< Mwanzo 17 >

1 Abramu alipokuwa na miaka tisini na tisa, Bwana akamtokea akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi; enenda mbele zangu na uishi kwa unyofu.
Wakati Abram alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Yahwe alimtokea Abram na akamwambia, “Mimi ni Mungu wa uwezo. Uende mbele yangu, na uwe mkamilifu.
2 Nami nitafanya Agano langu kati yangu na wewe, nami nitakuzidisha sana sana.”
Kisha nitalithibitisha agano langu kati yangu mimi na wewe, na nitakuzidisha sana.
3 Abramu akaanguka kifudifudi, naye Mungu akamwambia,
Abram akainama uso wake hadi chini ardhini na Mungu akazungumza naye, akisema,
4 “Kwa upande wangu, hili ndilo Agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi.
“Mimi, tazama, agano langu liko nawe. Utakuwa baba wa mataifa mengi.
5 Jina lako hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Abrahamu, kwa maana nimekufanya wewe baba wa mataifa mengi.
Wala jina lako halitakuwa tena Abram, bali jina lako litakuwa Abraham - kwa kuwa ninakuchagua kuwa baba wa mataifa mengi.
6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, kwako yatatoka mataifa nao wafalme watatoka kwako.
Nitakufanya uwe na uzao mwingi zaidi, na nitakufanya mataifa, na wafalme watatoka kwako.
7 Nitalithibitisha Agano langu kama Agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo niwe Mungu wako na Mungu wa wazao wako.
Nitaimarisha agao langu kati yangu mimi na wewe na uzao wako baada yako, katika vizazi vyao vyote kwa agano la milele, nitakuwa Mungu kwako na kwa wazao wako baada yako.
8 Nchi yote ya Kanaani, unakoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na uzao wako, nami nitakuwa Mungu wao.”
Nitakupa wewe, na wazao wako baada yako, nchi ambayo ulikuwa unaishi, nchi yote ya Kanaani, kuwa miliki ya milele, na nitakuwa Mungu wao.”
9 Ndipo Mungu akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wako, lazima ushike Agano langu, wewe na wazao wako kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kisha Mungu akamwambia Abraham, “nawe lazima ulishike agano langu, wewe pamoja na uzao wako baada yako kwa vizazi vyao.
10 Hili ni Agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, Agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa.
Hili ndilo agano langu, ambalo utalishika, kati yangu na wewe na wazao wako baada yako: Kila mwanaume wa kwenu lazima atahiriwe.
11 Mtafanyiwa tohara na hii itakuwa ni alama ya Agano kati yangu na ninyi.
Lazima mtatahiriwa katika nyama ya govi la ngozi ya mbele, na hii itakuwa ishara ya agano kati yangu mimi na ninyi.
12 Kwa vizazi vijavyo, kila mwanaume miongoni mwenu mwenye siku nane ni lazima atahiriwe, pamoja na watakaozaliwa nyumbani mwako au walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, wale ambao sio watoto wako.
Kila mwanaume wa kwenu aliye na umri wa siku nane lazima atahiriwe, katika vizazi ya watu wenu. Hii ni pamoja na yule azaliwaye katika nyumba yako na yeye ambaye amenunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni yeyote ambaye si mmoja wa wazao wako.
13 Awe amezaliwa nyumbani mwako au amenunuliwa kwa fedha yako, ni lazima watahiriwe. Agano langu katika mwili wako litakuwa ni Agano la milele.
Mtu ambaye amezaliwa katika nyumba yako na yule aliye nunuliwa kwa fedha yako lazima atahiriwe. Hivyo agano langu litakuwa katika mwili wenu kuwa agano la milele.
14 Kila mwanaume asiyetahiriwa, ambaye hajapata tohara ya mwilini, atatengwa na watu wake, amelivunja Agano langu.”
Mwanaume yeyote asiye tahiriwa katika mwili govi la ngozi yake ya mbele atatengwa na watu wake. Amevunja agano langu.”
15 Pia Bwana akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wa Sarai mkeo, hutamwita tena Sarai bali jina lake litakuwa Sara.
Mungu akamwambia Abraham, “kwa habari ya Sarai mkeo, usimuite tena Sarai. Badala yake jina lake litakuwa Sara.
16 Nitambariki na hakika nitakupatia mwana kwake. Nitambariki na kwamba atakuwa mama wa mataifa, wafalme wa mataifa watatoka kwake.”
Nitambariki, na nitakupatia mtoto wa kiume kwake. Nitambariki, na atakuwa mama wa mataifa. Wafalme wa watu wa mataifa watapatikana kutokana na yeye.
17 Abrahamu akaanguka kifudifudi, akacheka na kusema moyoni mwake, “Je, mtu wa miaka mia moja aweza kuzaa mwana? Je, Sara atazaa mtoto katika umri wa miaka tisini?”
Kisha Abraham akainama uso wake hadi ardhini, na akacheka, akasema moyoni mwake, Je yawezekana mtoto azaliwe kwa mwanaume ambaye ana umri wa miaka miamoja? na Je Sara, ambaye ana umri wa miaka tisini anaweza kuzaa mwana?”
18 Abrahamu akamwambia Mungu, “Laiti Ishmaeli naye angeshiriki baraka yako!”
Abraham akamwambia Mungu, “Lau Ishmaeli angeweza kuishi kabla yako!”
19 Ndipo Mungu akasema, “Ndiyo, lakini mkeo Sara atakuzalia wewe mwana, nawe utamwita jina lake Isaki. Nitalithibitisha Agano langu naye kama Agano la milele kwa ajili yake na wazao wake baada yake.
Mungu akasema, Hapana, Sarai mkeo atakuzalia mtoto wa kiume na utamwita jina lake Isaka. Nita imarisha agano langu na yeye kama agano la milele pamoja na uzao wake baada yake.
20 Kwa upande wa Ishmaeli, nimekusikia: hakika nitambariki, nitamfanya awe na uzao mwingi na nitaongeza sana idadi yake. Atakuwa baba wa watawala kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kubwa.
Na kwa habari ya Ishmaeli nimekusikia. Tazama, ninambariki, na nitamfanya kuwa na uzao na kumzidisha maradufu. Atakuwa baba wa viongozi kumi na mbili wa makabila, na nitamfanya kuwa taifa kuu.
21 Lakini Agano langu nitalithibitisha kwa Isaki, ambaye Sara atakuzalia mwaka ujao majira kama haya.”
Lakini agano langu nitalifanya imara na Isaka, ambaye Sarai atazaa kwako majira haya mwakani.”
22 Wakati alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, Mungu akapanda juu akaondoka kwa Abrahamu.
Alipo kuwa amemaliza kuzungumza naye, Mungu akaondoka kwa Abraham.
23 Siku ile ile, Abrahamu akamchukua Ishmaeli mwanawe na wote waliozaliwa nyumbani mwake pamoja na walionunuliwa kwa fedha zake, kila mwanaume wa nyumbani mwake, akawatahiri, kama Mungu alivyomwagiza.
Kisha Abraham akamtwaa Ishmaeli mwanawe, na wote ambao walizaliwa katika nyumba yake, na wote ambao walinunuliwa kwa fedha yake, kila mwanaume miongoni mwa watu wa nyumba ya Abraham, walitahiriwa mwili wa magovi ya ngozi ya mbele katika siku iyo hiyo, kama Mungu alivyo kuwa amesema.
24 Abrahamu alikuwa na umri wa miaka tisini na tisa alipotahiriwa,
Abraham alikuwa na umri wa miaka tisini na tisa alipotahiriwa katika mwili wa govi la ngozi yake ya mbele.
25 naye Ishmaeli mwanawe alitahiriwa akiwa na umri wa miaka kumi na mitatu.
Na Ishmaeli mwanawe alikuwa na umri wa miaka kumi na tatu alipotahiriwa katika mwili wa govi la ngozi yake ya mbele.
26 Abrahamu na Ishmaeli mwanawe walitahiriwa siku ile ile,
Siku ile ile ambayo wote wawili Abraham na Ishmael mwanawe walipotahiriwa, ndipo
27 Kila mwanaume nyumbani mwa Abrahamu, pamoja na wote waliozaliwa nyumbani mwake au aliyenunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, alitahiriwa pamoja naye.
wanaume wote wa nyumba yake walitahiriwa pia, hawa ni pamoja na wale waliozaliwa katika nyumba ile na wale walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni.

< Mwanzo 17 >