninyi nyote katika siku moja?
46 Kisha Rebeka akamwambia Isaki, “Nimechukia kuishi kwa sababu ya hawa wanawake wa Kihiti. Ikiwa Yakobo ataoa mke miongoni mwa wanawake wa nchi hii, wanawake wa Kihiti kama hawa, sitakuwa na faida kuendelea kuishi.”
Rebeka akamwambia Isaka, “Nimechoka na maisha kwa sababu ya hawa binti za Hethi. Ikiwa Yakobo atachukua mmojawapo wa binti wa Hethi kuwa mkewe, kama wanawake hawa, baadhi ya binti za nchi, maisha yatakuwa na maana gani kwangu?”