< Mwanzo 24 >
1 Wakati huu Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, naye Bwana alikuwa amembariki katika kila njia.
Basi Abraham alikuwa mzee sana na Yahwe akawa amembariki katika mambo yote.
2 Akamwambia mtumishi wake mkuu wa vitu vyote katika nyumba yake, yule aliyekuwa msimamizi wa vitu vyote alivyokuwa navyo, “Weka mkono wako chini ya paja langu,
Abraham akamwambia mtumwa wake, ambaye alikuwa mkubwa kuliko wote wa nyumbani mwake na mkuu wa vyote alivyo kuwa navyo.”Weka mkono wako chini ya paja langu
3 Ninataka uape kwa Bwana, Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao,
na nitakufanya uape kwa Yahwe, Mungu wa Mbingu na nchi, kwamba hutampatia mwanangu mke kutoka kwa mabinti wa Wakanaani, miongoni mwao wale nikaao kati yao.
4 bali utakwenda katika nchi yangu na jamaa zangu umpatie Isaki mwanangu mke.”
Lakini utakwenda kwenye nchi yangu, na kwa ndugu zangu, na kumtafutia mwanangu Isaka mke.”
5 Yule mtumishi akamuuliza, “Je, kama huyo mwanamke atakataa kuja nami katika nchi hii? Je, nimpeleke mwanao katika hiyo nchi uliyotoka?”
Yule mtumwa wake akamwambia, “Itakuwaje ikiwa mwanamke hatakuwa tayari kufuatana nami hadi katika nchi hii? Je nitamrudisha mwanao katika nchi ambayo ulitoka?”
6 Abrahamu akasema, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu huko.
Abraham akamwambia, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu kule!
7 Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na nchi yangu niliyozaliwa na aliyesema nami na akaniahidi kwa kiapo, akisema, ‘Nitawapa watoto wako nchi hii,’ atatuma malaika wake akutangulie ili umpatie mwanangu mke kutoka huko.
Yahwe, Mungu wa mbingu, ambaye alinitoa mimi kutoka katika nyumba ya baba yangu na kutoka katika nchi ya ndugu zangu, na ambaye aliniahidia kwa kiapo maalumu akisema, 'Nitawapa uzao wako nchi hii,' atatuma malaika wake mbele yako, na utapata mke kwa ajili ya mwanangu kutoka huko.
8 Kama huyo mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi utafunguliwa kutoka kiapo nilichokuapisha. Ila usimrudishe mwanangu huko.”
Lakini ikiwa mwanamke hatakuwa tayari, ndipo utakuwa huru katika hiki kiapo changu. Cha muhimu tu ni kwamba usije ukamrudisha mwanangu huko.”
9 Basi yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la bwana wake Abrahamu akamwapia kuhusu shauri hili.
Kwa hiyo mtumwa akaweka mkono wake jini ya paja la Abraham bwana wake, na akaapa kuhusiana na jambo hili.
10 Ndipo huyo mtumishi akachukua ngamia kumi miongoni mwa ngamia za bwana wake, akaondoka, akiwa amechukua aina zote za vitu vizuri kutoka kwa bwana wake. Akaelekea Aramu-Naharaimu na kushika njia kwenda mji wa Nahori.
Mtumwa akachukua ngamia kumi wa bwana wake na akaondoka. Akachukua pia aina zote za zawadi kutoka kwa bwana wake. Akaondoka na kwenda katika mkoa wa Aramu Naharaimu, mji wa Nahori.
11 Akawapigisha ngamia magoti karibu na kisima cha maji nje ya mji, ilikuwa inaelekea jioni, wakati ambapo wanawake wanakuja kuteka maji.
Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji. Ilikuwa jioni wakati ambao wanawake huenda kuchota maji.
12 Kisha akaomba, “Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nipatie ushindi leo, uonyeshe huruma kwa bwana wangu Abrahamu.
Kisha akasema, “Yahwe, Mungu wa bwana wangu Abraham, anijalie kufanikiwa leo na aoneshe agano la uaminifu kwa bwana wangu Abraham.
13 Tazama, nimesimama karibu na kisima hiki cha maji, nao binti za watu wa mji huu wanakuja kuteka maji.
Tazama, nimesimama hapa karibu na chemchemi ya maji na binti za watu wa mji wanakuja kuteka maji.
14 Basi na iwe hivi, nitakapomwambia binti mmojawapo, ‘Tafadhali tua mtungi wako nipate kunywa maji,’ naye akisema, ‘Kunywa, nitawanywesha na ngamia wako pia.’ Basi na awe ndiye uliyemchagua kwa ajili ya mtumishi wako Isaki. Kwa hili nitajua umemhurumia bwana wangu.”
Na itokee hivi kwamba. Nikimwambia msichana, tafadhari tua mtungi wako ili niweze kunywa maji,' na akiniambia, 'Kunywa, na kwamba nitawanywesha ngamia wako pia,' huyo ndiye awe ambaye umemchagulia mtumwa wako Isaka. Kwa njia hii nitajua kuwa umeonesha agano la uaminifu kwa bwana wangu.”
15 Ikawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti wa Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Abrahamu.
Ikawa kwamba hata kabla hajamaliza kuzungumza, tazama, Rebeka akaja akiwa na mtungi wake wa maji begani mwake. Rebeka alizaliwa na Bethueli mwana wa Milka, mke wa Nahori, ndugu yake na Abraham.
16 Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mtu aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake akapanda juu.
Msichana huyu alikuwa mzuri na alikuwa bikira. Hapana mwanaume aliye kuwa amekwisha lala naye. Akashuka kisimani na kuujaza mtungi wake, na kupanda juu.
17 Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.”
Kisha mtumwa yule akakimbia kumlaki yule msichana, na kusema, “Tafadhari nipatie maji kidogo ya kunywa kutoka katika mtungi wako.”
18 Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa.
Akasema, “kunywa tafadhari bwana wangu,” na kwa haraka akatua mtungi wake juu ya mkono wake, na akampatia maji ya kunywa.
19 Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitateka maji kwa ajili ya ngamia zako pia mpaka wote watosheke.”
Alipokuwa amemaliza kumpatia maji, akasema, “Nitachota maji kwa ajili ya ngamia wako pia, mpaka watakapomaliza kunywa.”
20 Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote.
Hivyo akaharakisha akamwaga maji yaliyokuwa mtungini kwenye chombo cha kunywshea mifugo, kisha akakimbia tena kisimani kuchota maji, na kuwanywesha ngamia wake wote.
21 Pasipo kusema neno, yule mtumishi akamtazama kwa makini aone kama Bwana ameifanikisha safari yake, au la.
Yule mtu akamtazama msichana akiwa kimya kuona kama Yahwe amefanikisha njia yake au la.
22 Ikawa ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtumishi akampa huyo msichana pete ya puani ya dhahabu yenye uzito wa beka moja na bangili mbili za dhahabu zenye uzito wa shekeli kumi.
Ngamia walipomaliza kunywa maji, yule mtu akaleta pete ya pua ya dhahabu yenye uzito wa nusu shekeli, na bangili mbili za dhahabu kwa ajili ya mikono yake zenye uzito wa shekeli kumi,
23 Kisha akamuuliza, “Wewe ni binti wa nani? Tafadhali uniambie, je, kuna nafasi katika nyumba ya baba yako tutakapoweza kulala?”
akamuuliza, “wewe ni binti wa nani? Niambie tafadhali, Je kuna nafasi nyumbani mwa baba yako kwa ajili yetu kupumzika usiku?”
24 Yule msichana akamjibu, “Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka aliyemzalia Nahori.”
Akamwambia, “Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, ambaye alimzaa kwa Nahori.”
25 Akaendelea kusema, “Kwetu kuna majani mengi na malisho, tena kuna nafasi kwa ajili yenu kulala.”
Akasema pia, “Tunayo malisho tele na chakula, na iko nafasi kwa ajili yako kulala usiku.”
26 Yule mtumishi akasujudu na kumwabudu Bwana,
Kisha yume mtu akainama chini na kumwabudu Yahwe.
27 akisema, “Atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hakuondoa wema na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mimi nami, Bwana ameniongoza safarini akanifikisha nyumbani kwa jamaa za bwana wangu.”
Akasema, “Abarikiwe Yahwe, Mungu wa bwana wangu Abraham, ambaye hakuacha agano lake la uaminifu na kweli yake mbele ya bwana wangu. Kwa vile Yahwe ameniongoza moja kwa moja kwenye nyumba ya ndugu zake bwana wangu.”
28 Yule msichana akakimbia akawaeleza watu wa nyumbani mwa mama yake kuhusu mambo haya.
Kisha yule msichana akakimbia na kwenda kuwaeleza watu wa nyumba ya mama yake juu ya mambo yote haya.
29 Rebeka alikuwa na kaka aliyeitwa Labani, huyo akaharakisha kukutana na yule mtumishi kule kisimani.
Na sasa Rebeka alikuwa na kaka yake, jina lake aliitwa Labani. Labani akakimbia kwa yule mtu aliye kuwa nje barabarani karibu na kisima.
30 Mara alipoiona ile pete puani, na bangili mikononi mwa dada yake na kusikia yale maneno Rebeka aliyoambiwa na huyo mtumishi, alimwendea huyo mtumishi, akamkuta amesimama karibu na ngamia wake pale karibu na kisima.
Akisha kuona hereni ya puani pamoja na zile bangili kwenye mikono ya dada yake, na kusikia maneno ya Rebeka dada yake, “Hivi ndivyo yule mtu alicho niambia,” alikwenda kwa yule mtu, na, Tazama, alikuwa amesimama karibu na ngamia pale kisimani.
31 Akamwambia, “Karibu nyumbani wewe uliyebarikiwa na Bwana, kwa nini unasimama huko nje? Mimi nimekuandalia nyumba na mahali kwa ajili ya ngamia.”
Labani akasema, “Njoo, wewe uliye barikiwa na Yahwe. Kwa nini umesimama nje? nimekwisha andaa nyumba, pamoja na mahali kwa ajili ya ngamia.”
32 Hivyo yule mtumishi akaenda nyumbani, mizigo ikaondolewa juu ya ngamia. Majani na malisho yakaletwa kwa ajili ya ngamia na maji kwa ajili yake na watu wake ili kunawa miguu.
Kwa hiyo yule mtu akaingia ndani ya nyumba na akashusha mizigo kutoka kwa wale ngamia. Ngamia wakapatiwa malisho na chakula, na maji yakatolewa kuosha miguu yake pamoja na miguu ya wale watu aliokuwa pamoja nao.
33 Ndipo chakula kikaandaliwa kwa ajili yake, lakini akasema, “Sitakula mpaka niwe nimewaambia yale niliyo nayo ya kusema.” Labani akasema, “Basi tuambie.”
Wakaandaa chakula mbele yake ale, lakini akasema, “Sitakula mpaka niseme kile ninacho paswa kusema.” Kwa hiyo Labani akmwambia, “Sema.”
34 Hivyo akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu.
Akasema, “Mimi ni mtumwa wa Abraham.
35 Bwana amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ngʼombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda.
Yahwe amembariki sana bwana wangu na amekuwa mtu mkuu. Amempatia mifugo na makundi ya wanyama, fedha, dhahabu, watumwa wa kiume na watumwa wa kike, pamoja na ngamia na punda.
36 Sara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho.
Sara, mke wa bwana wangu, alimzalia mwana bwana wangu alipokuwa mzee, na amempatia mwanawe kila kitu anachomiliki.
37 Naye bwana wangu ameniapisha na akasema, ‘Kamwe usimtwalie mwanangu mke katika binti za Wakanaani, ambao ninaishi katika nchi yao,
Bwana wangu aliniapisha, akisema, “Usije ukampatia mwanangu mke kutoka kwa mabinti wa Wakanaani, ambao kwao nimefanya makazi.
38 ila uende mpaka kwa jamaa ya baba yangu na ukoo wangu mwenyewe, ukamtwalie mwanangu mke huko.’
Badala yake, lazima uende kwa familia ya baba yangu, na kwa ndugu zangu, na kupata mke kwa ajili ya mwanangu.'
39 “Kisha nikamuuliza bwana wangu, ‘Je, kama huyo mwanamke hatakubali kurudi nami?’
Nikamwambia bwana wangu, pengine mwanamke huyo asikubali kufuatana nami.'
40 “Akanijibu, ‘Bwana ambaye nimetembea mbele zake, atatuma malaika wake pamoja nawe, na kuifanikisha safari yako, ili uweze kupata mke kwa ajili ya mwanangu katika ukoo wangu na kutoka jamaa ya baba yangu.
Lakini akaniambia, Yahwe, ambaye ninakwenda mbele yake, atatuma malaika wake pamoja nawe na atakufanikisha njia yako, kwamba utapata mke kwa ajili ya mwangu kutoka miongoni mwa ndugu zangu na kutoka katika ukoo wa baba yangu.
41 Kisha, utakapokwenda kwenye ukoo wangu, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu hata kama wakikataa kukupa huyo binti, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu.’
Lakini utakuwa huru katika kiapo changu ikiwa utafika kwa ndugu zangu na wasikuruhusu kuja naye. Ndipo utakuwa huru katika kiapo changu.
42 “Nilipokuja kisimani leo nilisema, ‘Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ikikupendeza, naomba uifanikishe safari niliyoijia.
Hivyo nimefika leo kisimani, na nikasema, 'O Yahwe, Mungu wa bwana wangu Abraham, tafadhari, ikiwa kweli umekusudia kuifanya safari yangu kuwa yenye kufanikiwa -
43 Tazama, ninasimama kando ya kisima hiki, kama mwanamwali akija kuteka maji nami nikimwambia, tafadhali niruhusu ninywe maji kidogo kutoka kwenye mtungi wako,
tazama niko hapa nimesimama karibu na kisima cha maji - na iwe kwamba binti ajaye kuchota maji, nitakaye mwambia, “Tafadhari unipatie maji kidoka kutoka kwenye mtungi wako ninywe,” mwanamke atakaye niabia,
44 naye kama akiniambia, “Kunywa, nami nitateka maji kwa ajili ya ngamia wako pia,” basi huyo awe ndiye mke ambaye Bwana amemchagulia mwana wa bwana wangu.’
“Kunywa, na nitakuchotea pia maji kwa ajili ya ngamia wako” - na awe ndiye ambaye wewe Yahwe, umemchagulia mtoto wa bwana wangu.”
45 “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, Rebeka akatokea, amebeba mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka maji, nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ninywe.’
Ikawa hata kabla sijamaliza kuzungumza moyoni mwangu, Tazama, Rebeka akaja na mtungi wake juu ya bega lake akashuka chini kisimani akachota maji. Hivyo nikamwambia, 'Tafadhari nipatie maji ninywe.'
46 “Akafanya haraka kushusha mtungi wake begani na kusema, ‘Kunywa na nitawanywesha ngamia wako pia,’ basi nikanywa, akawanywesha na ngamia pia.
Ndipo kwa haraka alipoushusha mtungi wake begani mwake na akasema, 'Kunywa, na pia nitawapatia maji ngamia wak.' Kwa hiyo nikanywa, na akawanywesha ngamia pia.
47 “Nikamuuliza, ‘Wewe ni binti wa nani?’ “Akasema, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia.’ “Ndipo nilipotia pete puani mwake na bangili mikononi mwake,
Nikamuuliza na kusema, 'Wewe ni binti wa nani?' Akasema, 'Binti wa Bethueli, Mwana wa Nahori, ambaye Milka alizaa kwake.' Kisha nikamwekea pete puani mwake pamoja na bangili mikononi mwake.
48 nikasujudu na nikamwabudu Bwana. Nikamtukuza Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake.
Kisha nikainama chini nikamwabudu Yahwe, na kumbariki Yahwe, Mungu wa bwana wangu Abraham, ambaye ameniongoza katika njia sahihi kumpata binti wa ndugu za bwana wangu kwa ajili ya mwanawe.
49 Ikiwa mtaonyesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie, la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.”
Kwa hiyo, ikiwa mko tayari kumfanyia rehema na kweli, niambieni. Lakini kama sivyo, niambieni, ili kwamba niweze kwenda upande wa kulia, au kushoto.”
50 Labani na Bethueli wakajibu, “Jambo hili limetoka kwa Bwana, hatuwezi kukuambia jambo lolote baya au jema.
Ndipo Labani na Bethueli wakajibu na kusema, “Jambo hili limetoka kwa Yahwe; hatuwezi kusema kwako aidha neno baya au zuri.
51 Rebeka yuko hapa, mchukue na uende, awe mke wa mwana wa bwana wako, sawasawa na Bwana alivyoongoza.”
Tazama, Rebeka yu mbele yako. Mchukue na uende, ili awe mke wa mtoto wa bwana wako, kama Yahwe alivyosema.”
52 Ikawa huyo mtumishi wa Abrahamu aliposikia waliyosema, alisujudu mpaka nchi mbele za Bwana.
Mtumwa wa Abraham aliposikia maneno yao, akainama mwenyewe chini ardhini kwa Yahwe.
53 Ndipo huyo mtumishi akatoa vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu na kwa fedha pamoja na mavazi, akampa Rebeka, pia akawapa zawadi za thamani kubwa nduguye na mamaye.
Mtumwa akaleta vipande vya fedha na vipande vya dhahabu, na nguo, akampatia Rebeka. Akampatia pia kaka yake na mama yake zawadi zenye thamani.
54 Kisha yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye wakala, wakanywa na kulala palepale. Walipoamka asubuhi, yule mtumishi, akasema, “Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”
Kisha yeye na watu aliokuwa nao wakala na kunywa. wakakaa pale mpaka usiku, na walipoamka asubuhi, akasema, Niruhusuni niende kwa bwana wangu.”
55 Lakini ndugu yake Rebeka pamoja na mama yake wakajibu, “Acha binti akae kwetu siku kumi au zaidi, ndipo mwondoke.”
Kaka yake na mama yake wakasema, mwache binti abaki nasi kwa siku chache zingine, angalau siku kumi. baada ya hapo anaweza kwenda.”
56 Lakini yule mtumishi akawaambia, “Msinicheleweshe, kwa kuwa Bwana amefanikisha safari yangu, nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”
Lakini akawambia, msinizuie, kwa kuwa Yahwe amefanikisha njia yangu. Niruhusuni niende kwa bwana wangu.”
57 Ndipo wakasema, “Acha tumwite huyo binti tumuulize, tusikie atakavyosema.”
Wakasema, “Tutamwita binti na kumuuliza.”
58 Kwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?” Akasema, “Nitakwenda.”
Kwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je utakwenda na mtu huyu?” Akajibu, “Nitakwenda.”
59 Hivyo wakamwaga ndugu yao Rebeka aondoke, pamoja na mjakazi wake, mtumishi wa Abrahamu na watu wake.
Kwa hiyo wakampeleka dada yao Rebeka, pamoja na watumishi wake wa kike, kwenda njiani pamoja na mtumishi wa Abraham na watu wake.
60 Wakambariki Rebeka, wakamwambia, “Ndugu yetu, uwe wewe kumi elfu, mara elfu nyingi, nao wazao wako wamiliki malango ya adui zao.”
Wakambarikia Rebeka, na wakamwambia, “Ndugu yetu, na uwe mama wa maelfu na wa makumi elfu, uzao wako upate kumiliki lango la wale wanao wachukia.”
61 Rebeka na vijakazi wake wakajiandaa, wakapanda ngamia zao wakafuatana na yule mtu. Hivyo yule mtumishi akamchukua Rebeka akaondoka.
Kisha Rebeka akasimama, yeye na watumishi wake kwa hesabu ya ngamia, na wakamfuata yule mtu. Hivyo watumishi wakamchukua Rebeka, na wakaenda zao.
62 Basi Isaki alikuwa ametoka Beer-Lahai-Roi, kwa kuwa alikuwa anaishi nchi ya Negebu.
Nyakati hizo Isaka alikuwa anakaa katika Negebu, na alikuwa tu amerejea kutoka Beerlahairoi.
63 Isaki akatoka kwenda shambani kutafakari wakati wa jioni, alipoinua macho yake, akaona ngamia wanakuja.
Isaka akaenda kutafakari shambani jioni. Alipotazama akaona, natazama, kulikuwa na ngamia wakija!
64 Rebeka pia akainua macho akamwona Isaki. Akashuka kutoka kwenye ngamia wake
Rebeka akatazama na alipomwona Isaka, akaruka kutoka kwenye ngamia.
65 na akamuuliza yule mtumishi, “Ni nani mtu yule aliye kule shambani anayekuja kutulaki?” Yule mtumishi akajibu, “Huyu ndiye bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake akajifunika.
Akamwambia mtumwa, “mtu huyo ni nani anaye tembea shambani akija kutupokea?” Mtumwa akasema, “Ni bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake akajifunika.
66 Kisha yule mtumishi akamweleza Isaki mambo yote aliyoyatenda.
Mtumwa akamwambia Isaka mambo yote ambayo amefanya.
67 Ndipo Isaki akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake, Isaki akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaki akampenda, akafarijika baada ya kifo cha mama yake.
Kisha Isaka akamleta katika hema ya Sara mama yake na akamchukua Rebeka, na akawa mke wake, na akampenda. Kwa hiyo Isaka akafarijika baada ya kifo cha mama yake.