< Mwanzo 13 >
1 Hivyo Abramu akakwea kutoka Misri kwenda Negebu, yeye na mkewe na kila kitu alichokuwa nacho, pia Loti akaenda pamoja naye.
Kwa hiyo Abram akaondoka akatoka Misri na akaenda Negebu, Yeye, mke wake, na vyote alivyokuwa navyo. Lutu pia akaenda pamoja naye.
2 Wakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu.
Na sasa Abram alikuwa tajiri wa mifugo, fedha na dhahabu.
3 Kutoka Negebu, akapita mahali hadi mahali, hadi akafika Betheli, mahali hapo ambapo mwanzoni alipiga hema lake kati ya Betheli na Ai
Aliendelea na safari yake kutoka Negebu hadi Betheli, mahali ambapo hema yake ilikuwa tangu mwanzo, kati ya Betheli na mji wa Ai.
4 hapo ambapo alikuwa amejenga madhabahu ya kwanza. Huko Abramu akaliitia jina la Bwana.
Akaenda mahali ambapo madhabahu ilikuwa imejengwa mwanzoni. Hapa akaliitia jina la Yahwe.
5 Basi Loti, ambaye alikuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na makundi ya mbuzi, kondoo, ngʼombe na mahema.
aliyekuwa anasafiri na Abram, alikuwa pia na ngo'mbe, makundi ya mifugo, na mahema.
6 Lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali zao.
Nchi haikuwatosha wote kukaa pamoja karibu kwa sababu mali zao zilikuwa nyingi sana, kiasi kwamba hawakuweza kukaa pamoja.
7 Ukazuka ugomvi kati ya wachunga mifugo wa Abramu na wale wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo.
Pia, kulikuwa na ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abram na wachunga wanyama wa Lutu. Wakanaani pamoja na Waperizi walikuwa wakiishi katika nchi ile wakati huo.
8 Hivyo Abramu akamwambia Loti, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu.
Kwa hiyo Abram akamwambia Lutu, “Pasiwe na ugomvi kati yako na mimi, na kati ya wachunga wanyama wako na wachunga wanyama wangu; licha ya hayo sisi ni familia.
9 Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Kama ukielekea kushoto, nitakwenda kulia; kama ukielekea kulia, mimi nitakwenda kushoto.”
Je nchi hii yote haiko mbele yako? Nenda na ujitenge na mi. Ikiwa utakwenda kushoto, mimi nitakwenda kulia. au ikiwa utakwenda kulia, mimi nitakwenda kushoto.”
10 Loti akatazama akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora.)
Kwa hiyo Lutu akatazama, na akaona kuwa nchi yote tambarare ya Yorodani ilikuwa na maji kila mahali hadi Zoari, kama vile bustani ya Yahwe, na kama nchi ya Misri. Hii ilikuwa ni kabla Yahwe hajaiangamiza Sodoma na Gomora.
11 Hivyo Loti akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana:
Kwa hiyo Lutu akajichagulia yeye mwenyewe nchi tambarare ya Yorodani na akasafiri mashariki, na ndugu hawa wakatengana wao kwa wao.
12 Abramu akaishi katika nchi ya Kanaani, wakati Loti aliishi miongoni mwa miji ya lile bonde na kupiga mahema yake karibu na Sodoma.
Abram akaishi katika nchi ya Kanaani, na Lutu akaishi katika miji ya tambarare. Akatandaza hema zake hadi Sodoma.
13 Basi watu wa Sodoma walikuwa waovu, wakifanya sana dhambi dhidi ya Bwana.
Na sasa watu wa Sodoma walikuwa waovu na wenye dhambi nyingi dhidi ya Yahwe.
14 Baada ya Loti kuondoka Bwana akamwambia Abramu, “Ukiwa hapo ulipo, inua macho yako utazame kaskazini na kusini, mashariki na magharibi.
Yahwe akamwambia Abram baada ya Lutu kuondoka kwake, “Angalia kuanzia mahali ulipo simama hadi kaskazini, kusini, mashariki, na magharibi.
15 Nchi yote unayoiona nitakupa wewe na uzao wako hata milele.
Nchi yote hii uionayo, nitakupatia wewe pamoja na uzao wako milele.
16 Nitaufanya uzao wako uwe mwingi kama mavumbi ya nchi, hivyo kama kuna yeyote awezaye kuhesabu mavumbi, basi uzao wako utahesabika.
Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama mavumbi ya nchi, kiasi kwamba kama kuna mtu anaweza kuhesabu mavumbi ya nchi, ndipo na uzao wako pia utahesabika.
17 Ondoka, tembea katika marefu na mapana ya nchi, kwa maana ninakupa wewe.”
Inuka, tembea katika urefu na upana wa nchi hii, kwa kuwa nitakupatia.”
18 Basi Abramu akaondoa mahema yake, akaenda kuishi karibu na mialoni ya Mamre huko Hebroni, huko akamjengea Bwana madhabahu.
Kwa hiyo Abram akachukua hema yake, akaja na kukaa katika mwaloni wa Mamre, ambao uko Hebroni, na pale akajenga Madhabahu ya Yahwe.