< Ezekieli 47 >

1 Yule mtu akanirudisha mpaka kwenye ingilio la Hekalu, nami nikaona maji yakitoka chini ya kizingiti cha Hekalu yakitiririkia upande wa mashariki (kwa maana upande wa mbele wa Hekalu ulielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitoka chini upande wa kusini wa Hekalu, kusini mwa madhabahu.
Kisha yule mtu akanirudisha nyuma kwenye lango la kuingia la hekalu, na kulikuwa na maji yakitiririka nje kutoka chini ya hekalu kizingiti cha nyumba kuelekea masharikii-kwa mbele ya hekalu kulekea mashariki-na maji yalikuwa yakitiririka chini upande wa kusini mwa hekalu, kuelekea upande wa kuume wa madhabahu.
2 Ndipo akanitoa nje kupitia lango la kaskazini na kunizungusha mpaka kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nayo maji yalikuwa yakitiririka kutoka upande wa kusini.
Hivyo akanileta kwenye lango la kaskazini na kuniongoza kuzunguka lango kuelekea mashariki, na hapo maji yalikuwa yakitiririka kutoka lango hili kwa upande wa kusini yake.
3 Mtu yule alipokwenda upande wa mashariki akiwa na kamba ya kupimia mkononi mwake, akapima dhiraa 1,000 kisha akanipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kwenye vifundo vya miguu.
Yule mtu alipokuwa akienda mashariki, kulikuwa na kamba ya kupimia kwenye mkono wake; akapima dhiraa elfu moja akanivusha kwenye maji hata maji yakafika kwenye magoti.
4 Akapima dhiraa 1,000 nyingine na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika magotini. Akapima dhiraa nyingine 1,000 na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kiunoni.
Kisha akapima dhiraa elfu moja ten akanivusha kwenye yale maji yaliyofika kwenye magoti; akapima dhiraa elfu kumi nyingine na kunivusha maji yakafika hata kwenye nyonga.
5 Akapima tena dhiraa 1,000 nyingine, lakini wakati huu yalikuwa mto ambao sikuweza kuvuka, kwa kuwa maji yalikuwa na kina kirefu ambacho ni cha kuogelea, mto ambao hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuvuka.
Tena akapima dhiraa elfu moja nyingine, lakini ulikuwa mto ambao sikuweza kuuvuka kwa sababu maji yalizidi na yalijaa maji ya kuogelea ndani-yalikuwa mto usiovukika
6 Akaniuliza, “Je, mwanadamu, unaona hili?” Kisha akanirudisha mpaka kwenye ukingo wa huo mto.
Yule mtu akanambia, “Mwanadamu, unaona hii?” akanipeleka na kunirudisha karibu na ukingo wa mto.
7 Nilipofika pale, nikaona idadi kubwa ya miti kila upande wa ule mto.
Nilipokuwa nikirudi, hapo kwenye ukingo wa mto kulikuwa na miti mingi katika huu upande na upande mwingine pia.
8 Akaniambia, “Haya maji yanatiririka kuelekea nchi ya mashariki na kushuka mpaka Araba, ambapo huingia Baharini. Yanapomwagikia kwenye hiyo Bahari, maji yaliyoko humo huponywa na kuwa safi.
Yule mtu akanambia, “Haya maji yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki na chini hata Araba; haya maji hutiririka kwenye Bahari ya Chumvi itaifanya kuwa mpya.
9 Popote mto huu uendapo kila kiumbe hai kinachoyaparamia hayo maji kitaishi, nako kutakuwa na samaki wengi mno, mara maji haya yafikapo huko. Maji hayo yatakuwa hai na kila kitu kitakachoishi kule mto uendako.
Itakuwa kwamba kila kiumbe hai kisongamanacho kitaishi mahali maji yanapoelekea; kutakuwa na samaki wengi, kwenye hayo maji yatiririkayo huko. Itafanya maji ya chumvi kuwa mapya. Kila kitu kitaishi popote mto utakapoelekea.
10 Wavuvi watasimama kando ya bahari, kuanzia En-Gedi hadi En-Eglaimu huko patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki. Samaki watakuwa wa aina nyingi, kama samaki wa Bahari Kuu
Kisha itatokea kwamba wavuvi wa En Gedi watasimama karibu na maji, na kutakuwa na sehemu ya kutandazia nyavu za samaki karibu na En Eglaimu. Kutakuwa na samaki nyingi za aina tofauti tofauti katika Bahari ya Chumvi, kama samaki kwenye Bahari Kuu kwa wingi wao.
11 Lakini madimbwi yake na mabwawa yake hayatakuwa na maji yanayofaa kunywa, bali yatabakia kuwa maji ya chumvi.
Lakini Bahari ya Chumvi ikajaa maji na matope hayataachwa mapya; yataachwa yawe kwa ajili ya kutengeneza chumvi.
12 Miti ya matunda ya kila aina itaota kwenye kingo zote mbili za mto huu. Majani yake hayatanyauka wala haitaacha kuwa na matunda katika matawi yake. Kila mwezi kutakuwa na matunda, kwa sababu maji yatokayo patakatifu yanaitiririkia. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatakuwa dawa.”
Karibu na huo mto juu ya ukingo wake, pande zote, aina zote za miti utazaa chakula. Majani yake hayatanyauka na matunda yake hayataacha kukua. Kila mwezi miti itazaa matunda, kwa sababu maji kutoka patakatifu yatatirirka kwenda kwenye hiyo miti. Matunda yake yatakuwa kwa ajili ya chakula, na majani yake yatakuwa kwa ajili ya dawa.
13 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “Hii ndiyo mipaka ambayo kwayo mtagawanya hiyo nchi kuwa urithi miongoni mwa hayo makabila kumi na mawili ya Israeli, pamoja na mafungu mawili ya Yosefu.
Bwana Yahwe asema hivi: Hii itakuwa njia ambayo mtaigawanya nchi kwa ajili ya kabila kumi na mbili za Israeli: Yusufu atakuwa na mafungu mawili.
14 Mtagawa kwa usawa miongoni mwao. Kwa sababu niliapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu, nchi hii itakuwa urithi wenu.
Mtaigawa kila mtu sawa sawa ambayo niliinua mkono wangu na kuapa kuwapa baba zenu. Hii nchi itakuja kuwa urithi kwenu.
15 “Huu ndio utakuwa mpaka wa hiyo nchi: “Upande wa kaskazini utaanzia Bahari Kuu kwa njia ya Hethloni kupitia Lebo-Hamathi hadi maingilio ya Sedadi.
Huu utakuwa mpaka wa nchi upande wa kaskazini kutoka Bahari Kubwa kwa njia ya Hethloni, na kisha kuelekea Zedada.
16 Berotha na Sibraimu (ambao uko kwenye mpaka kati ya Dameski na Hamathi), hadi kufikia Haser-Hatikoni, ambao uko katika mpaka wa Haurani.
Kisha mpaka utaenda hata Berotha, hadi Sibraimu, iliyopo kati ya Damaskasi na Hamathi, na kisha hata Hazer-hatikoni, iliyopo karibu na mpaka wa Haurani.
17 Hivyo mpaka utaendelea kuanzia Baharini hadi Hasar-Enoni, ukiambaa na mpaka wa kaskazini wa Dameski, pamoja na mpaka wa Hamathi upande wa kaskazini. Huu utakuwa ndio mpaka wa kaskazini.
Hivyo mpaka utaenda kutoka kwenye bahari hadi Hazar-enoni kwenye mpaka wa Damaskasi na Hamathi hata kaskazini. Huu utakuwa upande wa kaskazini.
18 Upande wa mashariki mpaka utapita kati ya Haurani na Dameski, kuambaa Yordani na kati ya Gileadi na nchi ya Israeli, hadi bahari ya mashariki na kufika Tamari. Huu utakuwa ndio mpaka wa mashariki.
Kwa upande wa mashariki, kati ya Haurani na Damaskasi na kati ya Geliadi na nchi ya Israeli kutakuwa na mto Yordani. Mtapima kutoka kwenye mpaka hata kwenye bahari ya mashariki; huo wote utakuwa mpaka wa mashariki.
19 Upande wa kusini utaanzia Tamari hadi kufikia maji ya Meriba-Kadeshi, kisha utaambaa na Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu. Huu utakuwa ndio mpaka wa kusini.
Kisha upande wa kusini: kusini mwa Tamari hadi kwenye maji ya Meriba Kadeshi, kijito cha Misri hata Bahari Kuu, na upande wa kusini kuelekea kusini.
20 Upande wa magharibi, Bahari Kuu itakuwa ndio mpaka hadi kwenye sehemu mkabala na Lebo-Hamathi. Huu utakuwa ndio mpaka wa magharibi.
Kisha mpaka wa magharibi utakuwa Bahari Kuu utaelekea hata nyuma ya Hamathi. Huu utakuwa upande wa mgharibi.
21 “Mtagawanya nchi hii miongoni mwenu kufuatana na makabila ya Israeli.
Kwa njia hii mtaigawanya hii nchi kwa ajili yenu wenyewe, kwa kabila za Israeli.
22 Mtaigawanya kuwa urithi kwa ajili yenu na kwa ajili ya wageni wanaoishi miongoni mwenu na ambao wana watoto. Wao watakuwa kwenu kama wenyeji wazawa wa Israeli, pamoja na ninyi watagawiwa urithi miongoni mwa makabila ya Israeli.
Hivyo mtagawana urithi kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya wageni walio kati yenu, wale watakaozaa watoto kati yenu na waliokuwa, kati yenu, kama wazaliwa wa watu wa Israeli. Mtapewa urithi miongoni mwa makabila ya Israeli.
23 Katika kabila lolote mgeni atakapoishi hapo ndipo mtakapompatia urithi wake,” asema Bwana Mwenyezi.
Kisha itatokea kwamba wageni watakuwa pamoja na kabila miongoni mwa yule anayeishi. Mtapatia urithi-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.”

< Ezekieli 47 >