< Ezra 1 >
1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la Bwana lililosemwa na nabii Yeremia, Bwana aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi:
Katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Yahwe akatimiza neno lake ambalo Yeremia alisema, na kuinua roho ya Koreshi. Sauti ya Koreshi ikasambaa na kusikika katika ufalme wake. Hiki ndicho kilichoandikwa na kusemwa:
2 “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi: “‘Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda.
“Koreshi, mfalme wa Uajemi, anasema: Yahwe, Mungu wa mbinguni, amenipa mimi ufalme wote wa dunia, na ameniteua mimi kumjengea yeye nyumba katika Yerusalem ya Yuda.
3 Yeyote wa watu wake miongoni mwenu, Mungu wake na awe pamoja naye, wacha apande kwenda Yerusalemu katika Yuda na kujenga Hekalu la Bwana, Mungu wa Israeli, Mungu aliyeko huko Yerusalemu.
Yeyote katika watu wake (Mungu awe pamoja naye) anaweza kwenda Yerusalem na kujenga nyumba kwa ajili ya Yahwe, Mungu wa Israel, Mungu ambaye yuko Yerusalem.
4 Nao watu wa mahali popote wale walionusurika wanapoishi sasa, watu hao wampe fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, mbali na sadaka za hiari kwa ajili ya Hekalu la Mungu huko Yerusalemu.’”
Watu wa kila sehemu katika ufalme waliosalia katika nchi na kuishi wanapaswa kuwapa wao fedha na dhahabu, mali na wanyama, pamoja na kutoa kwa hiari kwenye nyumba ya Mungu Yerusalem.”
5 Kisha viongozi wa jamaa ya Yuda na Benyamini na makuhani na Walawi kila mmoja ambaye moyo wake ulisukumwa na Mungu, akajiandaa kupanda ili kuijenga nyumba ya Bwana huko Yerusalemu.
Ndipo wakuu wa jamii ya Yuda na Benjamini, makuhani na walawi, na kila mmoja ambaye Roho wa Mungu alimwinua kuondoka na kujenga nyumba yake alisimama.
6 Majirani zao wote wakawasaidia vyombo vya fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, pia na zawadi za thamani, pamoja na sadaka zote za hiari.
Wale waliowazunguka karibu waliwasaidia kwa kuwapa fedha na vitu vya dhahabu, mali, wanyama, vitu vya thamani, na kutoa kwa hiari.
7 Zaidi ya hayo, Mfalme Koreshi akavitoa vyombo vilivyokuwa mali ya Hekalu la Bwana, ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la mungu wake.
Mfalme Koreshi akarusu vitu ambavyo vilikuwa kwenye nyumba ya Yahwe, ambavyo Nebukadreza alitoa kutoka Yerusalem na kuviweka katika nyumba ya miungu yake.
8 Koreshi mfalme wa Uajemi akavitoa kwa mkono wa Mithredathi mtunza hazina, aliyevihesabu mbele ya Sheshbaza mkuu wa Yuda.
Koreshi akavikabidhi kwenye mikono ya Mithredathi mtunza fedha, ambaye akavitoa na kuhesabu kwa Sheshbaza, kiongozi wa Yuda
9 Hii ilikuwa ndio orodha ya vifaa: masinia ya dhahabu yalikuwa 30 masinia ya fedha yalikuwa 1,000 vyetezo vya fedha vilikuwa 29
Hii ilikuwa idadi yake: beseni thelathini za dhahabu, beseni elfu moja za fedha, beseni zingine ishirini na tisa,
10 mabakuli ya dhahabu yalikuwa 30 mabakuli ya fedha yanayofanana yalikuwa 410 vifaa vingine vilikuwa 1,000.
mabakuli thelathini ya dhahabu, mabakuli madogo ya fedha 410, na vitu elfu moja vya kuongezea.
11 Kwa ujumla, kulikuwa na vyombo 5,400 vya dhahabu na vya fedha. Sheshbaza akavileta hivi vyote wakati watu walipotoka uhamishoni Babeli kwenda Yerusalemu.
Kulikuwa na vitu 5, 400 vya fedha na dhahabu. Sheshbaza akavileta vyote wakati wa uhamisho kutoka Babeli kwenda Yerusalem.