< Wagalatia 2 >
1 Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito ili awe pamoja nami.
Baada ya miaka kumi na minne, nilikwenda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba; nilimchukua pia Tito pamoja nami.
2 Nilikwenda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure.
Kwenda kwangu kulitokana na ufunuo alionipa Mungu. Katika kikao cha faragha niliwaeleza hao viongozi ujumbe wa Habari Njema niliohubiri kwa watu wa mataifa. Nilifanya hivyo kusudi kazi yangu niliyokuwa nimefanya, na ile ninayofanya sasa isije ikawa bure.
3 Lakini hata Tito ambaye alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa.
Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa,
4 Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani,
ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa.
5 hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili kwamba ukweli wa Injili ubaki nanyi.
Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Habari Njema ubaki nanyi daima.
6 Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote.
Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi—kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje—watu hawa hawakuwa na kitu cha kuongeza katika Habari hii Njema kama niihubirivyo.
7 Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi.
Badala yake, walitambua kwamba Mungu alikuwa amenituma kuhubiri Habari Njema kwa watu wa mataifa mengine kama vile Petro alivyokuwa ametumwa kuihubiri kwa Wayahudi.
8 Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa.
Maana, yule aliyemwezesha Petro kuwa mtume kwa Wayahudi, ndiye aliyeniwezesha nami pia kuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine.
9 Basi, Yakobo, Kefa na Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupa mkono wa shirika, mimi na Barnaba walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa na wao waende kwa Wayahudi.
Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, ambao waonekana kuwa viongozi wakuu, walitambua kwamba Mungu alinijalia neema hiyo, wakatushika sisi mkono, yaani Barnaba na mimi, iwe ishara ya ushirikiano. Sisi ilitupasa tukafanye kazi kati ya watu wa mataifa mengine, na wao kati ya Wayahudi.
10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.
Wakatuomba lakini kitu kimoja: tuwakumbuke maskini; jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kutekeleza.
11 Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi.
Lakini Kefa alipofika Antiokia nilimpinga waziwazi maana alikuwa amekosea.
12 Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara.
Awali, kabla ya watu kadhaa waliokuwa wametumwa na Yakobo kuwasili hapo, Petro alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa mengine. Lakini, baada ya hao watu kufika, aliacha kabisa kula pamoja na watu wa mataifa mengine, kwa kuogopa kikundi cha waliosisitiza tohara.
13 Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.
Hata ndugu wengine Wayahudi walimuunga mkono Petro katika kitendo hiki cha unafiki, naye Barnaba akakumbwa na huo unafiki wao.
14 Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?
Basi, nilipoona kuwa msimamo wao kuhusu ukweli wa Habari Njema haukuwa umenyooka, nikamwambia Kefa mbele ya watu wote: “Ingawa wewe ni Myahudi, unaishi kama watu wa mataifa mengine na si kama Myahudi! Unawezaje, basi kujaribu kuwalazimisha watu wa mataifa mengine kuishi kama Wayahudi?”
15 “Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa,
Kweli, sisi kwa asili ni Wayahudi, na si watu wa mataifa mengine hao wenye dhambi!
16 bado tunajua ya kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.
Lakini, tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo. Na sisi pia tumemwamini Yesu Kristo ili tupate kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani yetu kwa Kristo, na si kwa kuitii Sheria.
17 “Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha!
Sasa, ikiwa katika kutafuta kukubaliwa kuwa waadilifu kwa kuungana na Kristo sisi tunaonekana kuwa wenye dhambi, je, jambo hili lina maana kwamba Kristo anasaidia utendaji wa dhambi? Hata kidogo!
18 Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonyesha kwamba mimi ni mkosaji.
Lakini ikiwa ninajenga tena kile nilichokwisha bomoa, basi nahakikisha kwamba mimi ni mhalifu.
19 Kwa maana mimi kwa njia ya sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu.
Maana, kuhusu Sheria hiyo, mimi nimekufa; Sheria yenyewe iliniua, nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani,
20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.
na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu.
21 Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure!”
Sipendi kuikataa neema ya Mungu. Kama mtu huweza kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya Sheria, basi, Kristo alikufa bure!