+ Mwanzo 1 >

1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.
Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na nchi.
2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.
Nayo nchi haikuwa na umbo na ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji. Roho wa Mungu alikuwa akielea juu ya uso wa maji.
3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo.
Mungu akasema, “na kuwe nuru,” na kulikuwa na nuru.
4 Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza.
Mungu akaona nuru kuwa ni njema. Akaigawa nuru na giza.
5 Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.
Mungu akaiita nuru “mchana” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni na asubuhi, siku ya kwanza.
6 Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.”
Mungu akasema, “na kuwe na anga kati ya maji, na ligawe maji na maji.”
7 Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo.
Mungu akafanya anga na kugawanya maji yaliyo kuwa chini ya anga na maji ambayo yalikuwa juu ya anga. Ikawa hivyo.
8 Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.
Mungu akaita anga “mbingu.” Ikawa jioni na asubuhi siku ya pili.
9 Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo.
Mungu akasema, “maji yaliyo chini ya mbingu yakusanyike pamoja mahali pamoja, na ardhi kavu ionekane.” Ikawa hivyo.
10 Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.
Mungu aliita ardhi kavu “nchi,” na maji yaliyo kusanyika akayaita “bahari.” Akaona kuwa ni vyema.
11 Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo.
Mungu akasema, nchi ichipushe mimea: miche itoayo mbegu na miti ya matunda itoayo matunda ambayo mbegu yake imo ndani ya tunda, kila kitu kwa namna yake.” Ikawa hivyo.
12 Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema.
Nchi ikatoa mimea, miche itoayo mbegu ya aina yake, na miti itoayo tunda ambalo mbegu yake imo ndani yake, kwa aina yake. Mungu akaona kuwa ni vyema.
13 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.
Ikawa jioni na asubuhi, siku ya tatu.
14 Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka,
Mungu akasema, “kuwe na mianga katika anga kutenganisha mchana na usiku. Na ziwe kama ishara, kwa majira, kwa siku na miaka.
15 nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo.
Ziwe mianga katika anga ili kutoa mwanga juu ya nchi.” Ikawa hivyo.
16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota.
Mungu akafanya mianga mikuu miwili, mwanga mkuu zaidi kutawala mchana, na mwanga mdogo kutawala usiku. Akafanya nyota pia.
17 Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia,
Mungu akazipanga katika anga kutoa mwanga juu nchi,
18 itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
kutawala mchana na usiku, na kugawanya mwanga kutoka kwenye giza. Mungu akaona kuwa ni vyema.
19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.
Ikawa jioni na asubuhi, siku ya nne.
20 Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.”
Mungu akasema, “maji yajae idadi kubwa ya viumbe hai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu.”
21 Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini, pamoja na kila kiumbe hai cha aina yake, viumbe waendao na wanaojaa kila mahali majini, na kila ndege mwenye mabawa kwa aina yake. Mungu akaona kuwa ni vyema.
22 Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.”
Mungu akavibariki, akisema, “zaeni na muongezeke, na mjae majini katika bahari. Ndege waongezeke juu nchi.”
23 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.
Ikawa jioni na asubuhi, siku ya tano.
24 Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo.
Mungu akasema, “nchi na itoe viumbe hai, kila kiumbe kwa aina yake, mnyama wa kufugwa, vitu vitambaavyo, na wanyama wa nchi, kila kitu kwa jinsi yake.” Ikawa hivyo.
25 Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
Mungu akafanya wanyama wa nchi kwa aina yake, wanyama wa kufugwa kwa aina yake, na kila kitambaaho juu ya ardhi kwa aina yake. Akaona kuwani vyema.
26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”
Mung akasema, “na tumfanye mtu katika mfano wetu, wa kufanana na sisi. Wawe na mamlaka juu ya samaki wa bahari, juu ya ndege wa angani, juu ya wanyama wa kufuga, juu ya nchi yote, na juu ya kila kitu kitambaacho kinacho tambaa juu ya nchi.”
27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu alimuumba; mwanaume na mwanamke aliwaumba.
Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake. Katika mfano wake alimuumba. Mwanaume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”
Mungu akawabariki na akawaambia, “zaeni na kuongezeka. Jazeni nchi, na muitawale. Muwe na mamlaka juu ya samaki wa baharini, juu ya ndege wa angani, na juu ya kila kiumbe hai kiendacho juu ya nchi,”
29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu.
Mungu akasema, “tazama, nimewapeni kila mmea uzaao mbegu ambao uko juu ya nchi, na kila mti wenye tunda ambalo lina mbegu ndani yake. Vitakuwa ni chakula kwenu.
30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.
Kwa kila mnyama wa nchi, kwa kila ndege wa angani, na kila kitambaacho juu ya nchi, na kila kiumbe ambacho kina pumzi ya uhai ni metoa kila mmea kwa ajili ya chakula.” ikawa hivyo.
31 Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.
Mungu akaona kila kitu alichokiumba. Tazama, kikawa chema sana. Ikawa jioni na asubuhi siku ya sita.

+ Mwanzo 1 >