< Mwanzo 26 >

1 Basi njaa kubwa ikawa katika nchi hiyo, kuliko ile njaa iliyotangulia iliyotokea wakati wa Abrahamu. Isaki akamwendea Abimeleki mfalme wa Wafilisti huko Gerari.
Basi njaa ikatokea katika nchi, mbali na njaa ya kwanza iliyotokea siku za Ibrahimu. Isaka akaenda kwa Abimeleki, mfalme wa Wafilisiti huko Gerari.
2 Bwana akamtokea Isaki, akamwambia, “Usiende Misri, bali ukae katika nchi nitakayokuambia.
Basi Yahwe akamtokea na kumwambia, “Usishuke kwenda Misri; kaa katika nchi niliyokuambia.
3 Kaa katika nchi hii kwa kitambo, mimi nitakuwa pamoja na wewe na nitakubariki. Kwa maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote na nitatimiza kiapo nilichomwapia Abrahamu baba yako.
Kaa katika nchi hii hii niliyokuambia, nami nitakuwa pamoja nawe na kukubariki; kwani kwako wewe na uzao wako, nitawapa nchi hii yote, nami nitatimiza kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.
4 Nitafanya wazao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa nchi hizi zote na kutokana na uzao wako mataifa yote yatabarikiwa,
Nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote. Kupitia uzao wako mataifa yote ya dunia yatabarikiwa.
5 kwa sababu Abrahamu alinitii mimi akatunza kanuni zangu na maagizo yangu, amri zangu pamoja na sheria zangu.”
Nitalifanya hili kwa sababu Ibrahimu aliitii sauti yangu na kutunza maelekezo yangu, amri zangu na sheria zangu.”
6 Hivyo Isaki akaishi huko Gerari.
Hivyo Isaka akakaa Gerari.
7 Watu wa mahali pale walipomuuliza habari za mke wake, akasema, “Huyu ni dada yangu,” kwa sababu aliogopa kusema, “Huyu ni mke wangu.” Alifikiri, “Watu wa mahali pale wataweza kumuua kwa sababu ya Rebeka, kwa kuwa alikuwa mzuri wa sura.”
Watu wa eneo hilo walipomwuliza juu ya mke wake, alisema, “Yeye ni dada yangu.” Aliogopa kusema, “Yeye ni mke wangu,” kwa kuwa alidhani, “Watu wa nchi hii wataniua ili wamchukue Rebeka, kwa kuwa ni mzuri wa uso.”
8 Wakati Isaki alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki mfalme wa Wafilisti akachungulia dirishani, akaona jinsi Isaki alivyomkumbatia Rebeka mke wake.
Baada ya Isaka kuwa amekaa pale kwa muda mrefu, Ikatukia kwamba Abimeleki mfalme wa Wafilisiti alichungulia katika dirisha. Tazama, akamwona Isaka akimpapasa Rebeka, mke wake.
9 Abimeleki akamwita Isaki akamwambia, “Hakika huyu ni mke wako! Mbona uliniambia, ‘Huyu ni dada yangu?’” Isaki akamjibu, “Kwa sababu nilifikiri ningeweza kuuawa kwa sababu yake.”
Abimeleki akamwita Isaka kwake na kusema, “Tazama, kwa hakika yeye ni mke wako. Kwa nini ulisema, 'Yeye ni dada yangu?” Isaka akamwambia, “Kwa sababu nilidhani mtu mmoja aweza kuniua ili amchukue.”
10 Ndipo Abimeleki akamjibu, “Ni nini hiki ulichotufanyia? Ingewezekana mtu yeyote akawa amekutana kimwili na mke wako, nawe ungeleta hatia juu yetu.”
Abimeleki akamwambia, “Ni jambo gani hili ulilotufanyia? Mmojawapo wa watu angeweza bila shaka kulala na mke wako, nawe ungeweza kuleta hatia juu yetu.”
11 Hivyo Abimeleki akatoa amri kwa watu wote, akisema, “Yeyote atakayemnyanyasa mtu huyu au mkewe hakika atauawa.”
Hivyo Abimeleki akawaonya watu wote na kusema, “Mtu yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake atauwawa.”
12 Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki.
Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo na kuvuna mwaka huo vipimo mia, kwa kuwa Yahwe alimbariki.
13 Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana.
Mtu huyo akawa tajiri, naye akaongezeka zaidi hata akawa mkuu sana.
14 Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu.
Alikuwa na kondoo na ngombe na familia kubwa. Wafilisiti wakamwonea wivu.
15 Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Abrahamu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo.
Basi visima vyote watumishi wa baba yake walikuwawamevichimba katika siku za Ibrahimu baba yake, Wafilisiti wakavikatalia kwa kwa kuvijaza kifusi.
16 Ndipo Abimeleki akamwambia Isaki, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.”
Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kati yetu, kwa kuwa wewe una nguvu kuliko sisi.”
17 Basi Isaki akatoka huko akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko.
Hivyo Isaka akaondoka pale na kukaa katika bonde la Gerari, na kuishi pale.
18 Ndipo Isaki akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Abrahamu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya kufa Abrahamu, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa.
Kwa mara nyingine tena Isaka akachimba visima vya maji, vilivyokuwa vimechimbwa siku za Ibrahimu baba yake. Wafilisiti walikuwa wamevizuia baada ya kufa kwake Ibrahimu. Isaka akaviita visima kwa majina aliyokuwa ameviita baba yake.
19 Watumishi wa Isaki wakachimba katika lile bonde wakagundua huko kisima chenye maji safi.
Watumishi wa Isaka walipochimba katika bonde, wakaona kisima cha maji yaliyokuwakuwa yakibubujika.
20 Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaki wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.
Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka, na kusema, “Haya ni maji yetu.”Hivyo Isaka akakiita kisima hicho “Eseki,” kwa sababu waligombana naye.
21 Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania, akakiita Sitna.
Wakachimba kisima kingine, wakakigombania hicho nacho, hivyo akakiita “Sitina.”
22 Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi, akisema, “Sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.”
Akatoka hapo na akachimba kisima kingine, lakini hicho hawakukigombania. Hivyo akakiita Rehobothi, na akasema, “Sasa Yahwe ametufanyia nafasi, na tutafanikiwa katika nchi.”
23 Kutoka pale akaenda Beer-Sheba.
Kisha Isaka akaenda Beersheba.
24 Usiku ule Bwana akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa Abrahamu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi niko pamoja nawe, nitakubariki na kuongeza idadi ya wazao wako kwa ajili ya Abrahamu mtumishi wangu.”
Yahwe akamtokea usiku huohuo na akasema, “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi nipo pamoja nawe na nitakubariki na kuvidisha vizazi vyako, kwa ajili ya mtumishi wangu Ibrahimu.”
25 Isaki akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. Akapiga hema lake huko, nao watumishi wake wakachimba kisima.
Isaka akajenga madhabahu pale na akaliita jina la Yahwe. Akapiga hema yake pale, na watumishi wake wakachimba kisima.
26 Wakati huo, Abimeleki alikuwa amemjia kutoka Gerari, akifuatana na Ahuzathi mshauri wake, pamoja na Fikoli jemadari wa majeshi yake.
Kisha Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi, rafiki yake, na Fikoli, jemedari wa jeshi.
27 Isaki akawauliza, “Mbona mmekuja kwangu na ninyi mlinichukia na kunifukuza?”
Isaka akawambia, “Kwa nini mmekuja kwangu, kwani mlinichukia na kunifukuza kwenu.
28 Wakamjibu, “Tuliona wazi kuwa Bwana alikuwa pamoja nawe, kwa hiyo tukasema, ‘Inabidi kuwe na kiapo cha mapatano kati yetu, kati yetu na wewe. Na tufanye mkataba pamoja nawe
Nao wakasema, “Tumeona yakini kwamba Yahwe amekuwa nawe. Hivyo tukaamua kwamba kuwe na kiapo kati yetu, ndiyo, kati yetu nawe. Hivyo na tufanye agano nawe,
29 kwamba hutatudhuru, kama jinsi nasi hatukuwanyanyasa bali tuliwatendea mema wakati wote na kuwaondoa kwetu kwa amani. Tena sasa umebarikiwa na Bwana.’”
kwamba hautatudhuru, kama ambavyo sisi hatukukudhuru, na kama sisi tulivyokutendea vema wewe na tumekuacha uondoke kwa amani. Kwa kweli, Yahwe amekubariki.”
30 Basi Isaki akawaandalia karamu, nao wakala na kunywa.
Hivyo Isaka akawaandalia sherehe, na wakala na kunywa.
31 Kesho yake asubuhi na mapema, wakaapizana wao kwa wao. Kisha Isaki akawaruhusu waende zao, wakamwacha Isaki kwa amani.
Wakaamuka mapema asubuhi na wakaapiana kiapo. Kisha Isaka akawaruhusu kuondoka, nao wakamwacha katika amani.
32 Siku hiyo watumishi wa Isaki wakaja wakampa habari kuhusu kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, “Tumepata maji!”
Siku hiyohiyo watumishi wake wakaja na kumwambia juu ya kisima walichokuwa wamekichimba. Wakasema, “Tumeona maji.”
33 Naye akakiita Shiba, mpaka leo mji huo unaitwa Beer-Sheba.
Akakiita kile kisima Shiba, hivyo jina la mji ule ni Beersheba hata leo.
34 Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akamwoa Yudithi binti Beeri Mhiti, kisha akamwoa Basemathi binti Eloni Mhiti.
Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akajitwalia mke, Yudithi binti Beeri Mhiti, na Basemathi binti Eloni Mhiti.
35 Hawa walikuwa chanzo cha huzuni ya Isaki na Rebeka.
Wakamhuzunisha Isaka na Rebeka.

< Mwanzo 26 >