< Mwanzo 23 >
1 Sara aliishi akawa na umri wa miaka mia na ishirini na saba.
Sara akaishi mika mia moja na ishirini na saba. Hii ndiyo ilikuwa ni miaka ya maisha ya Sara.
2 Sara akafa huko Kiriath-Arba (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani, Abrahamu akamwombolezea na kumlilia Sara.
Sara akafa katika Kiriathi Arba, ambayo ni Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abraham akaomboleza na kumlilia Sara.
3 Ndipo Abrahamu akainuka kutoka pale penye maiti ya mke wake. Akazungumza na Wahiti, akasema,
Kisha Abraham akainuka na kutoka kwa mkewe aliye kufa, akanena na watoto wa kiume wa Hethi, akisema,
4 “Mimi ni mpitaji na mgeni miongoni mwenu. Niuzieni sehemu ya ardhi yenu ili niweze kumzika maiti wangu.”
“Mimi ni mgeni kati yenu. Tafadhari nipatieni mahali pa kuzikia miongoni mwenu, ili kwamba niweze kuzika wafu wangu.”
5 Wahiti wakamjibu Abrahamu,
Wana wa Hethi wakamjibu Abraham, wakasema,
6 “Bwana, tusikilize. Wewe ni mtawala mkuu sana miongoni mwetu. Zika maiti wako katika kaburi unalolipenda kati ya makaburi yetu. Hakuna mtu wa kwetu atakayekuzuia kaburi lake ili kuzika maiti wako.”
“Tusikilize, bwana wangu. Wewe ni mwana wa Mungu miongoni mwetu. Zika wafu wako katika makaburi yetu utakayochagua. Hakuna miongoni mwetu atakaye kuzuilia kaburi lake, kwa ajili ya kuzikia wafu wako.”
7 Abrahamu akainuka na akasujudu mbele ya wenyeji wa nchi, yaani Wahiti.
Abraham akainuka na kusujudu chini kwa watu wa nchi ile, kwa wana wa Hethi.
8 Akawaambia, “Kama mnaniruhusu kumzika maiti wangu, basi nisikilizeni mkamsihi Efroni mwana wa Sohari kwa niaba yangu
Akawaambia, akisema, “ikiwa mmekubali mimi kuzika wafu wangu, ndipo nisikilizeni, msihini Efroni mwana wa Sohari kwa ajili yangu.
9 ili aniuzie pango la Makpela, lililo mali yake, nalo liko mwisho wa shamba lake. Mwambieni aniuzie kwa bei kamili atakayosema ili liwe mahali pangu pa kuzikia miongoni mwenu.”
Mwambieni aniuzie pango la Makpela, ambalo analimiliki, ambalo liko mwishoni mwa shamba lake. Kwa bei kamili aniuzie waziwazi mbele ya watu kama miliki ya kuzikia.”
10 Efroni Mhiti alikuwa ameketi miongoni mwa watu wake, akamjibu Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokuwepo katika lango la mji.
Efroni alikuwa ameketi miongoni mwa wana wa Hethi, hivyo Efroni Mhiti akamjibu Abraham alipowasikia wana wa Hethi, wote ambao walikuwa wamekuja langoni mwa mji wake, akasema,
11 “La hasha, bwana wangu, nisikilize, nakupa shamba, pia nakupa pango lililomo ndani yake. Nakupa mbele ya watu wangu. Uzike maiti wako.”
“Hapana, bwana wangu, nisikilize. Ninakupatia shamba na pango ambalo limo ndani yake. Ninakupatia mbele ya wana wa watu wangu. Ninakupatia uzike wafu wako.”
12 Abrahamu akasujudu tena, mbele ya wenyeji wa nchi,
Kisha Abraham akasujudu chini mbele ya watu wa nchi ile.
13 akamwambia Efroni wale watu wakiwa wanasikia, “Tafadhali nisikilize. Nitakulipa fedha za hilo shamba. Kubali kuzipokea ili niweze kumzika maiti wangu.”
Akamwambia Efroni watu wa nchi ile wakisikiliza, akasema, ikiwa uko radhi, tafadhari nisikilize. Nitalipia shamba. Chukua fedha kwangu, na nitazika wafu wangu pale.”
14 Efroni akamjibu Abrahamu,
Efroni akamjibu Abraham, akisema,
15 “Nisikilize, bwana wangu, thamani ya ardhi hiyo ni shekeli 400 za fedha, lakini hiyo ni nini kati yako na mimi? Mzike maiti wako.”
“Tafadhari bwana wangu, nisikilize. Kipande cha ardhi kinathamani ya shekeli mia nne za fedha, na hiyo ni kitu gani kati yangu mimi na wewe? wazike wafu wako.”
16 Abrahamu akakubali masharti ya Efroni, akampimia ile fedha aliyotaja masikioni mwa Wahiti: Shekeli 400 za fedha kulingana na viwango vya uzito vilivyokuwa vikitumika wakati huo na wafanyabiashara.
Abraham akamsikiliza Efroni na akampimia Efroni kiwango cha fedha alizosema mbele ya wana wa Helthi wakisikiliza, shekeli mia nne za fedha, kwa mujibu wa viwango vya vipimo vya kibiashara.
17 Hivyo shamba la Efroni huko Makpela karibu na Mamre, yaani shamba pamoja na pango lililokuwamo, nayo miti yote iliyokuwamo ndani ya mipaka ya shamba hilo, vilikabidhiwa,
Kwa hiyo shamba la Efroni, lililokuwa katika Makpela, mbele ya Mamre, shamba pamoja na pango lililokuwamo ndani yake na miti yote iliyokuwamo ndani ya shamba na iliyokuwa mpakani ikatolewa
18 kwa Abrahamu kuwa mali yake mbele ya Wahiti wote waliokuwa wamekuja kwenye lango la mji.
kwa Abraham kwa njia ya manunuzi mbele ya wana wa Hethi, na mbele ya wote waliokuja malangoni pa mji wake.
19 Baada ya hayo Abrahamu akamzika Sara mkewe kwenye pango ndani ya shamba la Makpela karibu na Mamre (huko Hebroni) katika nchi ya Kanaani.
Baada ya haya, Abraham akamzika Sara mkewe katika pango la shamba la Makpela, lililo mbele ya Mamre, ambayo ni Hebroni, katika nchi ya Kanaani.
20 Hivyo Wahiti wakamkabidhi Abrahamu shamba pamoja na pango lililokuwa humo kuwa mahali pa kuzikia.
Kwa hiyo shamba pamoja na pango likatolewa na wana wa Hethi kwa Abraham kama milki na eneo la kuzikia.