< Wagalatia 5 >

1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.
Kristo alitupa uhuru akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa.
2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote.
Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote.
3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote.
Nasema tena wazi: kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika Sheria yote.
4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu.
Kama mnatazamia kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu.
5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki.
Kwa upande wetu, lakini, sisi tunatumaini kwamba kwa nguvu ya Roho tunakubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani.
6 Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.
Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo.
7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli?
Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi aliyewazuia kuuzingatia ukweli?
8 Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita.
Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni.
9 “Chachu kidogo huchachua donge zima.”
“chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!”
10 Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani.
Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba ninyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni—awe nani au nani—hakika ataadhibiwa.
11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa.
Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote.
12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!
Laiti hao wanaowavurugeni wangejikatakata wenyewe!
13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo.
Ninyi, ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo.
14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”
Maana Sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”
15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.
Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe!
16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
Basi, nasema hivi: mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia.
17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.
Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya Roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka ninyi wenyewe.
18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.
Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya Sheria.
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi,
Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: uzinzi, uasherati, ufisadi;
20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano;
21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.
husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: watu wanaotenda mambo hayo hawatakuwa na nafasi yao katika ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu,
23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.
upole na kuwa na kiasi. Hakuna Sheria inayoweza kupinga mambo hayo.
24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake.
Wale walio wa Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho.
Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake.
26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.
Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.

< Wagalatia 5 >