< Ezra 9 >
1 Baada ya mambo haya kutendeka, viongozi walinijia na kusema, “Watu wa Israeli, wakiwemo makuhani na Walawi, hawakujitenga na majirani zao katika kufanya machukizo, kama yale ya Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi, Waamoni, Wamoabu, Wamisri na Waamori.
2 Wamewaoa baadhi ya binti zao kuwa wake zao na wake za wana wao, nao wamechanganya taifa takatifu na watu waliowazunguka. Nao viongozi na maafisa wamekuwa mstari wa mbele katika njia hii potovu.”
3 Niliposikia jambo hili nilirarua koti langu na joho langu, nikazingʼoa nywele za kichwa changu na ndevu zangu na kuketi nikishangaa.
4 Kisha kila mmoja aliyetetemeshwa na maneno ya Mungu wa Israeli alikusanyika kunizunguka kwa sababu ya upotovu huu wa hao watu waliorudi kutoka utumwani. Nami niliketi pale nikishangaa mpaka wakati wa dhabihu ya jioni.
5 Ndipo wakati wa kutoa dhabihu ya jioni nikainuka kutoka kujidhili kwangu nikiwa na koti na joho langu lililoraruka, nikapiga magoti mikono yangu ikiwa imeinuliwa kwa Bwana Mungu wangu.
6 Nami nikaomba: “Ee Mungu wangu, natahayari na kuona aibu kukuinulia uso wangu Mungu wangu, kwa sababu dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni.
7 Tokea siku za babu zetu mpaka sasa, hatia yetu imekuwa kubwa. Kwa sababu ya dhambi zetu, sisi na wafalme wetu na makuhani wetu tumekabiliwa na vita, utumwa, kutekwa na kudhiliwa katika mikono ya wafalme wa kigeni, kama ilivyo leo.
8 “Lakini sasa, kwa muda mfupi, Bwana Mungu wetu amekuwa na neema kwa kutuachia mabaki na kutupa mahali imara katika mahali pake patakatifu, hivyo Mungu wetu atupa mwanga machoni petu na unafuu katika utumwa wetu.
9 Ingawa tu watumwa, Mungu wetu hajatuacha katika kufungwa kwetu. Ametuonyesha huruma mbele ya wafalme wa Uajemi: Ametujalia maisha mapya kwa kujenga upya nyumba ya Mungu wetu na kukarabati magofu yake, naye ametupa ukuta wa ulinzi katika Yuda na Yerusalemu.
10 “Lakini sasa, Ee Mungu wetu, tunaweza kusema nini baada ya hili? Kwa maana tumedharau maagizo
11 uliyoyatoa kupitia watumishi wako manabii uliposema: ‘Nchi mnayoiingia kuimiliki ni nchi iliyochafuliwa na uovu wa watu wake. Kwa matendo yao ya machukizo wameijaza nchi kwa unajisi wao kutoka mwisho mmoja hadi mwingine.
12 Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wowote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’
13 “Yale yaliyotupata ni matokeo ya matendo yetu mabaya, pia hatia yetu kubwa. Hata hivyo, wewe Mungu wetu, umetuadhibu kidogo kuliko dhambi zetu zilivyostahili na umetupa mabaki kama haya.
14 Je, tutavunja maagizo yako tena na kuoana na watu ambao hufanya mambo ya machukizo? Je, hutakuwa na hasira ya kutosha juu yetu na kutuangamiza, bila kutuachia mabaki wala atakayenusurika?
15 Ee Bwana, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki! Leo hii tumeachwa kama mabaki. Tupo hapa mbele zako na hatia yetu, ingawa katika hali hii hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusimama mbele zako.”