< Ezekieli 39 >
1 “Mwanadamu, tabiri dhidi ya Gogu useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ee Gogu mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali.
“Kisha wewe, mwanadamu, tabiri dhidi ya Gogu na sema, 'Bwana Yahwe asema hivi: Tazama! ni kinyume nawe, Gogu, mkuu wa Mesheki na Tubali.
2 Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukuburuta. Nitakuleta kutoka kaskazini ya mbali na kukupeleka wewe dhidi ya milima ya Israeli.
Nitakugeuza na kukuongoza; nitakupandisha juu kutoka mbali kaskazini na kukuleta hata milima ya Israeli.
3 Kisha nitaupiga upinde wako kutoka mkono wako wa kushoto na kuifanya mishale ianguke kutoka mkono wako wa kuume.
Kisha nitaufunga upinde wako utoke katika mkono wako wa kushoto na kuifanya mishale kuanguka kutoka kwenye mkono wako wa kuume.
4 Utaanguka kwenye milima ya Israeli, wewe pamoja na vikosi vyako vyote na yale mataifa yaliyo pamoja nawe. Nitakutoa uwe chakula cha ndege wa aina zote walao nyama na cha wanyama wa mwituni.
Utaanguka juu ya milima ya Israeli-wewe na jeshi lako late na maaskari walio pamoja nawe. Nitawapatia ndege mbua na wanyama pori wa mashambani kwa ajili ya chakula.
5 Utaanguka katika uwanja, kwa kuwa nimenena, asema Bwana Mwenyezi.
Utaanguka juu ya uso wa shamba, kwa kuwa mimi mwenyewe nimesema hivyo-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
6 Nitatuma moto juu ya Magogu na kwa wale wanaoishi kwa salama huko pwani, nao watajua kwamba Mimi ndimi Bwana.
Kisha nitapeleka moto juu ya Magogu na kwa wale waishio salama juu ya pwani, na watajua yakwamba mimi ni Yahwe.
7 “‘Nitalifanya Jina langu takatifu lijulikane miongoni mwa watu wangu Israeli. Sitaliacha tena Jina langu takatifu litiwe unajisi, nayo mataifa watajua kuwa Mimi Bwana ndimi Aliye Mtakatifu wa Israeli.
Kwa kuwa nitalifanya jina langu takatifu lijulikane kati ya watu wangu Israeli, na sitaruhusu tena jina langu takatifu litukanwe; mataifa watajua kwamba mimi ni Yahwe, Mtakatifu katika Israeli.
8 Hili jambo linakuja! Hakika litatokea, asema Bwana Mwenyezi. Hii ndiyo siku ile niliyosema habari zake.
Tazama! Siku inakuja, na itachukua nafasi-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
9 “‘Ndipo wale wanaoishi katika miji ya Israeli watakapotoka na kutumia hizo silaha kuwashia moto na kuziteketeza, yaani, kigao na ngao, pinde na mishale, rungu za vita na mikuki. Kwa miaka saba watavitumia kama kuni.
Hao wakaao katika miji ya Israeli watatoka nje na watatumia silaha kuwasha moto na kutengeneza moto na kuwachoma-ngao ndogo, ngao kubwa, pinde, mishale, rungu, na mikuki; watatengeneza mioto pamoja nao kwa muda wa siku saba.
10 Hawatahitaji kukusanya kuni kutoka mashambani wala kukata kuni kutoka kwenye misitu, kwa sababu watatumia silaha kuwa kuni. Nao watawateka mateka wale waliowateka na kuchukua nyara mali za wale waliochukua mali zao nyara, asema Bwana Mwenyezi.
Hawatakusanya kuni kutoka mashambani wala kukata miti kutoka kwenye misitu, kwa kuwa watazichoma hizo silaha; watawateka nyara wale watakaotaka kuwateka nyara-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.”
11 “‘Siku ile nitampa Gogu mahali pa kuzikia katika Israeli, katika bonde la wale wasafirio upande wa mashariki kuelekea baharini. Jambo hili litazuia njia ya wasafiri kwa sababu Gogu na makundi yake yote ya wajeuri watazikwa huko. Kwa hiyo litaitwa Bonde la Hamon-Gogu.
Kisha itakuwa katika hiyo siku ambayo nitaifanya sehemu huko kwa ajili ya Gogu-kaburi la Israeli, bonde kwa ajili ya wale wanaosafiri hata mashariki ya bahari. Litawazuia wale wanaotegemea kupita. Huko watamzika Gogu pamoja na kundi lake lote. Watapaita bonde la Hamon-Gogu.
12 “‘Kwa miezi saba nyumba ya Israeli itakuwa ikiwazika ili kuisafisha nchi.
Kwa muda wa siku saba nyumba ya Israeli itawazika ili kuitakasa nchi.
13 Watu wote wa nchi watawazika, nayo siku nitakayotukuzwa itakuwa siku ya kumbukumbu kwa ajili yao, asema Bwana Mwenyezi.
Kwa kuwa watu wa nchi watawazika; itakuwa siku ya kukumbukwa kwao wakati nitakapotukuzwa-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
14 “‘Watu wataajiriwa mara kwa mara kuisafisha nchi. Baadhi yao watapita nchini kote na zaidi yao hao wengine, watawazika wale waliosalia juu ya uso wa nchi. Mwisho wa hiyo miezi saba wataanza upekuzi wao.
Kisha watawateua watu kuendelea kwenda kwenye nchi, kuwatafuta wale waliokuwa wakisafiri, lakini waliokufa na miili yao kubaki juu ya uso wa nchi, ili kwamba waweze kuwazika, kwa ajili ya kusafisha nchi. Katika siku ya mwisho ya mwezi wa saba wataanza kutafuta.
15 Wakati wanapopita nchini kote na mmoja wao akaona mfupa wa mwanadamu, ataweka alama kando yake mpaka wachimba kaburi wawe wameuzika katika Bonde la Hamon-Gogu.
Kama hawa watu wapitao kwenye nchi, watakapoona mfupa wowote wa binadamu, wataweka alama kwa huo, hadi wachimba kaburi watakapokuja na kuizika katika bonde la Hamoni Gogu.
16 (Pia mji uitwao Hamona utakuwa humo.) Hivyo ndivyo watakavyoisafisha nchi.’
Kutakuwa na mji huko unaitwa Hamona. Wataitakasa nchi kwa njia hii.
17 “Mwanadamu, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ita kila aina ya ndege na wanyama wote wa mwituni, waambie: ‘Kusanyikeni mje pamoja kutoka pande zote kwa ajili ya dhabihu ninayowaandalia, dhabihu kuu katika milima ya Israeli. Huko mtakula nyama na kunywa damu.
Kwako wewe, mwanadamu, Bwana Yahwe asema hivi: Waambie ndege wote wenye mabawa na wanyama wote wa porini katika mashamba, 'Kusanyikeni pamoja na mje. Kusanyikeni kutoka pande zote kwenda kwenye dhabihu yote ambayo mimi mwenyewe ninayoifanya kwa ajili yako, dhabihu kubwa juu ya milima ya Israeli, ili kwamba mle nyama na kunywa damu.
18 Mtakula nyama za watu mashujaa na kunywa damu za wakuu wa dunia kana kwamba ni za kondoo dume na kondoo wake, mbuzi na mafahali, wote walionona kutoka Bashani.
Mtakula nyama ya walio hodari na kunywa damu ya wakuu wa dunia; watakuwa kondoo waume, wana kondoo, mbuzi, na ng'ombe, wote walikuwa wanene katika Basheni.
19 Katika dhabihu ninayoandaa kwa ajili yenu, mtakula mafuta mpaka mkinai na kunywa damu mpaka mlewe.
Kisha mtakula mafuta hata kuridhika kwenu; mtakunywa damu hadi kulewa; hii itakuwa dhabihu nitakayoichinja kwa ajili yenu.
20 Kwenye meza yangu watajishibisha kwa farasi na wapanda farasi, watu mashujaa na askari wa kila aina,’ asema Bwana Mwenyezi.
Mtatosheka kwenye meza yangu pamoja na farasi, magari ya farasi, shujaa, na kila mtu wa vita-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.'
21 “Nitauonyesha utukufu wangu miongoni mwa mataifa, nayo mataifa yote wataiona adhabu nitakayotoa na mkono wangu nitakaouweka juu yao.
Nitauweka utukufu wangu kati ya mataifa, na mataifa yote yataona hukumu yangu ninayoionyesha na mkono wangu nimeuweka juu yao.
22 Kuanzia siku ile na kuendelea nyumba ya Israeli itajua kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wao.
Nyumba ya Israeli itajua yakwamba mimi ni Yahwe Mungu wao kutoka hiyo siku na kuendelea.
23 Na mataifa watajua kuwa nyumba ya Israeli walikwenda utumwani kwa ajili ya dhambi yao, kwa sababu hawakuwa waaminifu kwangu. Hivyo niliwaficha uso wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao, nao wote wakaanguka kwa upanga.
Mataifa yatajua kwamba nyumba ya Israeli wameenda uhamishoni kwa sababu ya udhalimu wao kwa kunisaliti, hivyo naficha uso wangu kwao na kuwaweka kwenye mkono wa maadui zao ili kwamba wote waanguke kwa upanga.
24 Niliwatendea sawasawa na uchafu wao na makosa yao, nami nikawaficha uso wangu.
Nimewafanyia kutokana na uchafu wao na dhambi zao, nitakapokuwa nimeuficha uso wangu kwao.
25 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Sasa nitamrudisha Yakobo kutoka utumwani, nami nitawahurumia watu wote wa Israeli, nami nitakuwa na wivu kwa ajili ya Jina langu takatifu.
Kwa hiyo Bwana Yahwe asema hivi: Sasa nitawarudisha watu wa Yakobo, na kuwa na huruma juu ya nyumba yote ya Israeli, wakati nitakapoona wivu kwa ajili ya jina langu.
26 Wataisahau aibu yao na jinsi walivyoonyesha kutokuwa waaminifu kwangu mimi wakati waliishi salama katika nchi yao, bila kuwa na mtu yeyote wa kuwatia hofu.
Kisha watabeba aibu yao na uhaini mkubwa walio nihaini. Watayasahau haya yote watakapopumzika katika nchi yao katika usalama, wala hakuna mtu atakaye waogofya.
27 Nitakapokuwa nimewarudisha kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi za adui zao, mimi nitajionyesha kuwa mtakatifu kwa kupitia kwao machoni mwa mataifa mengi.
Wakati nitakapokuwa nimewarudisha kutoka kwa watu na kuwakusanya kutoka kwenye nchi za maadui zao, nitajionyesha mimi mwenyewe kuwa mtakatifu kwenye uso wa mataifa mengi.
28 Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wao, ingawa niliwapeleka uhamishoni miongoni mwa mataifa, nitawakusanya tena katika nchi yao wenyewe, bila kumwacha yeyote nyuma.
Kisha watajua kwamba mimi ni Yahwe Mungu wao, kwa kuwa nimewapeleka utumwani kati ya mataifa, lakini kisha nitawakusanya kuwarudisha hata nchi yao. Sitamuacha hata mmoja wao kati ya mataifa.
29 Sitawaficha tena uso wangu, kwa maana nitamimina Roho wangu juu ya nyumba ya Israeli, asema Bwana Mwenyezi.”
Sitawaficha uso wangu kwao wakati nitakapomwaga Roho wangu katika nyumba ya Israeli-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.”