< Ezra 1 >
1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la Bwana lililosemwa na nabii Yeremia, Bwana aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi:
2 “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi: “‘Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda.
3 Yeyote wa watu wake miongoni mwenu, Mungu wake na awe pamoja naye, wacha apande kwenda Yerusalemu katika Yuda na kujenga Hekalu la Bwana, Mungu wa Israeli, Mungu aliyeko huko Yerusalemu.
4 Nao watu wa mahali popote wale walionusurika wanapoishi sasa, watu hao wampe fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, mbali na sadaka za hiari kwa ajili ya Hekalu la Mungu huko Yerusalemu.’”
5 Kisha viongozi wa jamaa ya Yuda na Benyamini na makuhani na Walawi kila mmoja ambaye moyo wake ulisukumwa na Mungu, akajiandaa kupanda ili kuijenga nyumba ya Bwana huko Yerusalemu.
6 Majirani zao wote wakawasaidia vyombo vya fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, pia na zawadi za thamani, pamoja na sadaka zote za hiari.
7 Zaidi ya hayo, Mfalme Koreshi akavitoa vyombo vilivyokuwa mali ya Hekalu la Bwana, ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la mungu wake.
8 Koreshi mfalme wa Uajemi akavitoa kwa mkono wa Mithredathi mtunza hazina, aliyevihesabu mbele ya Sheshbaza mkuu wa Yuda.
9 Hii ilikuwa ndio orodha ya vifaa: masinia ya dhahabu yalikuwa 30 masinia ya fedha yalikuwa 1,000 vyetezo vya fedha vilikuwa 29
10 mabakuli ya dhahabu yalikuwa 30 mabakuli ya fedha yanayofanana yalikuwa 410 vifaa vingine vilikuwa 1,000.
11 Kwa ujumla, kulikuwa na vyombo 5,400 vya dhahabu na vya fedha. Sheshbaza akavileta hivi vyote wakati watu walipotoka uhamishoni Babeli kwenda Yerusalemu.