< Ezra 4 >
1 Adui za Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanajenga Hekalu kwa ajili ya Bwana, Mungu wa Israeli,
2 wakamjia Zerubabeli na viongozi wa jamaa, nao wakasema, “Turuhusuni tuwasaidie kujenga, kwa sababu sisi tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi na tumekuwa tukimtolea dhabihu tangu wakati wa Esar-Hadoni mfalme wa Ashuru, aliyetuleta hapa.”
3 Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa jamaa ya Israeli wakawajibu, “Ninyi hamna sehemu nasi katika kujenga Hekalu la Mungu wetu. Sisi peke yetu tutajenga Hekalu kwa ajili ya Bwana, Mungu wa Israeli, kama Mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi alivyotuagiza.”
4 Ndipo watu waliowazunguka wakajipanga kuwakatisha tamaa watu wa Yuda na kuwafanya waogope walipokuwa wakiendelea na ujenzi.
5 Wakaajiri washauri kuwapinga katika kazi yao, nao wakaipinga mipango yao wakati wote wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi hadi wakati wa utawala wa Dario mfalme wa Uajemi.
6 Mnamo mwanzo wa utawala wa Ahasuero, hao adui waliandika mashtaka dhidi ya watu wa Yuda na Yerusalemu.
7 Pia katika siku za utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli pamoja na wenzao waliandika barua kwa Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa mwandiko wa Kiaramu na katika lugha ya Kiaramu.
8 Rehumu afisa msimamizi na mwandishi Shimshai waliandika barua kwa Mfalme Artashasta dhidi ya watu wa Yerusalemu kama ifuatavyo:
9 Rehumu afisa msimamizi na mwandishi Shimshai, pamoja na wenzao, yaani mahakimu na maafisa walio juu ya watu kuanzia Tripoli, Uajemi, Ereki na Babeli, Waelami wa Shushani,
10 na watu wengine ambao mheshimiwa Asur-Banipali aliwahamisha na kuwakalisha katika mji wa Samaria na mahali pengine Ngʼambo ya Mto Frati.
11 (Hii ndiyo nakala ya barua waliyompelekea.) Kwa Mfalme Artashasta, Kutoka kwa watumishi wako, watu wa Ngʼambo ya Mto Frati:
12 Yapasa Mfalme ajue kuwa Wayahudi waliopanda kuja kwetu kutoka kwenu, wamekwenda Yerusalemu nao wanaujenga upya ule mji wa uasi na uovu. Wanajenga kuta upya na kukarabati misingi yake.
13 Zaidi ya hayo, mfalme yampasa ajue kwamba kama mji huu ukijengwa na kuta zake zikafanywa upya, hakutakuwa na ulipaji wa kodi wala ada au ushuru, hivyo hazina za mfalme zitaathirika.
14 Sisi sasa kwa kuwa tunawajibika kwa jumba la kifalme na kwamba siyo sawasawa kwetu kuona mfalme akidharauliwa, basi tunatuma ujumbe huu kumtaarifu mfalme,
15 ili kwamba ufanyike uchunguzi kwenye kumbukumbu ya maandishi ya waliokutangulia. Katika kumbukumbu hizi utagundua kwamba mji huu ni wa maasi, unaowataabisha wafalme na majimbo, ni mahali pa maasi tangu zamani. Ndiyo maana mji huu uliharibiwa.
16 Tunamjulisha mfalme kwamba kama mji huu ukijengwa na kuta zake zikifanywa upya, hutabakiwa na chochote Ngʼambo ya Mto Frati.
17 Mfalme alirudisha jibu hili: Kwa Rehumu, afisa msimamizi, mwandishi Shimshai na wenzenu wote wanaoishi katika Samaria na penginepo Ngʼambo ya Mto Frati: Salamu.
18 Barua mliyotutumia imesomwa na kutafsiriwa mbele yangu.
19 Nilitoa amri na uchunguzi ukafanyika na imegundulika kwamba mji huu una historia ndefu ya maasi dhidi ya wafalme na pamekuwa mahali pa maasi na uchochezi.
20 Yerusalemu umepata kuwa na wafalme wenye nguvu wakitawala nchi yote iliyo Ngʼambo ya Mto Frati, wakitoza kodi, ada na ushuru huko.
21 Kwa hiyo toeni amri kwa watu hawa wasimamishe ujenzi, ili kwamba mji huu usiendelee kujengwa hadi nitakapoagiza.
22 Mwe waangalifu msipuuze jambo hili. Kwa nini kuruhusu tishio hili kuendelea na kusababisha hasara kwa ufalme?
23 Mara waliposomewa nakala ya barua ya Mfalme Artashasta, Rehumu na Shimshai aliyekuwa mwandishi na wenzao, walikwenda mara moja kwa Wayahudi huko Yerusalemu na kuwalazimisha kwa nguvu kusimamisha ujenzi.
24 Hivyo kazi ya ujenzi wa nyumba ya Mungu huko Yerusalemu ikasimamishwa kabisa hadi mwaka wa pili wa utawala wa Dario mfalme wa Uajemi.