< Mwanzo 21 >

1 Wakati huu Bwana akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, naye Bwana akamtendea Sara kile alichokuwa ameahidi.
Yahwe akamsikiliza Sara kwa umakini kama alivyo kuwa amemwambia, Yahwe akamfanyia Sara kama alivyo kuwa amemwahidi.
2 Sara akapata mimba, akamzalia Abrahamu mwana katika uzee wake, majira yale ya Mungu aliomwahidi.
Sara akachukua mimba na akamzalia Abraham mtoto wa kiume katika uzee wake, katika muda ule ule ambao Mungu alikuwa amemwambia.
3 Abrahamu akamwita Isaki yule mwana ambaye Sara alimzalia.
Abraham akamwita jina mwanawe, ambaye alizaliwa kwake, na Sara, Isaka.
4 Isaki alipokuwa na umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru.
Abraham akamtahiri mwanawe Isaka alipofikisha siku nane, kama vile Mungu alivyokuwa amemwagiza.
5 Abrahamu alikuwa na miaka 100 wakati Isaki mwanawe alipozaliwa.
Abraham alikuwa na umri wa miaka mia moja wakati mwanawe Isaka anazaliwa kwake.
6 Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.”
Sara akasema, “Mungu amenifanya nicheke; kila mtu atakaye sikia atacheka pamoja na nami.”
7 Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Abrahamu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Tena nimemzalia mwana katika uzee wake.”
Pia akasema, “Nani angesema kwa Abraham kwamba Sara atalea mtoto, na sasa kweli nimemzalia mtoto wakiume katika uzee wake!”
8 Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya. Siku hiyo Isaki alipoachishwa kunyonya, Abrahamu alifanya sherehe kubwa.
Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya, na Abraham akafanya sherehe kubwa katika siku ambayo Isaka aliachishwa.
9 Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hagari, Mmisri, aliyemzalia Abrahamu alikuwa anadhihaki,
Sara akamwona mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alikuwa amezaliwa kwa Abraham, akidhihaki.
10 Sara akamwambia Abrahamu, “Mwondoe mwanamke huyo mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwanangu Isaki.”
Kwa hiyo akamwambia Abraham, “Mfukuze huyu mwanamke huyu mtumwa pamoja na mtoto wake: kwa kuwa mtoto huyu wa mwanamke mtumwa hawezi kuwa mrithi pamoja na mwanangu Isaka.”
11 Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa sababu lilimhusu mwanawe.
Jambo hili likamuhuzunisha sana Abraham kwa sababu ya mwanawe.
12 Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana na mtumishi wako wa kike. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaki.
Lakini Mungu akamwambia Abraham, “Usihuzunike kwa sababu ya kijana huyu, na kwa sababu ya mwanamke huyu mtumwa wako. Sikiliza maneno asemayo Sara juu ya jambo hili, kwa sababu itakuwa kupitia Isaka kwamba uzao wako utaitwa.
13 Nitamfanya huyu mwana wa mtumishi wako wa kike kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”
Nitamfanya pia mtoto wa mjakazi kuwa taifa, kwa sababu ni uzao wako.”
14 Kesho yake asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari. Akaviweka mabegani mwa Hagari, akamwondoa pamoja na kijana. Hagari akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.
Abraham akaamka asubuhi na mapema, akachukua mkate na kiriba cha maji, akampatia Hajiri, akiweka juu ya bega lake. Akamtoa kijana akampatia Hajiri na akawaondoa. Hajiri akaondoka akapotea katika jangwa la Beerisheba.
15 Maji yalipokwisha kwenye kiriba, akamwacha kijana chini ya mojawapo ya vichaka.
Maji yalipokwisha kwenye kiriba akamtelekeza kijana katika moja ya vichaka.
16 Kisha akajiendea zake akaketi karibu, umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Ikawa alipokuwa ameketi pale karibu, akaanza kulia kwa huzuni.
Kisha akaondoka, na akakaa umbali kidogo na yule kijana, umbali kama wa kutupa mshale, kwa vile alisema, “Na nisitazame kifo cha mtoto.” Alipokuwa amekaa kumkabili, akapaza sauti yake akalia.
17 Mungu akamsikia kijana akilia, malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini Hagari? Usiogope, Mungu amesikia kijana analia akiwa amelala pale.
Mungu akasikia kilio cha kijana, na malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, “Nini kinakusumbua? Usiogope, kwa kuwa Mungu amesikia kilio cha kijana mahali alipo.
18 Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”
Inuka msimamishe mtoto, na umtie moyo; kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.”
19 Ndipo Mungu akamfumbua Hagari macho yake naye akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.
Kisha Mungu akayafunua macho ya Hajiri, natazama akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, na akampatia kijana akanywa.
20 Mungu akawa pamoja na huyu kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde.
Mungu akawa pamoja na kijana, na akakua. Akaishi jangwani akawa mwindaji.
21 Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akampatia mke kutoka Misri.
Akaishi katka jangwa la Parani, na mama yake akampatia mke kutoka Misri.
22 Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Abrahamu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya.
Ikawa kwamba katika wakati ule Abimeleki na Fikoli kamanda wa jeshi lake akamwambia Abraham, akisema, “Mungu yuko pamoja na wewe katika yote uyatendayo.
23 Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”
Sasa niapie kwa Mungu kwamba hutanifanyia baya, wala mwanangu, wala uzao wangu. Onesha kwangu na kwa nchi ambayo umekuwa ukikaa agano lile lile la uaminifu ambalo nimekuonesha wewe.”
24 Abrahamu akasema, “Ninaapa hivyo.”
Abraham akasema, “Nina apa.”
25 Ndipo Abrahamu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamekinyangʼanya.
Abraham pia akamlalamikia Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki wamekinyang'anya.
26 Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ambaye amefanya hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”
Abimeleki akasema, “Sijui ni nani amefanya jambo hili. Hukuniambia mapema; na sijalisikia ila leo hii.”
27 Hivyo Abrahamu akaleta kondoo na ngʼombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano.
Kwa hiyo Abraham akachukua kondoo na ng'ombe maksai akampatia Abimeleki, na wawili hawa wakafanya agano.
28 Abrahamu akatenga kondoo wa kike saba kutoka kwenye kundi,
Kisha Abraham akatenga wanakondoo wa kike saba pekeyao.
29 Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ni nini maana ya hawa kondoo wa kike saba uliowatenga peke yao?”
Abimeleki akamwambia Abraham, “Nini maana ya hawa wanakondoo wa kike saba ambao umewatenga pekeyao?”
30 Abrahamu akamjibu, “Upokee hawa kondoo wa kike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”
Akajibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba utawapokea kutoka mkonono mwangu, ili kwamba uwe ushahidi kwangu, kuwa nichimba kisima hiki.”
31 Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu wawili waliapiana hapo.
Kwa hiyo akaita mahali pale Beerisheba, kwa sababu mahali pale wote wawili wali apa kiapo.
32 Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi katika nchi ya Wafilisti.
Walifanya agano hapo Bersheba, kisha Abimeleki na Fikoli, amiri wa jeshi, wakarudi katika nchi ya Wafilisti.
33 Abrahamu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Bwana, Mungu wa milele.
Abraham akapanda mti wa mkwaju katika Beerisheba. Na pale akamwabudu Yahwe, Mungu wa milele.
34 Naye Abrahamu akakaa katika nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.
Abraham akasalia kuwa mgeni katika nchi ya Wafilisti kwa siku nyingi.

< Mwanzo 21 >