< Ezekieli 5 >

1 “Mwanadamu, sasa chukua upanga mkali na uutumie kama wembe wa kinyozi ili kunyolea nywele za kichwa chako na ndevu zako. Kisha uchukue mizani ya kupimia ukazigawanye nywele hizo.
“Kisha wewe mwana wa adamu, chukua upanga mkali kama wembe wa kinyozi kwa ajili yako mwenyewe, na pitisha hayo makali juu ya kichwa chako na ndevu zako, kisha chukua mizani za kupimia uzito na uzigawanye nywele zako.
2 Wakati siku zako za kuzingirwa zitakapokwisha, choma theluthi moja ya hizo nywele zako kwa moto ndani ya mji. Chukua theluthi nyingine ya hizo nywele uzipige kwa upanga kuuzunguka mji wote na theluthi nyingine ya mwisho utaitawanya kwa upepo. Kwa kuwa nitawafuatia kwa upanga uliofutwa.
Choma theluthi ya tatu ya hiyo kwa moto katikati ya mji wakati siku za kuzingirwa zitakapokamilika, na chukua theluthi ya nywele na uipige kwa panga na kuuzunguka mji. Kisha tawanya theluthi yake kwenye upepo, na nitasogeza panga karibu ili kufukuza watu.
3 Lakini chukua nywele chache uzifungie ndani ya pindo la vazi lako.
Lakini chukua kiasi kidogo cha nywele na zifunge kwenye pindo za nguo yako.
4 Tena chukua nywele nyingine chache uzitupe motoni uziteketeze. Moto utaenea kutoka humo na kufika katika nyumba yote ya Israeli.
Kisha chukua tena zile nyewele na zitupe katikati ya moto; na zichome kwenye moto; kutoka hapo utatoka nje kwenda nyumba zote za Israeli.”
5 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Huu ndio Yerusalemu ambao nimeuweka katikati ya mataifa ukiwa umezungukwa na nchi pande zote.
Bwana Yahwe asema hivi, “Hii ndio Yerusalemu katikati ya mataifa, nilipomuweka, na ambapo nilipomzunguka kwa nchi zingine.
6 Lakini katika uovu wake umeasi sheria na amri zangu kuliko mataifa na nchi zinazouzunguka. Umeasi sheria zangu wala haukufuata amri zangu.
Lakini anaudhaifu wa kukataa amri zangu zaidi kuliko mataifa yalivyo, na sheria yangu zaidi kuliko mataifa ambayo yanayomzunguka. Watu wamezikataa humuku zangu na kuacha kutembea katika sheria zangu.”
7 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ninyi mmekuwa wakaidi kuliko mataifa yanayowazunguka na hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu. Wala hamkuweza hata kuzifuata kawaida za mataifa yanayowazunguka.
Kwa hiyo Bwana Yahwe asema hivi, “Kwa sababu mmekuwa kikwazo kuliko mataifa ambayo yanayowazunguka na kuacha kutembea kwenye amri zangu wala kutenda kulingana na amri zangu, wala hata kutenda kulingana na amri za mataifa yanayowazunguka,”
8 “Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo, Mimi mwenyewe, niko kinyume nanyi Yerusalemu, nitawapiga kwa adhabu yangu mbele ya mataifa.
kwa hiyo Bwana asema hivi, “Tazama! Mimi mwenyewe nitatenda juu yenu. Nitato hukumu kati yenu ili mataifa waone.
9 Kwa ajili ya sanamu zenu zote za machukizo, nitawafanyia kile ambacho kamwe sijawafanyia kabla wala kamwe sitawafanyia tena.
Nitawafanyia yale ambayo sijawahi kuyafanya na kile ambacho sintokifanya tena, kwa sababu ya matendo yenu ya kuchukiza.
10 Kwa hiyo katikati yenu baba watakula watoto wao na watoto watakula baba zao. Nitawapiga kwa adhabu, nami nitawatawanya watu wenu walionusurika pande zote za dunia.
Kwa hiyo baba watawala watoto kati yenu, na watoto watawala baba zao, kwa kuwa nitafanya hukumu juu yenu na kuwatawanya kila mahali wote ninyi mliobaki.
11 Kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, kwa kuwa mmenajisi mahali pangu patakatifu kwa sanamu zenu mbaya sana na desturi zenu za machukizo, mimi mwenyewe nitaondoa fadhili zangu kwenu.
Kwa hiyo, kama niishivyo-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo-bila shaka hii ilikuwa kwa sababu umapanajisi patakatifu pangu kwa mambo ya machukizo yako yote na kwa matendo yako yote niyachukiayo, kwamba mimi mwenyewe nitakupunguza katika hesabu; jicho langu halitakuhurumia, na sintoacha kukuharibu.
12 Theluthi ya watu wako watakufa kwa tauni au kwa njaa humu ndani yako, theluthi nyingine itaanguka kwa upanga nje ya kuta zako, nayo theluthi nyingine nitaitawanya kwenye pande nne kuwafuatia kwa upanga uliofutwa.
Theluthi yenu mtakufa kwa tauni, na wataliwa na njaa katikati yenu. Theluthi wataanguka kwa upanga likiwazunguka. Kisha nitawatawanya theluthi katika mahali pote, na nitafuatisha upanga kuwafukuza pia.
13 “Ndipo hasira yangu itakapokoma na ghadhabu yangu dhidi yao itatulia, nami nitakuwa nimelipiza kisasi. Baada ya kuimaliza ghadhabu yangu juu yao, watajua kuwa mimi Bwana nimenena katika wivu wangu.
Hivi ndivyo ghadhabu yangu itavyokamilika, na nitasababisha ghadhabu yangu juu yao hata kulala. Nitajiridhisha, na watajua kwamba, mimi Yahwe, nimenena kwa ghadhabu yangu wakati nitakapo kamilisha ghadhabu yangu dhidi yao.
14 “Nitakuangamiza na kukufanya kitu cha kudharauliwa miongoni mwa mataifa yanayokuzunguka, machoni pa watu wote wapitao karibu nawe.
Nitakufanya mkiwa kwa mataifa yanayokuzunguka kwenye uso wa kila mtu apitaye karibu.
15 Utakuwa kitu cha kudharauliwa na cha aibu, cha dhihaka, ovyo na kitu cha kutisha kwa mataifa yanayokuzunguka, nitakapokupiga kwa adhabu yangu katika hasira na ghadhabu yangu kwa kukukemea kwa ukali. Mimi Bwana nimesema.
Hivyo Yerusalemu itakuwa jambo kwa watu wengine kushutumu na kufanya mzaha, na chukizo kwa mataifa ambayo yanayowazunguka. Nitafanya hukumu dhidi yenu kwa ghadhabu na hasira, na kwa kukemea kwa hasira-Mimi, Yahwe nimesema hivi!
16 Nitakapokupiga kwa mishale yangu ya kufisha na yenye kuharibu ya njaa, nitaipiga ili kukuangamiza. Nitaleta njaa zaidi na zaidi juu yako na kukomesha upatikanaji wa chakula kwako.
Nitatuma mishale mikali ya njaa juu yenu ambayo itakuwa na maana ya kwamba nitawaharibu. Kwa kuwa nitaongeza njaa juu yenu na kuvunja tegemeo lenu la mkate.
17 Nitapeleka njaa na wanyama wa mwituni dhidi yenu, navyo vitawaacha bila watoto. Tauni na umwagaji wa damu utapita katikati yenu, nami nitaleta upanga juu yenu. Mimi Bwana nimenena haya.”
Nitaleta njaa na majanga dhidi yenu hivyo mtakuwa wagumba. Tauni na damu zitapita kati yako, na nitaleta upanga dhidi yenu-Mimi Yahwe, nimesema hivi.”

< Ezekieli 5 >